Prime
Alichosema Gaye siyo zengwe, bali ana hoja
KUNA video zinazosambaa mitandaoni zikimuonyesha mwandishi wa habari na mchambuzi wa mpira wa miguu wa Ivory Coast, Mamadou Gaye akizungumzia kauli yake kuhusu maandalizi ya fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Uganda na Kenya.
Waandishi wa habri walikuwa wamembana baada ya Gaye kueleza kuwa Morocco wamepandisha viwango vya ubora wa fainali hizo zilizomalizika nchini humo wiki iliyopita kwa Senegal kutwaa ubingwa baada ya kupata bao pekee katika muda wa nyongeza.
Gaye, ambaye anajulikana zaidi kutokana na uchambuzi wake, hasa wa uongozi wa mpira wa miguu, alisema Morocco imejiandaa vizuri kimiundombinu ya mpira wa miguu na hasa ya usafiri.
Alisema pamoja na kwamba fainali za mwaka huu zimefanyika katika kipindi cha mvua, hakukuwa na tatizo lolote lililovuruga mashindano hayo makubwa Afrika kutokana na viwanja kujaa maji au utelezi.
Kuhusu miundombinu ya usafiri, Gaye alisema nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ilishaweka mazingira mazuri kiasi kwamba haikuwa tabu kwa timu, mashabiki na watalii walioenda Morocco kusumbuliwa na tatizo kubwa barani Afrika la foleni zisizoisha.
Alisema nchi nyingi Afrika zina barabara nzuri katikati ya miji, lakini unapotoka nje kidogo huwezi kukuta barabara za kuanzia njia mbili zinazoenda sehemu moja, kitu ambacho Morocco walikikabili.
Ukitoka Casablanca, mji mkuu wa Morocco hadi Marrakesh jiji jingine kubwa lililoko umbali wa kilomita 243, karibu saa tatu, unapita kwenye barabara ya lami ya njia mbili zilizotengwa na eneo kubwa la wazi.
Ni kama utoke Dar es salaam kwenda Morogoro ukiwa kwenye barabara ya njia mbili. Hii inawezesha kupunguza foleni zisizo na umuhimu na maana yake ni kwamba mashabiki wanaotaka kuwahi mechi ya AFCON 2027 kutoka Morogoro hawatarajii kucheleweshwa na malori ya mizigo ambayo hujazana barabarani na kuwa kero kwa magari mengine.
Gaye pia alizungumzia upatikanaji wa hoteli bora za kuanzia nyota tatu hadi tano, akisema ni ngumu kuzikuta nje ya miji mikubwa ya Afrika Mashabiki na nchi nyingine nyingi za Afrika mambo ambayo huangaliwa na watu wanaofika kufuatilia fainali hizo kubwa za soka.
Anasema kauli yake haimaanishi kuwa anaziponda nchi zetu, bali anazungumzia uhalisia uliopo ukanda wa Afrika Mashariki na nchi nyingine nyingi za Afrika, akiongeza kuwa Morocco imepandisha sana viwango vya ubora vya uandaaji mashindano hayo.
Awali kauli ya mwandishi huyo nguli ilichukuliwa kama kejeli na kuziponda nchi hizo tatu zitakazoandaa fainali za AFCON 2027 pamoja baada ya kufanikiwa kuandaa fainali za Kombe la Ligi za Ndani Afrika (CHAN) mwaka jana.
Gaye anasema muda wa fainali hizo unapokaribia, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) huwa halina huruma kwa nchi zilizopewa uenyeji, akisema huchukua mara moja uamuzi wa kuzihamishia nchi nyingine zilizo tayari kama ilivyokuwa wakati Kenya ilipokonhywa uenyeji wa fainali hizo miaka michache iliyopita, hali kadhalika Cameroon kuahirishiwa uenyeji wake na fainali hizo kwenda Misri mwaka 2019.
Fainali hizo za AFCON zimekuwa hazina muda maalumu kutokana na matatizo ya hali ya hewa na wenyeji kutokuwa tayari. Hivi sasa zinachezwa mwishoni mwa mwaka na mwanzoni mwa mwaka kutegemeana na hali ya hewa ya ukanda ambao umepewa fainali hizo.
Hiyo husababisha klabu nyingi kuwa na mizozo na nchi ambazo wachezaji wake wanatakiwa kucheza fainali za AFCON kwa kuwa zinafanyika kipindi ambacho ligi za Ulaya zinaendelea.
Mvua imekuwa changamoto kubwa zaidi kwa fainali hizo kutokana na viwanja vingi kutokuwa na mtandao mzuri wa kuruhusu maji kutoka uwanjani badala ya kutuama.
Hapa Tanzania, mechi ya pili ya fainali za mashindano ya Kombe la Shirikisho baina ya Simba na Al Masry ilibidi ihamishiwe Uwanja wa New Amaan mjini Unguja baada ya mechi moja ya nusu fainali kukumbwa na tatizo la Uwanja wa Benjamin Mkapa kujaa maji.
CAF imeufungia uwanja huo mara kadhaa kutokana na matatizo tofauti, lakini katika siku za karibuni viongozi wameuthibitishia umma kuwa marekebisho yote muhimu yaliyoagizwa yametekelezwa na uwanja sasa unaweza kutumika bila ya matatizo.
Kuhusu miundombinu ya usafiri, Gaye pia ameliweka vizuri suala hilo. Jiji la Dar es salaam linaendelea na uboresha mkubwa wa barabara zake, huku likiongeza mradi wa mabasi yaendayo kasi kwa ajili ya usafiri wa umma.
Hili litasaidia sana kurahisisha usafiri jijini Dar es salaam, lakini haina maana kwamba kama kuna mradi wa uboreshaji miundombinu ya usafiri basi Gaye apuuzwe. Gaye ana hoja nzuri ambazo zikizingatiwa zinaweza kupunguza tatizo linaloweza kujitokeza la usafiri.
Ni wazi kama kukiwa na timu nane jijini Dar es salaam ambazo zitakuwa zikienda viwanja mbalimbali kwa ajili ya mazoezi, kunaweza kuibuka tatizo la usafiri sehemu nyingi kutokana na ukweli kwamba timu hizo zitatakiwa ziwe na njia maalum na magari yazuiwe kwa muda hadi zifike zinapokwenda.
Pamoja na kwamba timu zitasafiri vizuri, ukweli utabakia kuwa watu wengine, wanaohusika au wasiohusika na fainali hizo atakumbana na adha ya foleni na matokeo yake kuchafua sura iliyolengwa kusafishwa machoni pa dunia ili Tanzania ionekane na sehemu bora ya kutalii.
Kuhusu malazi, hoteli nyingi za hadhi ya kuanzia nyota tatu zipo maeneo kama Mikocheni, Oysterbay na katikati ya jiji. Wakati Uwanja wa Mkapa utakaotumika kwa mechi hizo, na vile vingine vya mazoezi kama Gymkhana, vipo katikati ya jiji.
Hili nalo halina budi kuangaliwa. Hata kama utatuzi wake ni wa muda mrefu, yafaa kuona ni jinsi gani litashughulikiwa kwa kipindi cha fainali hizo.
Sina uhakika kuhusu ubora wa viwanja vyetu wakati wa mvua kubwa ambazo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, zimekuwa hazitabiriki hasa msimu wake.
Kuna mambo mengi ambayo hata Gaye hakuyazungumzia lakini ametufumbua macho tuanze kuangalia maandalizi yetu kwa jicho pana zaidi kuokoa rasilimali zilizotumika kuhakikisha Tanzania inaandaa mashindano hayo na inanufaika kwa kuyaandaa.
Watu kama kina Mamadou Gaye ambao wanadiriki kusema kile wanachokiona hakiendi sawa, wasikilizwe na hoja zao zipewe tafakari nzito badala ya kujibiwa kirahisi kwa kumpachika sifa ya kutokuwa na uzalendo. Alichokisema sio zengwe, ni uhalisia ambao ni muhimu kutufungua masikio na macho.