Nigeria ilivyoteka soka la wanawake Afrika
Muktasari:
- Timu chache zilikuwa zikitamba, huku nyingine zikiingia kushiriki tu. Miongoni mwao, hakuna taifa lililotengeneza historia kubwa kama Nigeria.
KAMA kuna mashindano ambayo yamekuwa kioo cha ukuaji wa soka la wanawake barani Afrika, basi ni Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON). Leo hii kila taifa linapambana kufuzu, lakini miaka ya nyuma hali ilikuwa tofauti.
Timu chache zilikuwa zikitamba, huku nyingine zikiingia kushiriki tu. Miongoni mwao, hakuna taifa lililotengeneza historia kubwa kama Nigeria.
WAFCON ilianzishwa mwaka 1991 ikiwa na lengo la kumpata bingwa wa Afrika na mwakilishi wa bara hilo katika Kombe la Dunia la Wanawake.
Tangu wakati huo mashindano hayo yamekua kutoka timu nane hadi 12 na sasa 16, ishara kuwa soka la wanawake limeendelea kupiga hatua kwa kasi. Morocco imekuwa mwenyeji wa mashindano mara tatu mfululizo na michuano hiyo pia imekuwa ikitumika kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake 2027, Brazil.
Lakini nyuma ya ukuaji wa soka kuna utawala wa Nigeria. Super Falcons imejitengenezea heshima ambayo haijawahi kufikiwa na taifa lolote Afrika.
Katika matoleo 13 yaliyopita, Nigeria imetwaa mataji 10 zaidi ya mataifa yote mengine. Mara nyingi imekuwa ikipewa nafasi ya ubingwa hata kabla ya mashindano kuanza kutokana na ubora wa mfumo wake wa kuandaa vipaji, ligi yenye ushindani na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na Marekani.
Wengi wamekuwa wakijiuliza siri nyuma ya mafanikio ya Nigeria kwenye michuano hiyo ni ipi. Jibu ni kwamba mwendelezo tofauti na mataifa mengi ambayo huanza upya kila baada ya msimu wa mashindano, Nigeria imekuwa ikilea kizazi baada ya kizazi.
Kilipopita kizazi cha kina Mercy Akide, wakaja Perpetua Nkwocha na Rita Nwadike. Baadaye wakaibuka Asisat Oshoala, Onome Ebi, Chiamaka Nnadozie, Rasheedat Ajibade na kizazi cha sasa. Mfumo huo umeifanya ibaki kuwa imara kwa zaidi ya miaka 30.
Katika historia ya WAFCON, hakuna mshambuliaji mwenye rekodi kubwa kama Mnigeria Perpetua Nkwocha. Nyota huyo ndiye kinara wa mabao katika historia ya mashindano akiwa amefunga mabao 34 katika matoleo saba aliyoshiriki.
Mbali na rekodi hiyo, Nkwocha bado anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika WAFCON moja baada ya kutikisa nyavu mara 11 mwaka 2010.
Pia aliibuka mfungaji bora wa mashindano mara tatu mfululizo; mwaka 2004 (mabao 9), 2006 (mabao 7) na 2010 (mabao 11), huku akichaguliwa Mchezaji Bora wa Mashindano mwaka 2004.
Rekodi hizo zimemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la wanawake Afrika. Hata hivyo, kadiri miaka ilivyosonga mbele, mataifa mengine yalianza kuvunja utawala wa Nigeria. Equatorial Guinea iliyotwaa mataji mawili mwaka 2008 na 2012, kabla ya Afrika Kusini kuandika historia mwaka 2022 kwa kuinyang’anya Nigeria ubingwa na kutwaa taji lake la kwanza.
Ushindi huo haukuwa wa bahati mbaya. Ilikuwa matokeo ya uwekezaji mkubwa katika ligi ya wanawake, programu za vijana na kuendelea kumuamini kocha Desiree Ellis, ambaye ameibadilisha Banyana Banyana kuwa moja ya timu bora Afrika.
Wakati Afrika Kusini ikiandika rekodi hiyo, Morocco nayo iliamua kuwekeza nguvu kubwa. Serikali, Shirikisho la Soka la Morocco na klabu ziliwekeza kwenye miundombinu, akademi na ligi ya wanawake.
Baada ya uwekezaji huo mwaka 2022 Morocco ikafika fainali na kurudia tena mwaka 2024, ingawa ilipoteza zote mbili dhidi ya Afrika Kusini na Nigeria. Hata hivyo wengi wanaamini ni suala la muda kabla ya Atlas Lionesses kutwaa taji lao la kwanza.
Miongoni mwa timu zinazotarajiwa kufanya vizuri mwaka huu ni Zambia. Ikiwa na nyota kama Barbra Banda na Racheal Kundananji, Zambia imebadilika na kuonekana moja ya timu hatari zinazoweza kufanya maajabu mwaka huu.
Kasi yao ya kushambulia imeifanya timu hiyo kuwa tishio kwa vigogo, ingawa bado imekuwa ikikosa uimara wa kujilinda inapokutana na timu zenye uzoefu mkubwa kama Nigeria.
WAFCON ya mwaka huu pia imekuja na mabadiliko makubwa nje ya uwanja. CAF imeongeza zawadi ya bingwa kutoka dola milioni moja hadi milioni mbili za Marekani, huku jumla ya fedha za zawadi zikiongezeka hadi dola milioni 5.8.
Kila timu itakayoshiriki pia itapata fedha zaidi kuliko ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita, hatua inayolenga kuongeza ushindani na kuhamasisha mataifa kuwekeza zaidi katika soka la wanawake.
Twiga Stars inaingia WAFCON kwa mara ya tatu ikitafuta kuvunja mwiko wa kutofika robo fainali. Njia ya kufanya hivyo ipo kama ikiamua kujituma na kuwaheshimu wapinzani wao.