Prime
Tutafika mbinguni na Fei Toto tukiwa tumechoka hasa
MPAKA siku Fei Toto atakapotambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga au Simba ndipo roho za mashabiki wa mpira nchini zitakapotulia. Fei anahangaisha mioyo ya mashabiki, viongozi wa hizi timu pamoja na wachambuzi wa mitandaoni ambao wanajishughulisha na udaku wa tetesi za uhamisho.
Ndani yake kuna mambo mengi. Mashabiki wanajinasibu kwamba wamempata Fei. Viongozi nao majuzi waliamua kuitenga jezi namba 6 kama kete ya kuingiza mashabiki wengi katika mechi zao za mabonanza.
Iliwekwa mitego mingi mitandaoni kama vile timu moja kati ya hizi ilikuwa inajiandaa kumtambulisha Fei. Aibu iliyoje. Fei mwenyewe yupo Kigali na timu yake ya Azam akijiandaa na msimu mpya wa michuano mbalimbali.
Kitu kinachotusumbua ni kwamba hatujakubali kwamba Azam ni timu kubwa ambayo inaweza kuwa na Fei au inastahili kuwa na Fei. Zamani tulikuwa tunajidanganya kwamba ili Simba na Yanga zipate upinzani, basi ni lazima zitokee timu kubwa zenye nguvu nchini kwa ajili ya kuwapa changamoto.
Familia ya Bakhressa ikaanzisha Klabu ya Azam na imekuwa ikiwekeza kwa wachezaji wakubwa, lakini bado hatuipendi ‘project’ yao. Hatuamini kwamba Azam ni wakubwa na wanastahili kuwa na wachezaji wakubwa.
Kumbe wakati huo tukitamani ije timu kubwa nchini bado yale yalikuwa mawazo ya kinafiki. Bado akili zetu zipo kwa Simba na Yanga tu. Ndio maana hatuamini kwamba Fei yupo katika timu ambayo anastahili.
Kule kwa wenzetu mbona timu nzuri za kawaida zinamiliki wachezaji wazuri? Mbona Atletico Madrid inamiliki wachezaji wazuri? Mbona Tottenham Hostpurs inamiliki wachezaji wazuri? Mbona Lille inamiliki wachezaji wazuri?
Matokeo yake kinachotokea kwa sasa ni kwamba tunaikosea heshima katika kiwango ambacho tusingezikosea heshima Simba na Yanga. Tunapenda kumzungumzia mchezaji ambaye ana mkataba na timu yake.
Kama hili lingekuwa linazungumzwa dhidi ya Rushine De Reauck au Dickson Job jibu lingekuwa lile maarufu “tuna mkataba naye”. Lakini hatutaki kukubali kwamba hata Fei ana mkataba na Azam. Na jambo hili linachagizwa zaidi na ukimya wa watu wa Azam.
Pale Azam kuna matajiri, halafu kuna viongozi kama Abdulkarim Amin ‘Poppat’, na kuna wasemaji. Wote hawa sio watu wanaojishughulisha sana na kujibu tetesi za kila siku za kuhusu Fei na wachezaji wengi. Labda kwa sababu timu yao haina mashabiki wengi ambao wangehitaji ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya klabu.
Matokeo yake huwa wanakaa kimya tu. Hata hivyo ilitokea hivi hivi katika dirisha kubwa lililopita la uhamisho. Fei alihusishwa kuondoka kama hivi lakini jioni moja ghafla tukamuona anasaini mkataba mpya na klabu yake. Mashabiki na mabosi wa Simba na Yanga waliishia kusonya tu.
Kitu kingine katika hili ni kwamba nazipenda pia tabia binafsi za Fei. Huwa hana presha katika jambo lenyewe. Sio tu katika jambo hili, lakini Feisal mwenyewe ana tabia za kutojali sana mambo na kupenda mambo ya utani zaidi.
Kwa kiasi fulani hili linaiweka salama timu yake. Hata msimu uliopita kabla hajasaini mkataba mpya alikuwa kimya kama hivi ingawa watu walipandikiza maneno mengi kuhusu yeye kwamba amekubali kusaini Simba au Yanga.
Ni kama ilivyo sasa. Tunasikia tu kutoka kwa kina ‘Fabrizio Romano’ wetu kwamba tayari Fei amefikia makubaliano binafsi na Yanga. Tunasikia tu kwamba amefikia makubaliano binafsi na Simba. Mwenyewe yupo kimya, Poppat yupo kimya. Wasemaji wa timu wapo kimya.
Unajaribu kuwaza tu. Familia ya Bakhresa ni tajiri. Ina uwezo wa kummiliki Fei. Kwa sasa wamesajili vifaa kama saba hivi vya kigeni. Iweje wao waje halafu Fei aruhusiwe kuondoka katika mlango huo huo? Itakuwa wanajenga timu au wanafanya masihara.
Nadhani ni bora kuacha uvivu tu wa kusaka wachezaji mahiri katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Watanzania wakianza kumjengea mchezaji mazingira ya kumchukua unaweza kudhani mchezaji mwenyewe ni Zinedine Zidane. Wanapeleka presha kubwa isiyo ya kawaida.
Yanga wamewahi kufika fainali za Shirikisho Afrika bila ya Fei. Simba hawajawahi kumvalisha Fei jezi yao lakini wamefika fainali hizo bila ya Fei. Hata hivyo tunatengenezewa mazingira kwamba Fei ni kila kitu. Na kuna presha ambayo haina maana mashabiki wamejipa kuhusu Fei.
Kwa mfano, kuna mashabiki wa Yanga juzi walikuwa wanaulaumu uongozi wa klabu yao kwa kutomtambulisha Fei. Walijitengenezea hadithi kichwani kwamba jezi namba 6 ilikuwa inamsubiri Fei Toto. Iweje Fei awe Kigali halafu atambulishwe Temeke? Ni nani hasa aliyewaambia kwamba jezi hiyo ilikuwa inamgonja Fei?
Kuna simulizi nyingine ya kutunga ambayo nimeisikia mahala kwamba kuna mwanasiasa mmoja mkubwa alitumwa na uongozi wa Simba ili akaongee na Mzee Bakhresa aruhusu awape Fei. Nikaishia kuchoka.
Fei atafika mbinguni akiwa amechoka. Nahisi tu kwamba siku moja anaweza kurudi Yanga au kucheza Simba, lakini hadi siku hiyo ifike, yeye mwenyewe pamoja na mashabiki watakuwa wamechoka hasa.
Tetesi zake za usajili na picha yake iliyoambatana na logo za Simba na Yanga imetukimbiza mbio ndefu za marathoni kila dirisha la uhamisho likikaribia. Baada ya yeye kusaini mkataba mpya na Azam sikutazamia kama katika dirisha hili tungerudi na habari zake, lakini hauwezi kuamini kwamba tumerudi tena na habari zake.