Prime
Sowah ule utamu wake ulivyopotelea baharini
KATI ya vyakula vitamu vya baharini, ni samaki. Samaki ana ladha ya aina yake, ingawa hutofautiana.
Ukiacha wale samaki wa bei mbaya ambao hutumiwa kwenye sherehe za kifahari za matajiri, kwa sisi wa maisha ya kawaida samaki wengi watamu ni wale wenye miba mingi na si wale wenye nyama nyingi kama jodari au kwa Kiingereza King Fish.
Wawe wa mtoni, ziwani au baharini, wenye minofu mitamu ni wale wenye miba mingi.
Na kwa sababu hiyo, hata ulaji wake huhitaji umakini mkubwa la sivyo miba itachoma kinywa au mmoja ukaenda kukwama mlango wa koo na kulazimika kujikoholesha kila wakati au kula matonge makubwa ya ugali ili kuusukumu uingie ndani na kukuondolea kero.
Kula samaki mwenye miba mingi ni kama kutafuna mabomu ambayo umeambiwa yana nyama nzuri. Kazi itakuwa upate hiyo nyama nzuri, lakini usilipue bomu; kitu ambacho hakiwezekani.
Ndivyo unavyoweza kumuelezea mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah, ambaye ametokea Ghana.
Ni mshambuliaji ambaye Kiswahili tunamuelezea kama mtu anayelijua goli, ana nguvu, ana kimo kizuri na ni mpambanaji kwelikweli asiyehitaji kukumbushwa wajibu wake wa kusaidia timu kutafuta mpira, kupasia wenzake au kupigana vikumbo na wachezaji wa timu pinzani ilia pate nafasi ya kufunga.
Ari yake ya upambanaji hasa wakati wa kutafuta kupokonya mpira husababisha atumie nguvu za ziada na hivyo kujikuta akitumia mchezo mbaya ambao husababisha ama aonywe au apate kadi kara kadhaa.
Huu ndio umekuwa utamaduni wake tangu akiwa Medeama FC na baadaye Al Nasr ya Libya kabla ya kiujiunga na Singida Black Stars wakati wa dirisha dogo la msimu uliopita.
Mchezo wake wa matumizi ya nguvu na kutokuwa mwangalifu wakati wa kusaka umiliki wa mpira umesababisha hivi sasa awe mapumzikoni kwa mechi za ligi za ndani baada ya Kamati ya Saa 72 kumfungia mechi tano.
Hiyo ni adhabu yake ya kwanza akiwa na klabu yake mpya ya Simba SC. Lakini alitokea Singida Black Stars akiwa na kiporo cha kuzuiwa kucheza mechi baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB, hivyo kuikosa mechi ambayo ingekuwa ya kwanza kwake dhidi ya watani wa jadi, Yanga.
Akiwa Medeama nusura azawadiwe kadi ya rangi hiyo ya Msimbazi baada ya kumrukia kwa makusudi beki wa Yanga, Dickson Job aliyekuwa amelala chini ya kuuwahi mpira uliokuwa ukikimbiliwa na Mghana huyo.
Alirudia tukio kama hilo la kurukia kifuani wakati akiwa Singida Black Stars. Ilipigwa pasi ndefu na kama kawaida yake akachomoka kuifuata, lakini alikuwa tayari kipa Djigui Diarra ameuwahi. Badala ya kumuepuka, akamfuata akiwa amenyanyua guu lake la kulia lililoishia kumparaza kifuani kipa huyo wa Mali.
Kutokana na sifa zake nzuri kiuchezaji, ungetegemea Simba wamtegemee sana Sowah katika kupata ushindi wa mechi m muhimu ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Esperance de Tunis iliyochezwa Jumamosi nchini Tunisia.
Alianza kwa nguvu na nusura aipatie Simba bao katika dakika za mwanzoni wakati alipochomoka kuufuata mpira wa kichwa uliopigwa na benki wa Esperance kwenda kwa kipa wake. Hata hivyo, licha ya kuuwahi na kuudokoa, hakuweza kufunga bao kwa kuwa kipa alishajitenga vizuri kuuzuia.
Aliendelea kuwasumbua mabeki wa Esperance kila walipokuwa na mpira, kiasi kwamba walilazimika nyakati fulani kuitupa mipira mbele kuepuka wasije kuupotezea miguuni mwa mshambuliaji huyo mwenye miaka 27.
Lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo alivyoonekana kuanza kupoteza uvumilivu. Akaanza kulazimika kutumia nguvu zake za ziada na ilikuwa bahati kwamba hakuzawadiwa kadi ambayo ingesababisha acheze kwa wasiwasi kwa muda mwingi.
Sijui kama aliumia au kocha Steve Barker alikuwa na sababu nyingine za kumbadilisha mwanzoni mwa kipindi cha pili. Lakini sababu kubwa in aweza kuwa ni ile ya kuanza kupoteza umakini katika kutafuta mpira. Hatari ikawa kwamba akionyeshwa kadi ya njano, hatacheza vizuri tena na kama angeendelea, uwezekano mkubwa ulikuwa kadi ye pili ya njano.
Kwa sifa zake za kiuchezaji, kujituma na kimo chake, ungetegemea aendelee kuwasumbua mabeki wa Esperance na hivyo kumwekea ulinzi wa ziada ambao ungepunguza uwezo wake wa kwenda mbele. Lakini Seleman Mwalimu aliitwa kuchukua nafasi yake na huo ukawa mwisho wa hadithi ya Sowah katika mechi hiyo iliyokuwa muhimu kwa Simba kupata angalau pointi moja katika mechi tatu za hatua ya makundi ilizocheza hadi sasa.
Ni mchezaji mzuri mithili ya samaki mtamu, lakini matumizi yake yanahitaji uangalifu mkubwa kuepuka athari za kujiumiza. Pengine umakini wa kwanza ni kuzungumza naye sana kuhusu tabia hiyo ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuvamia wengine kwa makusudi.
Lakini kama Jose Mourinho alivyosema kuwa siku aliyotumia muda mwingi wa mapumziko kuzungumza na Mario Baloteli kuwa awe mwangalifu atakapomuingiza, ndiyo siku aliyoonyeshwa kadi nyekundu muda mfupi baada ya kuingia.
Kwa hiyo mazungumzo yaweza kuwa dawa au chachu ya kuboronga zaidi.
Pengine kuna uhusiano kati ya kutotulia kwake klabu moja na tabia hiyo ya uchezaji wa hatari. Kwanini Singida Black Stars waliamua kumpeleka Sowah Simba bila ya malipo yoyote wakati ni mchezaji ambaye ana sifa za kuuzwa kwa bei mbaya na ndio kwanza alikuwa ameanza kutumikia mkataba wake kwa walima alizeti hao?
Akiwa ametokea katika soka la ufukweni, Sowah alijiunga na Medema msimu wa mwaka 2023/24 na akafunga mabao 12 yaliyoisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa. Msimu uliofuata akaenda Al Nasr Bengazi ya Libya, ambako pia alidumua msimu mmoja kabla ya kuhamia Singida Black Stars wakati wa dirisha dogo.
Katika duru la pili la msimu ulioisha, Sowah alifunga mabao 13 kupitia mechi 14 tu na kuwaacha nyuma washambuliaji wengi waliocheza msimu mzima na sasa amejiunga na Simba na ameshaanza kuonyesha makali yake ya kutundika magoli. Pia alifunga bao moja la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba.
Safari hiyo ya misimu mitatu ndani ya timu nne yaweza kuonyesha kuwa ama ni mshambuliaji hatari anayesakwa kwa udi na uvumba, ama havumiliki kwa matendo yake yasiyo ya kianamichezo. Kilicho muhimu ni kwamba Sowah ni mtamu lakini ana miiba mingi.