Maboresho ya kanuni na kanuni mpya toleo la 2026
Muktasari:
- Katika uchambuzi huu wa kina, Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya vifungu ikilinganisha kanuni za zamani na hizi mpya ambazo zimeanza kutumika sasa.
MASHABIKI wa soka nchini na klabu za Ligi Kuu Bara, zinapaswa kukaa mkao wa kula! Hii ni baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuja kivingine kupitia Maboresho ya Kanuni za Toleo la 2026, ikileta mapinduzi makubwa kuanzia kwenye matumizi ya teknolojia uwanjani hadi adhabu kali za fedha ambazo ni wazi zipo kwa ajili ya kuwanyoosha wale wakaidi.
Maboresho haya, yaliyoundwa chini ya Ibara ya 78(3) ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya mwaka 2026, yanatajwa kuwa mwiba mchungu kwa wakaidi. Katika uchambuzi huu wa kina, Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya vifungu ikilinganisha kanuni za zamani na hizi mpya ambazo zimeanza kutumika sasa.
1. MAMLAKA (Kanuni ya 9)
Kanuni ya 9.6 (Mamlaka ya Uwanja): TFF/TPLB sasa ina mamlaka ya mwisho ya kuhamishia mchezo wowote katika uwanja tofauti na ule uliochaguliwa na timu mwenyeji, endapo wataona inafaa. Kanuni ya 9.7 (Uteuzi wa Viwanja): Timu inaweza kuteua viwanja viwili vya nyumbani ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ikijumuisha Visiwani), mradi viwe vimekaguliwa.
2. GHARAMA ZA USHIRIKI NA RUFAA (Kanuni ya 13, 27 na 74)
Ada ya Ushiriki (Kanuni 13.2): Imep anda kutoka Sh500 ,000 hadi Sh1 milioni.
Ada ya Mar ejeo/Rufaa (Kanuni 27.4 & 74.15): Imeongezeka kutoka Sh1 milioni hadi Sh2 milioni kwa ajili ya kuomba marejeo ya uamuzi.
Migogoro ya Kimkataba (Kanuni 74.15): Sasa kuna ada ya Sh50,000 ya kufungulia maombi ya utatuzi wa mgogoro mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.
3. UDHAMINI NA BIMA (Kanuni ya 16 na 21)
Ukiukwaji wa Udhamini (Kanuni 16.1): Faini imeongezeka takribani mara tatu, kutoka Sh3 milioni hadi Sh10 milioni kumi kwa kila mchezo utakaokiuka masharti.
Mawasiliano na Wadhamini (Kanuni 16.1.11): Marufuku ya kuwasiliana na mdhamini bila idhini sasa inawahusisha pia viongozi wa klabu. Adhabu imepanda kutoka Sh500,000 hadi faini isiyopungua Sh10 milioni. Muda wa Bima (Kanuni 21): Sasa ni lazima bima ya matibabu na ajali isipungue kipindi cha mwaka mmoja, na klabu lazima ziwasilishe Hati ya Bima (Cover Note) kwa uhakiki.
4. TARATIBU ZA MCHEZO NA MAENDELEO YA VIJANA (Kanuni ya 17)
Idadi ya Viongozi (Kanuni 17.6): Orodha ya viongozi inayowasilishwa kwa GC sasa lazima iwe na wasiopungua viongozi saba (7) badala ya watano.
Wachezaji Vijana (Kanuni 17.6.2): Hili ni mabadiliko makubwa; mbali na kuwa na vijana wawili kwenye orodha ya 21, angalau mchezaji mmoja lazima acheze kwa angalau 10% ya muda wa mchezo. Mazoezi ya Timu Ngeni (Kanuni 17.45): Kanuni iliyokuwa inaruhusu timu ngeni kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi mara moja imeondolewa.
5. ADHABU NA NIDHAMU (Kanuni ya 17, 32, 41, na 47)
Vurugu na Matangazo (Kanuni 32.9): Timu inayozuia matangazo ya TV/Redio itapigwa faini ya Sh5 milioni na inaweza kushushwa daraja.
Ukiukwaji wa Taratibu (Kanuni 17.62): Faini ya jumla imepanda hadi Sh10 milioni. Kwa makosa yanayojirudia, faini inaweza kufikia hadi Sh40 milioni. Vyumba vya Kuvalia (Kanuni 47.35 & 47.36 - MPYA): Timu inayovaa ndani ya gari, chini ya mti, au jukwaani itapigwa faini ya Sh50 milioni na kukatwa pointi tano (5). Kuingia chumba cha timu pinzani bila idhini ni faini ya Sh50 milioni. Kususia Sherehe (Kanuni 47.34 - MPYA): Klabu inayokaidi kushiriki sherehe za kukabidhi kikombe au medali itatozwa faini isiyopungua Sh50 milioni. Kuruka Ukuta (Kanuni 47.37 - MPYA): Timu inayopita milango isiyo rasmi au kuruka ukuta itapigwa faini ya Sh50 milioni na ikirudia inakatwa pointi mbili na faini ya Sh100 milioni.
6. KANUNI MPYA: Video Support System (VS) (Kanuni ya 20)
Hii ni teknolojia mpya iliyoanzishwa kwa ajili ya: Kusaidia kuamua bao, penalti, kadi nyekundu ya moja kwa moja, na kumtambua mchezaji aliyekosea. Kocha Mkuu pekee ndiye mwenye haki ya kuomba marejeo ya VS ndani ya dakika moja kupitia mwamuzi wa akiba. Ni marufuku kwa mchezaji kumkabili mwamuzi kushinikiza matumizi ya VS.
7. MAOFISA HABARI (Kanuni ya 48/49 - MPYA)
Sasa kuna udhibiti mkali kwa maofisa habari: Marufuku kutoa kauli za uchochezi, uzushi, kashfa za ukabila, ukanda, udini, au jinsia. Ofisa habari atawajibika binafsi kwa taarifa hasi anazotoa. Adhabu ni faini ya Sh10 milioni au kufungiwa miezi sita.
8. USAJILI NA WACHEZAJI WA KIGENI (Kanuni ya 64, 65, na 69)
Vigezo vya Kigeni (Kanuni 64): Wachezaji kutoka Amerika Kusini, Ulaya na sasa Asia, lazima wawe wanatoka walau Ligi Daraja la Pili. Wajibu wa Kutangaza Usajili (Kanuni 65.5): Jukumu hili limehamishwa kutoka kwa Kocha Mkuu na sasa ni wajibu wa klabu. Dirisha Dogo (Kanuni 65.11): Klabu inaruhusiwa kusajili na kuondoa wachezaji wasiozidi saba (7) pekee.
Nyaraka za Usajili (Kanuni 69): Kwa wachezaji wa vijana, sasa ni lazima kuambatanisha Pasi ya Kusafiria (Passport), Kitambulisho cha Taifa, au cheti cha kuzaliwa.
9. MAADILI: BETTING NA DAWA HARAMU (Kanuni ya 40 na 49)
Kubashiri (Betting - Kanuni 40.6): Udhibiti umeongezeka, ikijumuisha marufuku ya kutoa mbinu za timu kwa upande wa tatu. Adhabu ni kufungiwa maisha (life ban) au faini ya Sh30 milioni.
Dawa Haramu (Kanuni 49.1): Sasa inafuata kanuni za WADA moja kwa moja. Kiongozi anayeficha ushahidi wa matumizi ya dawa atapigwa faini ya milioni mbili na kufungiwa mwaka mmoja.