SPOTI XTRA: Maumivu ya elimu ya soka Tanzania
Muktasari:
- Na ni juma lililopita tu walishindwa kuichezea Taifa Stars huko Namibia eti tatizo, usafiri! Inaingia akilini hii?
KWENYE dunia hii ya sasa ya soka la Tanzania, leo hii jifanye mdau wa soka ama mwandishi wa habari za soka, na baada ya hapo chukua nafasi yako na uende kumuuliza mwanandinga wa Tanzania swali hili:
“Nini matarajio yako ya baadaye ya soka unalocheza?” Jibu lake litakuwa rahisi sana, nalo ni hili: “Natarajia kucheza soka la kulipwa!
Lakini pasipo kutambua masikini ya Mungu njia sahihi itakayomfanya afike huko kwenye soka hilo la kulipwa, analazimika kupitia njia zipi, kwani mwenyewe anaamini kuwa kula chipsi mayai mtaani, kunyoa kiduku, kuweka kipuri masikioni, kupaka dawa kwenye nywele, kuinua kola ya jezi, kukata vilinda ugoko vibakie vidogo sana mguuni, na mwisho kuzima, kupiga pasi, visigino na mbwembwe ndivyo vitakavyoweza kumfikisha safari yake ya mafanikio.
Achilia mbali kutoa visingizio baada ya matokeo mabaya, eti hakulipwa pesa ya milangoni ya mechi ile ya mwezi uliopita, muulize mkataba wake unasemaje kama kuna kipengele hicho, au hanung’uniki juu ya kiasi cha pesa anacholipwa mwenzake utafikiri walisaini pamoja mkataba, Au kisingizio cha kocha mbaya au tuliahidiwa pesa hatukulipwa na mengineyo ya ajabu tu.
Ajabu hajui kwamba kucheza soka la kulipwa si kujua kuzuia na kupiga pasi tu, kuna mengi anayopaswa kuyafanya ili kufika anakotaka katika maisha yake ya soka, kwani anashindwa kutambua kwamba leo hii kuna vingine vinatazamwa zaidi na zaidi ya yote jinsi mwanandinga anavyoweza kwenda na muda ndani ya uwanja, akiwa na mpira ama akiwa hana mpira.
Leo hii nina kituko kingine hapa, nacho ni kutotambua kwamba anapokwenda kufanyiwa majaribio, ataulizwa kwamba amecheza mechi ngapi za timu yake ya taifa, ambacho ni moja kati ya vigezo vikubwa kabisa, nani anakuchukua katika timu au ligi bora yenye malisho mazuri kama huna mechi za timu ya taifa mkononi?
Amini maneno yangu, mchezaji wa Kitanzania hataki kabisa kuisikia timu yake ya taifa ya nchi, na ndiyo maana usishangae ukasikia hata hao wachache wanaocheza barani Afrika kwenye nchi mbalimbali, wanakosa nafasi ya kuichezea timu yao ya taifa, ukiuliza sababu utaambiwa kwamba suala la usafiri limekuwa gumu.
Jiulize swali, wachezaji kama Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto wamekosa kuichezea timu ya taifa mara ngapi, wakati wenzao wote wanakwenda kuzitumikia nchi zao kwenye mechi hizi zinazochezwa kwa mujibu wa kalenda ya mamlaka kuu za kabumbu la dunia yaani Fifa lakini bado kunakuwa na tatizo kwa mchezaji.
Juma lililopita tu walishindwa kuichezea Taifa Stars huko Namibia eti tatizo, usafiri! Inaingia akilini hii?
Fikiria kama wanandinga wa kimataifa wa Zambia wanaokipiga TP Mazembe wanakwenda kucheza timu yao ya taifa kwenye kalenda ya Fifa, vipi wao? Vipi Wakongo wenyewe si wanakwenda kuichezea nchi yao, mbona hakuna tatizo, waulizeni vizuri hao wanandinga wetu, kwa nini ni wao ndiyo wasije?
Juma lililopita, akina Emmanuel Okwi na Kiiza wa Yanga walikwenda Ndola kuichezea Uganda Cranes, na baada ya hapo wakaelekea Cairo, Misri, kwa nini wao wanaweza, au wanafahamu uzalendo zaidi? Leo Yanga ingemsaini Kiiza kama isingemuona kwenye timu ya taifa?
Hapa ndipo unapoona elimu ya kabumbu ilivyo ndogo, ambayo inaanzia mbali sana, na mwishoni tunaanza kuainisha matatizo yanayosababisha ionekane haipo elimu hii kwa wanaotaka kucheza soka.