Tuendelee kubeti kwa Yanga, Waarabu ni Simba wa karatasi
Muktasari:
- Simba walipita kwa mbinde kwa matuta. Marehemu Christopher Alex alifunga penalti ya mwisho na Simba ikaitoa Zamalek ambaye alikuwa bingwa mtetezi.
KUNA siku mbili katika miaka tofauti huwa nazikumbuka. Kwanza ni usiku ule wa siku fulani mwaka 2003 pambano kati ya Simba na Zamalek pale Cairo Misri.
Simba walipita kwa mbinde kwa matuta. Marehemu Christopher Alex alifunga penalti ya mwisho na Simba ikaitoa Zamalek ambaye alikuwa bingwa mtetezi.
Kwa dakika 80 mpira ulikuwa unachezwa katika kumi na nane ya Simba. Akina Boniface Pawassa na Victor Costa walitaabika haswa.
Muda wote Israili alikuwa akitafuta roho ya Simba. Sijui ilikuaje siku ile Simba walisalimika.
Pengo baina ya timu zao lilikuwa kubwa. Mwishowe Waarabu hawakuamini kwa sababu ilikuwa kama miujiuza kutolewa na Simba katika uwanja wa nyumbani.
Halafu kuna mechi moja ilichezwa uwanja wa Taifa kati ya Yanga na Al Ahly. Huwa ninacheka ninapokumbuka kitu kuhusu hii mechi. Staa wa Angola, Flavio aliipatia Al Ahly bao la kuongoza dakika ya sita ya mchezo.
Wakati huo Al Ahly ilikuwa imejaza mastaa wengi kama akina Mohamed Aboutrika na Mohamed Barakat.
Al Ahly walikuwa wanapiga pasi nyingi uwanjani kiasi cha kuwaudhi wachezaji wa Yanga akina Athuman Idd Chuji. Akina Chuji wakaanza kucheza rafu za makusudi.
Alinisimulia Chuji mwenyewe kuna wakati wachezaji wa Al Ahly walikuwa wanawaambia wachezaji wa Yanga wasicheze rafu kwa sababu wanaweza kuwatia hasira wakafunga mabao mengine.
Kwamba hawakutaka kuwafunga mabao zaidi na kuwadhalilisha uwanja wa nyumbani.
Nimezikumbuka hizi mechi mbili baada ya kutazama mechi zetu na Waarabu siku hizi.
Tumeondoka katika mateso yale na sasa popote tunapocheza na Waarabu huwa tunatulia na kucheza kwa namna tunavyojisikia tofauti na zamani na wao walikuwa wanacheza kwa kadri wanavyojisikia.
Nadhani ujio wa akina Clatous Chotta Chama, Pacome Zouzoua, Djigui Diarra, Aziz Ki, Serge Wawa na wengineo katika mpira wetu umepunguza pengo kubwa ambalo lilikuwepo baina ya sisi na wao.
Sasa hivi tunaweza kupishana nao vizuri tu. Mwanzoni tulikuwa hatuleti wachezaji wa kigeni wenye ubora lakini sasa hivi tuna wachezaji ambao wanaweza hata kuitwa katika timu za taifa za mataifa ya Afrika Magharibi.
Ijumaa usiku Yanga walikuwa na mechi nyingine dhidi ya Waarabu.
Yanga wamepangwa na Waarabu watupu na kundi lao lilitajwa kuwa kundi la kifo lakini hivi tunavyozungumza Yanga wana pointi nne katika kundi lao.
Wana tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya wababe wa kundi Al Ahly.
Kabla mechi za kundi lao hazijachezwa ilikuwa inaonekana kama vile Yanga wasingeambulia chochote.
Binafsi niliamini Yanga wangefanya vizuri katika kundi lao kwa sababu bado hatujajibu swali fulani kwa umakini. Timu za Afrika Kaskazini zimeshuka au timu za Tanzania zimeongeza ubora?
Nikiwatazama Simba na Yanga wanavyocheza leo dhidi ya timu za Afrika Kaskazini nilishangaa kuona Yanga hapewi nafasi katika kundi lao.
Katika pambano Ijumaa jioni kuna mambo mawili. Kwanza kabisa Djigui Diarra alidhihirisha ubora wa wachezaji wa kigeni ambao wamekuwa wakiletwa nchini kwa sasa.
Hakuna kipa wa Tanzania anayefikia ubora wa Diarra kwa sasa. Ina maana kama Ijumaa jioni lango la Yanga lingekuwa na kipa Mtanzania basi si ajabu Yanga isingekuwa na pointi nne mpaka sasa.
Huu ni ukweli mchungu. Zamani tulikuwa na makipa wengi wazuri. Hata pambano lile la Simba na Zamalek pale Cairo langoni alikuwepo Juma Kaseja.
Lakini leo hatuna akina Kaseja tena ndio maana malango ya timu zetu kubwa yana makipa kutoka nje. Hauwezi kumlaumu Injinia Hersi Said kwenda Mali kumchukua Diarra.
Diarra anajua kuokoa michomo, anajua kujipanga langoni, anajua kutumia miguu yake vema. Katika mechi hii alijua pia kuchelewesha muda wakati JS Kayblie walipokuwa wanasaka pointi tatu katika kipindi cha pili. Anahitajika kipa mwenye uzoefu kufanya alichokuwa anafanya.
Kwa upande mwingine Celestin Ecua ndiye ambaye aliwanyima Yanga pointi tatu. Alipata nafasi nzuri ya dhahabu ambayo alipaswa kuitumia. Wiki moja kabla Prince Dube alifunga bao gumu kuliko nafasi ambayo Ecua amepoteza.
Uzuri wa viongozi wetu wa mpira siku hizi, pamoja na mashabiki wao huwa hawadanganyiki na ukubwa wa taifa ambalo mchezaji ametoka. Ecua ajiangalie.
Anaweza kujikuta hatakiwi msimu mmoja tu baada ya kuja kwa mbwembwe Tanzania.
Aziz Ki alikuja kwa mbwembwe katika usajili wake lakini msimu wake wa kwanza akawa kama Ecua wa leo. Nusura Yanga wamtoe kwa mkopo kwenda Singida. Msimu wa pili ndio akarekebisha tabia na kuimbwa na mashabiki.
Ecua anaweza kukutana na hali hiyo kama akiendelea kuonyesha kiwango anachoonyesha. Mpaka sasa Edmund John ni bora kuliko yeye.
Na sasa Yanga ina mechi mbili dhidi ya Al Ahly. Nyumbani na ugenini. Sioni Yanga akipoteza mechi hizi. Nawafuatilia Al Ahly wa sasa hivi sioni kama wana jipya sana.
Wana bahati watakutana na Yanga ambayo na yenyewe ni kama inajitafuta baada ya kuvurugwa na Roman Folz katika siku za karibu. Kama Yanga ingekuwa ile ya Manuel Gamondi nadhani Al Ahly angeweza kufa katika moja ya mechi hizi mbili.
Majuzi hapa tuliwalalamikia Simba walikuwa wabovu lakini walipocheza na Al Ahly katika mechi mbili za Super League walitoka sare Dar es salaam na Cairo wakaishia kufungwa kwa penalti. Siwaoni Al Ahly wakiwa wale ambao tuliwafahamu na kuwaogopa.
Sio wao watu, kule Kaskazini sasa hivi kuna shida ndio maana timu kama Stade Mallen wanakwenda kucheza na Esparance Du Tunis na wanatoka sare ugenini.
Timu za Afrika Magharibi hazina uwezekaji mkubwa lakini sasa hivi zinafanikiwa kutoka sare ugenini dhidi ya timu za Afrika Kaskazini. Vipi kwa Yanga ambayo imefanya uwekezaji?
Ndiyo maana sijashangaa kuona Yanga ana pointi nne katika kundi la Waarabu. Yanga ametia pesa na kina Pacome sasa hivi ndio maana naweza kuwabetia watapita katika hili kundi.
Hata mechi zao mbili dhidi ya Al Ahly wakijipanga vizuri wanaweza kuokota pointi nne nyingine kama ambazo wameokota kwa Far Rabat na JS Kayblie.
Nipo upande wao na nawabetia kwamba watapita katika kundi lao. Ndugu zenu wamekuwa Simba wa karatasi na wala hawana maajabu makubwa.
Majina yao ni makubwa lakini hali halisi ni kwamba ni bora umuogope Pyramids na Fiston Mayele wao kuliko kuwaogopa akina Al Ahly. Kila siku wamekuwa wakichana mikeka.