Kizunguzungu cha mechi ya kwanza AFCON
Muktasari:
- Katika mechi zote isipokuwa moja tu za ufunguzi za mashindano 34 yaliyopita kwenye Afcon yaliyohusisha timu mwenyeji, historia inaonyesha mchezo kwao hutuzwa.
RABAT, MOROCCO: MECHI za ufunguzi kwenye AFCON mara zote zinakuwa tamu kwa wenyeji. Je, Morocco itaendeleza utamaduni?
Katika mechi zote isipokuwa moja tu za ufunguzi za mashindano 34 yaliyopita kwenye Afcon yaliyohusisha timu mwenyeji, historia inaonyesha mchezo kwao hutuzwa.
Wakati Morocco ikijiandaa na mechi ya kuwakabili Comoros kwenye mechi ya ufunguzi ya mashindano ya Afcon 2025 huko Rabat, Jumapili matumaini ya wengi ni timu mwenyeji ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Kocha wa Morocco, Walid Regragui ameteua kikosi chenye mastaa wa maana kabisa akiwamo Achraf Hakimi, Yassine Bounou, Sofyan Amrabat na straika Youssef En-Nesyri. Hata hivyo, Hakimi hatacheza mechi ya ufunguzi na kwamba Noussair Mazraoui anaweza kuziba pengo lake, huku kwenye sehemu ya kiungo kuna mastaa makini kama Azzedine Ounahi.
Hii itakuwa mechi ya tano kwa Morocco kucheza na Comoros, huku kikosi cha Simba wa Atlas kikishinda mara tatu na kutoka sare moja, huku Comoros ikiishindwa kupata ushindi hata mara moja.
Hivyo, kwa rekodi hiyo, mzani umeegemea upande mmoja. Mechi tatu kati ya hizo ni za mashindano ya Afcon. Mechi ya kipindi cha karibuni kukutana ilikuwa Desemba 2 kwenye Arab Cup, ambapo Morocco ilishinda 3–1, licha ya kwamba wachezaji wengi waliocheza mashindano hayo hawatacheza kwenye hii mechi.
Tangu mashindano ya mwanzo kabisa, 1957, kuna mechi 19 za ufunguzi zilizoshuhudia timu mwenyeji ikishinda, huku mara tano tu ndiyo zilikuwa na matokeo ya mwenyeji kupoteza na tisa zilimalizika kwa sare.
Mara pekee, ambapo mechi ya ufunguzi haukushuhudia timu mwenyeji ilikuwa 1970 na Cameroon na Ivory Coast zilimenyana kwenye mechi ya kwanza katika mashindano yaliyofanyika Sudan. Sambamba na hilo, mechi ya ufunguzi ya kwanza kabisa kwenye Afcon ilimalizika kwa timu mwenyeji kuchapwa, wakati Sudan ilipokung’utwa 2–1 na Misri huko Khartoum mwaka 1957 na timu tatu tu zilishiriki.
Na baada ya hapo, ilichukua miongo mitatu kwa timu mwenyeji kukumbana na kipigo katika mechi ya ufunguzi.
Hiyo ilikuwa Cairo mwaka 1986, wakati Senegal ilipoichapa Misri 1–0. Licha ya kupoteza mechi ya ufunguzi, Misri ilibadilika mechi zilizofuatia na kwenda kunyakua ubingwa, ikiichapa Cameroon kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti.
Senegal ilipokuwa mwenyeji 1992, ilikumbana na kipigo cha mabao 2–1 mbele ya Nigeria huko Dakar, wakati Tunisia nao 1994 walikumbana na kipigo cha mabao 2–0 mbele ya Mali uwanjani El Menzah na kocha Youssef Zouaoui alitimuliwa.
Burkina Faso ni timu ya karibuni mwenyeji kupoteza mechi ya ufunguzi, wakati ilipochapwa 1–0 na Cameroon huko Ouagadougou mwaka 1998. Hata hivyo, wenyeji hao walijitahidi na kufika nusu fainali ya michuano hiyo.
Ushindi mnono zaidi kwa timu mwenyeji unabaki kuwa ile wa Algeria iliposhinda 5–1 dhidi ya Nigeria mjini Algiers mwaka 1990. Timu hizo mbili zilikutana tena fainali na Algeria iliichapa Super Eagles kwa tofauti ya bao moja tu.
Ushindi mwingine mkubwa kwa timu mwenyeji ni ule uliopata Tunisia wa mabao 4–0 dhidi ya Ethiopia mwaka 1965, Ivory Coast 3–0 dhidi ya Togo katika mechi ya ufunguzi na Afrika Kusini 3–0 dhidi Cameroon wakati wanaelekea kushinda ubingwa huo mwaka 1996.
Tukio la kushangaza zaidi kwenye mechi ya ufunguzi ya Afcon ilikuwa 2010, wakati Angola ilipopoteza uongozi wake wa mabao nne katika dakika 11 za mwisho wakati Mali ilipotokea nyuma na kufanya ubao usomeke 4–4 mjini Luanda.
Wakati Morocco ilipokuwa mwenyeji wa mashindano hayo 1988, iliruhusu uongozi wao wa bao la kipindi cha kwanza dhidi ya Zaire, sasa DR Congo kupotea baada ya kusawazishiwa katika dakika tatu za mwisho.
Safari hii, Morocco inataka kurudi kivingine kama timu mwenyeji wa Afcon 2025 ikiwa ni mashindano ya 35 kwenye mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Comoros.