Uhondo wa AFCON 2025 unaanza hivi
Muktasari:
- Mataifa 24 yatashuka uwanjani kusaka ubingwa wa taji hilo katika mashindano ya Afcon yatakayokuwa ya 35, ambapo kivumbi chake kitaanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.
RABAT, MOROCCO: NGOJA tuone. Ndicho unachoweza kusema kwa sasa, wakati mashindano ya kusaka ubingwa wa Afrika yakianza huko Morocco, Jumapili.
Mataifa 24 yatashuka uwanjani kusaka ubingwa wa taji hilo katika mashindano ya Afcon yatakayokuwa ya 35, ambapo kivumbi chake kitaanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.
Ivory Coast yenye sura kibao za kazi kwenye kikosi chaoke watakwenda kwenye mashindano hayo kujaribu kutetea ubingwa huo waliobeba kwenye fainali zilizopita. Watatoboa?
Wakati mashabiki wa soka wa hapa nchini wakisubiri kuona kikosi chao cha Taifa Stars kilichopangwa kwenye Kundi C kitakwenda kufanya nini kwenye mashindano ya Afcon 2025, makala haya yanahusu uchambuzi wa kila kundi na ubora wa timu zake katika msako wa ubingwa.
Kundi A: Morocco, Mali, Zambia, Komoros
Morocco ndio wenyeji wa AFCON 2025 wakifanya hivyo kwa mara ya kwanza tangu 1988, baada ya kujiondoa kuandaa mashindano ya mwaka 2015 kutokana na janga la Ebola.
Wanapojiandaa kuwa taifa la pili barani Afrika kuandaa Kombe la Dunia 2030, wamewekeza pakubwa katika miundombinu ya kiwango cha dunia pamoja na kujenga kikosi imara.
Kwa sasa, Morocco ndio taifa lenye nafasi ya juu zaidi katika viwango vya FIFA kati ya washiriki na wanatajwa waziwazi kama wagombea wakuu wa ubingwa kwenye Afcon 2025.
Kocha mkuu, Walid Regragui ana rekodi nzuri, lakini doa pekee ni kuondolewa katika hatua ya 16 bora kwenye AFCON iliyopita. Akiwa na kikosi kilichojaa wachezaji wa kiwango cha juu, atalenga kubadili hilo nyumbani na kutwaa taji la pili la Afcon.
Mpinzani mkubwa wa Morocco kwenye kundi hili inaonekana kuwa Mali. Timu hiyo inanolewa na kocha Mbelgiji mwenye mzoefu, Tom Saintfelt, ambaye amefanya kazi katika klabu za nchi tisa tofauti wakiwamo mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga na amefundisha timu za taifa 13.
Ana sifa ya kufanya vizuri zaidi ya matarajio na timu zisizopewa nafasi kubwa katika AFCON, hivyo Mali wanaamini anaweza kuwaongoza vijana wao wenye vipaji hadi hatua ya mtoano.
Zambia iliongoza kundi lake la kufuzu AFCON mbele ya mabingwa watetezi Ivory Coast, lakini walimwachisha kazi kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant miezi michache kabla ya mashindano kufuatia matokeo mabaya kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Msaidizi wake wa zamani, Moses Sichone amepandishwa kuwa kocha mkuu, na macho yote yatakuwa kwake kuona kama anaweza kuwaongoza Chipolopolo kufika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza tangu ubingwa wao wa kihistoria wa AFCON walioupata mwaka 2012.
Comoros ni kati ya timu zilizo na nafasi ya chini zaidi katika AFCON hii, ikishiriki kwa mara ya pili tu. Idadi ya watu wa taifa hilo isiyofikia milioni moja inawafanya kuwa nchi ndogo zaidi kwenye mashindano haya.
Kiungo Youssouf M’Changama, Zaydou Youssouf na winga Faïz Selemani wanatarajiwa kuwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Stefano Cusin.
Kundi B: Misri, Afrika Kusini, Angola, Zimbabwe
Misri ni timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya AFCON wakiwa na mataji saba, lakini hawajaongeza taji tangu mwaka 2010.
Wakishindwa kushinda safari hii, watakuwa wameweka rekodi ya ukame wao mrefu zaidi wa ubingwa. Macho yote yatakuwa kwa Mohamed Salah, ambaye bado anatafuta taji lake la kwanza la kimataifa. Omar Marmoush na Mostafa Mohamed ndio wenzake pekee wanaocheza Ulaya.
Kocha Hossam Hassan atategemea uzoefu wa kikosi chake kuvuka kundi hili gumu na kusonga mbele dhidi ya timu zenye vipaji zaidi katika hatua ya mtoano.
Afrika Kusini wana muundo wa kikosi unaofanana, wakiwa na wachezaji sita kutoka Ulaya na wawili Saudi Arabia, huku wengine wakicheza ligi ya nyumbani.
Wanajulikana kwa nidhamu ya kimbinu chini ya kocha mkongwe Hugo Broos, aliyewaongoza kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye AFCON iliyopita. Bafana Bafana wanalenga kufanya safari ndefu tena na watakuwa wapinzani wagumu kwa timu yoyote.
Angola imekuwa ikifanya vizuri zaidi ya matarajio katika miaka ya hivi karibuni, lakini ilishindwa kuendeleza hilo kwenye kufuzu Kombe la Dunia ilipomaliza katika nafasi ya nne kwenye kundi lake. Itarejea AFCON ikitaka kufufua mafanikio, baada ya kufika robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake kwenye toleo lililopita.
Mabadiliko makubwa ni kocha Patrice Beaumelle aliyechukua nafasi ya Pedro Gonçalves.
Zimbabwe haijawahi kufika hatua ya mtoano katika ushiriki wake mara tano zilizopita AFCON. Hilo litahitaji juhudi kubwa, hasa baada ya kushindwa kushinda mechi yoyote kati ya 10 za kufuzu Kombe la Dunia na kumteua kocha mpya Mario Marinica mwezi mmoja tu kabla ya mashindano. Kukosekana kwa kiungo wa Wolves, Marshall Munetsi kutokana na majeraha pia kumeibua mjadala.
Kundi C: Nigeria, Tunisia, Uganda, Tanzania
Nigeria, washindi wa pili wa AFCON iliyopita, wanatafuta kulipiza kisasi si tu kwa kipigo dhidi ya Ivory Coast bali pia kwa kushindwa kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Kama kawaida, wana wingi wa machaguo katika safu ya ushambuliaji akiwamo Victor Osimhen na Ademola Lookman, huku Tolu Arokodare na Victor Boniface wakiachwa nje. Changamoto kubwa bado ni kusawazisha safu ya kiungo.
Tunisia chini ya Sami Trabelsi ni timu ambayo hakuna anayependa kukutana nayo kutokana na mtindo wao wa ulinzi thabiti lakini wenye mafanikio.
Walimaliza kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia bila kuruhusu bao katika mechi 10.
Hata hivyo, ukosefu wa makali ya ushambuliaji uliwafanya waondoke mapema AFCON iliyopita, hivyo watatarajia mchango mkubwa kutoka kwa washambuliaji wao.
Uganda ilifanya kampeni nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia ikimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Algeria.
Kocha Paul Put amechagua wachezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani, wakiwamo Marekani, Thailand, Tanzania, Rwanda, Romania, Czechia na Burton Albion ya England, na kuunda kikosi chenye mchanganyiko mkubwa.
Tanzania imefuzu AFCON kwa mara ya tatu katika matoleo yake manne yaliyopita na tayari imehakikishiwa nafasi kwenye AFCON ijayo kama waandaaji wenza pamoja na Kenya na Uganda.
Bado haijawahi kushinda mechi ya hatua ya makundi, hivyo hilo litakuwa lengo kuu la kocha mpya Miguel Gamondi, ambaye ana uzoefu mkubwa barani Afrika licha ya kuwa hii ni mara yake ya kwanza kuinoa timu ya taifa.
Kundi D: Senegal, DR Congo, Benin, Botswana
Mabingwa wa AFCON 2021, Senegal walitolewa hatua ya 16 bora kwenye toleo lililopita baada ya kufungwa kwa penalti na mabingwa wa mwisho, Ivory Coast.
Pape Thiaw, aliyechukua nafasi ya Aliou Cisse, alianza vyema kwa kuiongoza Senegal bila kupoteza mechi kwenye kufuzu Kombe la Dunia.
Haya yatakuwa mashindano yake makubwa ya kwanza, lakini Senegal haijapoteza mechi 23 mfululizo za mashindano rasmi, na ina kikosi kilichoenea vizuri.
DR Congo ilionyesha ushindani mkubwa dhidi ya Senegal katika kufuzu Kombe la Dunia na hatimaye ikafuzu michezo ya mchujo wa kimataifa mbele ya Cameroon na Nigeria.
Walifika nusu fainali AFCON iliyopita licha ya kushinda mechi moja tu, na huenda wakalazimika kufanya hivyo tena bila mshambuliaji Yoane Wissa.
Benin wanarejea AFCON baada ya kukosa matoleo mawili yaliyopita, ikiwa ni ushiriki wao wa nne.
Licha ya kufika robo fainali mwaka 2019, bado hawajawahi kushinda mechi AFCON. Chini ya Gernot Rohr, wana nafasi nzuri ya kubadili historia hiyo, wakimtegemea Aiyegun Tosin, Steve Mounie na Andreas Hountondji.
Botswana ndio timu yenye nafasi ya chini zaidi kwenye viwango vya FIFA katika AFCON hii, wakishiriki kwa mara ya pili tu tangu 2012. Ushindi wao wa 1–0 dhidi ya Cape Verde uliwapa tiketi, lakini kikosi chao kinachotegemea sana ligi ya nyumbani kinakabiliwa na changamoto kubwa.
Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Sudan
Algeria kwa kawaida huonekana kati ya wapigania taji, lakini lengo lao la kwanza ni kuvuka hatua ya makundi baada ya kuondolewa mapema mara mbili mfululizo.
Vladimir Petkovic ameiongoza timu vizuri kwenye kufuzu, lakini sasa anakabiliwa na changamoto ya kuficha udhaifu wa ulinzi na kutumia ipasavyo vipaji vingi vya ushambuliaji.
Burkina Faso imefika hatua ya mtoano katika AFCON nne kati ya tano zilizopita, ikifika nusu fainali mara tatu tangu 2013. Kocha Brama Traore anaiongoza kwa mara ya kwanza, akichanganya wachezaji wazoefu kama Bertrand Traore, Edmond Tapsoba na Herve Koffi pamoja na vijana kama Dango Ouattara na Cyriaque Irie.
Equatorial Guinea walifanya mshangao mkubwa kwenye AFCON iliyopita walipoongoza kundi mbele ya Nigeria na Ivory Coast.
Wamefika hatua ya mtoano katika kila ushiriki wao mara minne zilizopit.
Migogoro ya ndani kuhusu kocha Juan Micha na masuala ya kifedha imeleta changamoto, lakini bado wana ubora wa kutosha kushindana.
Sudan walifanya kampeni ya kushangaza ya kufuzu AFCON, wakimaliza nafasi ya pili mbele ya Ghana, iliyomaliza mkiani. Mafanikio haya yamepatikana huku nchi yao ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, hivyo michezo yao itakuwa na maana kubwa zaidi ya soka pekee.
Kundi F: Ivory Coast, Cameroon, Gabon, Msumbiji
Ivory Coast ni mabingwa watetezi baada ya kutwaa taji lao la tatu kupitia mojawapo ya kampeni za kushangaza zaidi katika historia ya AFCON. Kocha Emerse Faé alipewa mkataba wa muda mrefu na sasa analenga kutetea taji kikamilifu.
Fae amefanya maamuzi ya ujasiri kwa kuwaacha nje Nicolas Pepe na Simon Adingra, akiwapa nafasi vijana Yan Diomande na Bazoumana Toure. Licha ya hilo, Tembo wa Afrika wana mchanganyiko mzuri wa uzoefu na ubora.
Cameroon ni nguli wa AFCON wakiwa na mataji matano, lakini wanakabiliwa na migogoro ya ndani kuhusu uongozi na kikosi. Mgogoro huo unahusisha kocha Marc Brys na Rais wa Shirikisho Samuel Eto’o, huku David Pagou akionekana kuongoza timu mashindanoni.
Gabon wanarejea AFCON wakiongozwa na Pierre-Emerick Aubameyang, huenda ikiwa ni mashindano yake makubwa ya mwisho. Denis Bouanga na Mario Lemina pia ni miongoni mwa wachezaji wazoefu, hivyo hii ni fursa ya mwisho kwa kizazi hiki kuacha alama.
Msumbiji inatafuta ushindi wake wa kwanza AFCON katika ushiriki wake wa sita.
Kikosi kimebakia karibu kilekile, na iwapo Domingues mwenye umri wa miaka 42 atacheza, ataweka rekodi ya kuwa mchezaji wa nafasi za ndani uwanjani mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya AFCON.
Kwa nafasi la kipa, mchezaji mzee zaidi ni kipa wa timu ya taifa ya Misri, Essam El Hadary aliyedaka akiwa na umri wa miaka 43, miezi mine na siku 20.