Dube alivyoigeukia bahati Pedro akageuza kiwango
Muktasari:
- Picha nzuri na ya kusisimua ilionekana jana akiwa anashangilia kwa furaha baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco.
PICHA ya huzuni ilitokea wiki chache zilizopita, ikimuonyesha Prince Dube akiwa peke yake katika benchi akijiinamia akilia kwa uchungu. Alikosa mabao ya wazi dhidi ya Silver Strikers huku miguu yake ikionekana kuwa mizito kama vile ilikuwa imefungwa na mawe.
Picha nzuri na ya kusisimua ilionekana jana akiwa anashangilia kwa furaha baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco.
Ilikuwa picha ya kusisimua. Kando yake alikuwapo Profesa wa Mpira, Pacome Zouzoua. Maisha yameenda kasi kwa Prince Dube ndani ya wiki hizi mbili. Na maisha yameenda kasi pia kwa Yanga yenyewe.
Hili la Dube shukrani kubwa inakwenda kwa mashabiki wa Yanga yenyewe. Mabosi wake. Benchi lake la ufundi. Unaanzia kwa mashabiki namna ambavyo wamebadilika katika miaka ya hivi karibuni.
Mashabiki wa zamani wana tofauti kubwa na mashabiki wa siku hizi. Mashabiki wa zamani 'wangekuua' pindi mambo yanapokwenda kombo. Mashabiki wa siku hizi wanakushika mkono pindi unapoanguka.
Yanga walijitokeza katika pambano lililofuata baada ya pambano dhidi ya Silver Strikers. Walikwenda pale Mwenge kutazama pambano dhidi ya Mtibwa Sugar na wakamshika mkono Dube kwa kuimba jina lake na kumchangia kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kumtia moyo. Jana hakuwaangusha. Alionyesha kile ambacho Yanga walikipigania katika kulipa kisasi cha kumtoa Azam ikiwa ni kama deni la kuibiwa Fei Toto.
Pasi ya Mudathir Yahya ilikuwa nzuri, lakini bado ilipaswa kufanyiwa kazi na kasi ya Dube pamoja na umaliziaji mzuri wa kuuweka mpira katika nyavu za Far Rabat. Lilikuwa bao zuri ambalo lilitukumbusha ubora wa Mtoto wa Mfalme. Alisajiliwa na Yanga kwa ajili mechi kama hizi. Hakusajiliwa na Yanga kwa ajili ya kuwa na miguu mizito.
Vinginevyo kiwango cha Dube kilienda sambamba na kiwango cha timu yake. Yanga ya jana waliumiliki mpira vema dhidi ya timu ambayo ilishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Morocco msimu uliopita.
Sio kitu rahisi sana ukilinganisha ugumu wa Ligi Kuu ya Morocco kulinganisha na ligi yetu. Yanga walionekana kurudi kuwa kama Yanga na kuachana na kivuli cha Roman Folz.
Pedro Goncalves na wenzake katika benchi la ufundi walionekana kuirudisha Yanga katika tempo, kasi, stamina na nguvu. Vitu hivi vilipotea chini ya Folz na Yanga wakaanza kuwa timu ya kawaida.
Jana walionekana kuwa katika ubora wao na kufanya mambo mengi sahihi. Kuanzia ukabaji, umiliki wa mpira, lakini usafirishaji wa mpira kutoka nyuma kwenda katikati kisha mbele.
Katika kusimamia yote haya, kama kawaida 'sterling' wa Yanga alikuwa Pacome. Anajua mpira. Anacheza kwa maringo wakati huo huo akifanya mambo mengi sahihi. Yeye ndiye ufunguo wa mashambulizi ya Yanga, huku pia akiwa kiini cha umiliki wa mpira wa Yanga. Amekuwa akifanya hivi katika mechi zote muhimu za Yanga.
Halafu kuna kipa Djigui Diarra. Ni mchezaji bora wa Yanga asiyeimbwa kama anavyoimbwa Pacome. Hata hivyo, umuhimu wao ni sawa tu. Diarra anajua kutulia langoni.
Hana makosa ya msingi kama ilivyo kwa makipa wengi nchini na kwingineko. 'Timing' yake katika mipira ya juu ni nzuri na kujipanga kwake langoni kunafanya mashambulizi ya timu pinzani yasionekane kuwa na hatari.
Halafu kuna Mohamed Hussein 'Tshabalala'. Nadhani anaweza kuwa chaguo la kwanza upande wa kushoto chini ya kocha Pedro.
Wakati wa Folz, beki Tshabalala alikuwa anasugua benchi, lakini inaonekana Pedro anamwamini zaidi yeye kuliko Chadrack Boka. Tuendelea kuona hadi mwisho wa safari yao itakuwaje, lakini mpaka sasa hali ya hewa imekuwa nzuri kwake.
Wakati mwingine mabadiliko ya benchi la ufundi huwa yanabadili bahati za wachezaji. Ni kama ambavyo Folz alimuamini Aziz Andabwile kiasi cha kuimbwa sana na mashabiki na akaitwa katika kikosi cha timu ya taifa, lakini ghafla nyota yake imepotea katika utawala wa Pedro. Huwa inatokea hata kule kwa wenzetu.
Kuna mchezaji anaitwa Celestin Ecua. Ana kipaji kizuri na kasi nzuri uwanjani, lakini apunguze mapepe. Kichwa chake hakijatulia katika suala la kufanya uamuzi. Wachezaji bora ni wale wenye kutoa uamuzi mzuri uwanjani.
Hiyo ndio inakuwa tofauti kubwa kati ya mchezaji mkubwa na mchezaji wa kawaida. Na kimsingi kuna tofauti kati ya kipaji na uamuzi. Kuna wachezaji wengi wana vipaji vya kuuchezea mpira lakini hawana uamuzi sahihi.
Wakati Yanga wakiendelea kushangilia ushindi ni muhimu pia wakumbuke kumuombea Clement Mzize apone mapema. Ni mshambuliaji anayeipa Yanga ladha tofauti katika safu yao ya ushambuliaji. Anahitajika katika mechi kama hizi na pengo lake lipo pale mbele, licha ya Dube kuwapa bao la furaha katika kipindi cha pili.
Na baada ya hapo ni muhimu pia kuwapongeza Yanga, ingawa pia walikuwa na bahati kuondoka na pointi zote tatu. Kama kungekuwa na VAR si ajabu Wamorocco wangekuwa wamesawazisha katika mpira ambao ingawa filimbi ilipigwa kabla, lakini tayari nyavu za Yanga zilishatikisika.
Na sasa wanashika nafasi ya pili katika kundi ambalo Watanzania walilipachika jina la kundi la kifo. Al Ahly alimchapa JS Kayblie mabao 4-1 na moja kwa moja ametwaa uongozi wa kundi. Kitu muhimu kwa Yanga kilikuwa kupata pointi tatu muhimu za nyumbani ambazo wamezipata. Katika michuano hii pointi tisa za nyumbani zinaweza kukupeleka robo fainali.
Kinachotakiwa kwa sasa ni kwamba wiki ijayo Yanga watakuwa ugenini Algeria kucheza na JS Kayblie na pointi moja tu, inaweza kuwatosha. Kama ndani ya mechi mbili watakuwa wamepata pointi nne nadhani watakuwa wametanguliza mguu mmoja kwenda robo fainali. Wafanye matumizi mazuri ya uwanja wa nyumbani kama ambavyo watani wao Simba wamekuwa wakifanya kiasi cha kutuletea kauli ya 'Kwa Mkapa hatoki mtu'.
Wakati wa maandalizi ya pambano hili nilikuwa na shaka na timu kubwa za Tanzania, Simba na Yanga. Viwango vyao havikunisisimua sana na sikuweka matumaini makubwa kwao.
Hata hivyo, kiwango cha Yanga cha jana kimenibadili mawazo. Nimegundua wana nafasi nzuri tu ya kwenda robo fainali kama wakiendelea kucheza hivi. Timu za Afrika Kaskazini kwa sasa hazina maajabu sana. Ni suala tu la kujipanga kwa sababu hata sisi wenyewe tumeongeza ubora katika maeneo mengi.
Al Ahly watakuwa ugenini kucheza na Far Rabat na Yanga wanapaswa kuwaombea Al Ahly washinde. Wakubali tu kwamba kuwe na mbabe mmoja katika kundi na sio lazima wawe wao. Timu tishio kati ya Far Rabat na JS Kayblie ni Far Rabat. Yanga awe na kampeni ya kumuombea mabaya Mmoroco ambaye katika kundi amepewa nafasi ya pili chini ya Al Ahly.