Prime
Tusahau hatuwezi kumpata Ronaldinho mwingine
MTU mmoja aliniuliza kama tunaweza kumpata Ronaldinho Gaucho mwingine katika mpira. Nilimjibu “Hapana tusahau”. Tusahau tu. Vipaji kama vyake vipo. Kuna watu watabisha. Lakini mpira kama wake haupo tena. Kuna sehemu tumekwenda na hatuwezi kukifikisha kipaji kuwa Ronaldinho kamili.
Hata ndani ya Brazil hauwezi kumpata Ronaldinho mwingine. Ni ngumu pia kumpata Neymar mwingine. Watoto wasiojua mpira na wale wenye kujua mpira wote wamechanganywa na wanafundishwa kucheza aina moja ya mpira. Mpira wa darasani na mpira wa namba. Mpira wa sayansi tofauti. Mpira wa matokeo sio mpira wa burudani.
Hakuna muda mwingi wa kujaribu vitu au kuburudisha watu. Hakuna. Tuna mpira wa kukaba kwa pamoja. Kuna mpira wa kushambulia kwa pamoja. Kuna mpira wa roboti ambao unaamuliwa na akili ya kocha na benchi lake la ufundi. Zamani watu wengi binafsi wangeweza kuamua mechi kwa uwezo binafsi. Siku hizi sio sana. Makocha wakali wanaamua mechi. Sio wachezaji binafsi.
Siku hizi mpira unaamuliwa namna ambavyo unaweza kuwa bora ukiwa na mpira na wakati hauna mpira. Ukiwa na mpira ghafla wachezaji wanne wanakuwa wameshafungua nafasi. Utaonekana chizi ukianza kupiga kanzu na chenga za madaha wakati watu wamechukua nafasi wanatengeneza shambulizi. Wachezaji wengi wana vifua vikubwa na wamefundishwa kuwa fiti kufika maeneo fulani ya uwanja bila ya kujali sana nafasi zao.
Leo ndio maana viungo wanafunga sana. Hata viungo wa chini wanafunga mabao ya kutosha. Washambuliaji tishio nao wameondoka kwa sababu mpira wa kisasa wakati mwingine unamuhukumu mshambuliaji kwa namna anavyowachezesha wenzake. Kama timu imeshinda mabao 3-0 na yeye hajafunga watu hawaoni kama ni kitu cha ajabu tofauti na zamani. Wanaangalia zaidi mchango wake katika mchezo kwa ujumla. Hii ndio dunia ya leo.
Ngumu kumpata Ronaldinho mwingine. Simama sehemu yoyote ambayo watoto wanafanya mazoezi siku hizi. Iwe wanasimamiwa au wanajisimamia wenyewe. Kitu cha msingi ni kupasiana zaidi mpira. Zamani wakati tunacheza kuna kitu lilikuwa kinaitwa ‘gombania goli’. Kunakuwa na goli moja na kipa mmoja. Wengine wote mnagombania kupigana chenga na kufunga. Hakukuwa na timu mbili uwanjani. Unajaribu tu kuwapita wenzako na kufunga.
Hayo ndio yalikuwa yanaongeza zaidi akili na maarifa. Unakuwa jeshi la mtu mmoja. Lakini sasa hivi unaonekana chizi wakati unapojaribu kupiga chenga wakati wenzako wawili au watatu wamefungua nafasi. Na ni kweli. Tunafundishwa kufungua sana nafasi wakati tukiwa na mpira. Tunafundishwa kuachia moja kwa haraka na kufungua nafasi. Sio kwamba akina Ronaldinho hawapo, hapana, wapo lakini wanafundishwa kufanya yale yale ambayo Declan Rice anafanya.
Mpira umekuwa wa timu zaidi. Zaidi mpira ulikuwa mchezo wa mchezaji mmoja mmoja zaidi. Watazame Wabrazil. Wanakwenda kombe la dunia wakiwa na mshambuliaji anayeitwa, Joao Pedro. Sio kwamba ni mchezaji mbaya, hapana, anafunga sana. Msimu huu tayari ana mabao 14 kwa Chelsea. Lakini Pedro sio Pele, sio Ronaldo de Lima, sio Zico. Sio Ronaldinho. Anategemea mfumo wa timu zaidi ili afunge. Anategemea pasi za wengi ili afunge. Anategemea pasi za wengine iki afunge. Ronaldo de Lima alikuwa anachukua watu wawili watatu anakwenda kufunga. Romario alikuwa hivyo hivyo. Lakini sasa hivi Pedro hata kama ana uwezo huo lakini analazimika kuachia kwa haraka ili akutane na mpira mbele yake. Asipofanya hivyo anaonekana kuwa mtu wa ajabu uwanjani. Akijaribu kufanya kitu chake binafsi halafu kikagoma anaonekana kuwa mwehu kwa sababu ameshapatiwa nafasi kadhaa za kupasia.
Ni ngumu kumpata Ronaldinho mwingine. Watu wanaweza kuhisi kwamba vipaji vimepungua. Sio sana. Vipaji vipo lakini vinabanwa na mifumo. Zamani mfumo ulikuwa mmoja tu. 4-4-2. Uwanja unakuwa mpana kwa kila mtu. Mawinga pia hawawajibiki ipasavyo katika kukaba. Dunia ya leo Ronaldinho, Zinedine Zidane, Jay Jay Okocha wangepaswa kukaba. Zamani walikuwa wanajiweka katika maeneo ya kupokea mpira tu. Siku hizi wangelazimika kukaba na kuachia mpira kwa haraka. Hatujui kama tunaweza kurudi katika mfumo wa mchezaji mmoja mmoja kutamba lakini siku hizi makocha ndio wanatamba zaidi. Watazame namna ambavyo Brighton and Hove wanavyocheza. Hawana mastaa wakubwa, lakini wanaweza kukutengenezea mfumo ambao utakuumiza kichwa. Zamani ilikuwa rahisi tu kwao kufumuliwa kwa uwezo binafsi wa wachezaji wakubwa wa timu kubwa. Siku hizi sio rahisi sana. Wanaweza kutengeneza fomesheni jeuri na wakakupa wakati mgumu. Nidhamu kubwa wa mpira imetuharibia vipaji maridhawa. Hata Wabrazil wa leo wanacheza kwa nidhamu kubwa ya mpira kuliko zamani. Ni ngumu kuona vipaji vyao. Zamani walikuwa wanacheza samba. Walikuwa wanatuletea mpira wao wa barabarani na ule wa katika fukwe kisha wanaucheza katika Kombe la Dunia. Walipotea walipoingizwa katika mfumo wa kucheza mpira wa Kizungu.
Leo, Brazil sio tishio tena. Zamani walikuwa na sayansi nzuri ya mpira lakini siku hizi wanacheza mpira wa Ulaya tu. Mpira wa kawaida. Watazame walinzi wawili wa Arsenal. William Saliba na Gabriel Magalhaes. Hapo kuna Mfaransa anacheza kama Mbrazil na kuna Mbrazil anacheza kama Mfaransa. Aina ya Saliba ndio ambavyo akina Lucio, Aldair, Roque Junior walikuwa wakicheza. Leo ndio ambavyo Saliba anacheza. Lakini mpira wa Gabriel ni wa Kiingereza zaidi. Mifano ya namna hiyo ipo mingi tu. Mtazame namna ambavyo Gabriel Martinelli anakimbia kama amekatwa kichwa. Halafu tazama namna ambavyo Eden Hazard alivyokuwa anacheza. Ni kama vile Martinelli ni Mbelgiji wakati Hazard anaonekana kuwa ni Mbrazil. Huu ni ukweli mchungu ndio maana Brazil sio tishio tena katika mpira. Mpira wa mifumo na takwimu za uwanjani umetuletea wachezaji wengi wa kawaida kuonekana wana maajabu uwanjani. Wale wenye vipaji vikubwa binafsi ambao wanashindwa kumudu mifumo tangu utotoni siku hizi wanatengwa. Hata klabu zinatumia data zaidi za mchezaji wakati wa kumsajili kuliko kuangalia kwa macho maajabu yake uwanjani.
Hata ukifanikisha kupiga chenga nyingi uwanjani watu wataangalia idadi ya pasi zako za mwisho na mabao. Katika eneo la kiungo mtu mwingine aliyeleta mabadiliko makubwa ya mpira ni Xavi Hernandez. Muda mwingi yeye ni pasi tu. Wachezaji wa Barcelona walikuwa wanamfanya kama ukuta. Wanagongesha mpira kwake kisha wanauchukua. Kuna makocha wengi wa kisasa ambao leo wangemchagua Xavi kuliko Zinedine Zidane.
Kwanini wangefanya hivyo? Kwa sababu Zidane alikuwa na umiliki mzuri wa mpira binafsi yeye kama yeye, lakini Xavi alikuwa anaisaidia zaidi timu kwa ujumla kuumiliki mpira. Hii ndio dunia ambayo Xavi alituleta. Hakuwa na takwimu za kanzu wala tobo. Huku kwetu mchezaji kama yeye ni Khalid Aucho wa Yanga.
Na katika eneo la mbele la kiungo mtu ambaye alitusaidia kubadilisha mawazo ya watoto na vijana ni Kevin De Bruyne. Hakuna na namba za tobo wala kanzu lakini alikuwa ana namba nzuri za kupiga pasi ndefu za mwisho kwa usahihi. Alikuwa bora katika maamuzi ya mpira mguuni mwake kuliko kupiga kanzu. Ukienda kutazama watoto wengi mtaani wanavyocheza huwa wanajifundisha mpira wa De Bruyne. Utamtoa wapi Ronaldinho katika mpira wa De Bruyne? Hauwezi
Ni ngumu kumpata Ronaldinho mwingine. Hata hawa kina Lionel Messi ndio wanamalizikia. Kyle Walker akiwa AC Milan alisikika akimwambia Joao Felix aachie mpira kwa haraka kwa sababu yeye sio Messi. Imeanza kuwa kauli maarufu dhidi ya watu wanaopenda kukaa na mpira kwa muda mrefu. Zamani kuanzia mtaani kwetu na duniani kwa ujumla kitu mtu alijiona anaweza kuwa Messi. Siku hizi hatukuruhusu uwe Messi wala Ronaldinho. Ndio ukweli mchungu.