Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukimshangaa Job pale Yanga, unakutana na Nangu Simba

JICHO Pict

Muktasari:

  • Halafu ghafla ameibuka beki wa kati wa Simba na timu ya taifa, Wilson Nangu.

HAPO mitaa ya kati watu waliwahi kuleta mjadala wa kimo cha mlinzi wa kati wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Dickson Job. Ni beki wa kati ambaye kwa kimo ni mfupi. Mara nyingi nafasi hiyo pamoja na ile ya kipa huwa inachezwa na wachezaji wenye vimo virefu.

Halafu ghafla ameibuka beki wa kati wa Simba na timu ya taifa, Wilson Nangu.

Naye ni mfupi kama alivyo Job. Simba walimchukua kutoka JKT Tanzania dirisha kubwa lililopita la majira ya joto. Kila siku ameendelea kuimarika katika kikosi cha Simba.

Zamani ilikuwa nadra kuwa beki wa kati halafu una kimo kifupi. Kwa wenzetu wazungu pia ni nadra kukutana na hali hii na ndiyo maana mabeki wao ni warefu kama Gabriel Magalhaes wa Arsenal. Wale ndio waliokuwa na maumbo ya kina Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’.

JIC 01

Miongoni mwa mabeki wa kati waliokuwa na maumbo mafupi ni pamoja na Fabio Cannavaro wa Italia. Hata hivyo, wenyewe wanakiri Cannavaro alikuwa na faida ya kuwa na kipaji cha kuruka hewani. Hasara za kuwa mfupi zilikuwa zinafidiwa na uwezo wake wa ajabu wa kuruka juu.

Hapa Tanzania tumewahi kuwa na George Magere Masatu. Alikuwa mfupi, lakini alibebwa sana na uwezo wake wa kutumia akili akiwa kama mtu mwisho. Sikumbuki kama Masatu alikuwa na uwezo mkubwa wa kuruka hewani, lakini alikuwa na kipaji kikubwa cha kuusoma mchezo katika eneo la lango lake.

Pamoja na uwezo wake huo bado makocha wazungu hawakumiani sana. Kuna kocha mmoja mzungu alikuja kutoka Brazil kufundisha timu ya taifa akaamua kumhamisha Masatu kutoka nafasi ya beki wa kati kwenda kuwa beki wa kulia.

JIC 02

Kocha huyo akaamua kumchukua beki wa klabu ya Sigara, Abuu Juma kuwa beki wa kati ingawa hayakuwa maamuzi yaliyopendwa na Watanzania kwa sababu walishangaa kumuona kipenzi chao Masatu akicheza kama beki wa kulia.

Lakini leo tuna Dickson Job. Halafu ghafla amekuja Nangu ambaye nimekuwa nikimuangalia mara kadhaa. Kwa nini wote ni bora? Nadhani wanaficha madhaifu ya vimo vyao kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kuruka hewani. Job na Nangu wana uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya hewani licha ya maumbile yao.

Kwa nini tumefika hapa? Kitu cha kwanza kabisa ni ukweli labda hatuzalishi walinzi wa kati ambao wanaweza kuwafanya kina Job wakimbie nafasi zao kwenda pembeni. Na hapa kuna mambo mawili ya msingi.

JIC 03

Jambo la kwanza kabisa tumepoteza wachezaji wenye maumbo makubwa. Tazama picha za wachezaji wa zamani wa Tanzania utagundua kwamba walikuwa wana maumbo makubwa. Na sio wachezaji tu, hata wanadamu wa zamani katika nchi ya Tanzania walikuwa na maumbo makubwa.

Haishangazi kuona zamani klabu mbalimbali za Ligi Kuu zilikuwa zina wachezaji ambao walikuwa wanasoma sekondari. Nilisoma sekondari ya Jitegemee na Renatus Njohole na Ally Mayay wakati walipokuwa wanachezea Simba na Yanga. Leo sioni uwezekano wa mwanafunzi wa sekondari kucheza Ligi Kuu.

Lakini pili katika hili hili la maumbo nadhani hatuzalishi mabeki wa kati wenye maumbo marefu na wenye akili ambao wanaweza kuwaondoa kina Job katika nafasi hizi na kuwarudisha katika nafasi za pembeni.

JIC 04

Zamani kulikuwa na wachezaji warefu mahiri katika nafasi hizi kiasi kwamba vijana wenye urefu wa kina Job hawakufikiria kucheza katikati.

Ni kama tunavyoona sasa hivi kule Ulaya. Mabeki wa kati ni warefu na wana akili ya kucheza katika maeneo hayo kiasi kwamba ni nadra kujitokeza mchezaji kama Cannavaro kucheza katika nafasi zao. Sisi wanaendelea kujitokeza kila kukicha.

Hata katika nafasi ya langoni tumepoteza sifa hiyo. Maumbo ya wachezaji wetu yamekwenda wapi? Hata katika nafasi ya ushambuliaji tunamuona Clement Mzize kama mchezaji mwenye umbo kubwa wakati katikati hali halisi sio mshambuliaji mwenye umbo tishio kuliko baadhi ya wachezaji wetu waliopita katika eneo hilo.

JIC 05

Ninachokiona kwa sasa ukiwa beki mwenye akili una nafasi kubwa ya kuchagua kucheza nafasi yoyote ya nyuma kwa sababu wanaostahili kucheza katika nafasi hizo hawapo.

Hatuwazalishi tena tofauti na wakati ule ambao tulikuwa tunawazalisha kina Mustapha Hoza.

Na kama utachunguza zaidi utagundua katika miaka ya karibuni tumekuwa tukipeleka wachezaji wengi wa nafasi nyingi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini sio mabeki wa kati. Wamekwenda kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Novatus Dismas, Kelvin John na wengineo.

Katika nafasi ya beki wa kati au katika nafasi ya kipa tunakosa vigezo kwa sababu ya vimo. Na kuna baadhi ya makipa naamini wapo nchini na wanamudu kucheza na kutamba kwa sababu ya vimo vyao.

JIC 06

Mmojawapo ni Djigui Diarra. Kama angekuwa mrefu nadhani sasa hivi angekuwa anadaka katika nchi za Ulaya. Ana kipaji kikubwa lakini wenzetu wanaangalia zaidi masuala ya vimo.

Nini kifanyike? Nadhani Marcio Maximo wakati ule alipokuja kuwa kocha wa timu ya taifa alianza kuhamasisha kuangalia vimo katika baadhi ya nafasi. Hilo hata Florent Ibenge anadaiwa amekuwa akilikomalia Azam FC.

Nasi inabidi tuwekeze katika sayansi hii. Tatizo kubwa hatuwekezi katika sayansi hii kwa sababu hatuwafundishi watoto wetu mpira tangu wakiwa wadogo.

Lakini tatizo jingine la msingi ni hata warefu wenyewe hawana vipaji vya kina Dickson Job. Kipaji ni kitu ambacho hafundishwi mtu.

Tatizo linaanzia hapo.

Na katika hili sio mabeki wa kati tu bali maeneo mengi ya ndani ya uwanja yanaendelea kukosa vipaji kama ilivyokuwa zamani.