Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CHAN kama AFL funzo la wakubwa kutojipanga

ZENGWE Pict


HATIMAYE Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limetangaza rasmi kufuta mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) kutokana na kuzidiwa na gharama za kuyaendesha tofauti na yale ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo hayakauki wadhamini.


CHAN yamekuwa ni mashindano yasiyo na msisimko na mara nyingi yamekumbwa na tatizo la nchi kujitoa, zikiongozwa na Misri ambayo ilishakuwa na mtazamo hasi tangu mashindano hayo yalipotangazwa mwaka 2008 na kuanza rasmi mwaka 2009.


CAF imetangaza kuyafuta mashindano hayo kutokana na kuhangaika kutafuta wadhamini bila ya mafanikio, hivyo kubeba mzigo mkubwa wa gharama na Rais wa shirikisho hilo, Patrice Motsepe alisema wameona mashindano hayo hayafai.

Misri ilishasema tangu awali kuwa mashindano hayo ni ya kujifariji na hayana umuhimu wowote, lakini ilipoanza kushiriki ikabaini jinsi yanavyoingiliana na mashindano yake ya ndani na hivyo kusababisha nchi hiyo, yenye mafanikio makubwa katika soka barani Afrika, kujitoa kila mara au ushiriki wake kuwa shakani.

ZENG 01

Mara nyingi viongozi wa mashirikisho ama vyama vya soka vya nchi wamekuwa wakikubali kila kinachoamuliwa na CAF au Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) bila ya kufikiria athari zake kwa mashindano yao ya ndani.

Wakati CAF inatangaza kuanzisha mashindano ya African Football League (AFL) nchi ambazo zinajali sana mashindano yake ya ndani, ikiwemo Afrika Kusini, ziliipinga ligi hiyo kwa maelezo inazidisha uwingi wa mashindano na hivyo kuathiriki ligi zake.

Awali, Chama cha Soka cha Afrika Kusini kilisita kuibadilishia Mamelodi Sundowns ratiba za mechi zake za Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa maelezo waandaaji walichelewa kutoa taarifa na kikawa na wasiwasi dhidi ya umiliki hasa wa CAF wa mashindano hayo baada ya kupata taarifa inayoonyesha makao makuu yao ni Kigali, Rwanda badala ya Cairo, Misri ziliko ofisi za CAF.

Kama wasiwasi wao ulivyokuwa wa kweli, African Football League (AFL) ikafanyika mara moja tu kwa kuanzia hatua ya robo fainali. Kwa kutumia mchanganuo wa ubora wa CAF, Simba ya Tanzania ilikuwa moja ya timu nane zilizoshiriki mashindano hayo ya kwanza na ya pekee.

ZENG 05

Wasiwasi huenda mashindano hayo yalipachikwa umiliki wa CAF huku yakiandaliwa na kikundi kimoja cha watu, unaweza kuwa wa kweli, kitu ambacho kinazidi kuthibitisha wasiwasi ni akili.

Barani Ulaya, mashindano yaliyopachikwa jina la European Super League yalikwama baada ya kutangazwa tu yanaanzishwa. Mashabiki walifikia hatua hadi ya kukwamisha mechi ya Ligi Kuu England baina ya Manchester United na Liverpool, wakionyesha kutokubaliana na uamuzi wa kuanzisha mashindano hayo ambayo yangeandaliwa na taasisi ambayo haikuwa na uhusiano na Chama cha Soka Ulaya (UEFA).

Mfumo wa kupata washiriki na muundo unaozipa baadhi ya timu haki ya kutoshuka daraja, ulionekana unapingana na utamaduni wa kawaida wa mpira wa miguu ambao hutoa nafasi kwa anayefanya vizuri kushiriki hatua yoyote anayoifikia, tofauti na mtindo uliotakiwa kutumika wa klabu maarufu kutoshuka daraja.

Hata FIFA ilipotangaza kupanua muundo wa Klabu Bingwa ya Dunia kutoka klabu nane hadi 32 kutoka mashirikisho sita ya mabara, baadhi ya nchi, vyama vya wachezaji wa kulipwa na umoja wa ligi za nchi, ulipinga vikali fainali hizo ukisema zinaongeza idadi ya mechi na hazikuzingatia afya za wachezaji wanaotakiwa wapate muda wa kutosha mwishoni mwa msimu kabla ya kuanza msimu mpya.

Kwa hiyo, ukiangalia CHAN unajiuliza kulikuwa na umuhimu gani wa kuanzisha mashindano hayo na kama kulikuwa na utafiti wa kutosha kujua kama yangekuwa na vyanzo vizuri vya mapato. Hakukuwepo na utafiti wa kutosha kama ilivyokuwa kwa African Football League.

ZENG 04

Na viongozi wa nchi wanachama hawakupata muda wa kutosha kuhoji umuhimu wa mashindano hayo na uwezo wake wa kuingiza fedha.

Mashindano ya CHAN yalikuwa yanashirikisha wachezaji wanaosakata soka kwenye ligi za ndani ya nchi zao, hali iliyoyafanya yashirikishe wachezaji ambao hawana umaarufu mkubwa nje ya nchi zao na hivyo kutofuatiliwa na wengi na kukosa msisimko kama ule wa AFCON.

Na mashindano yakikosa msisimko ni dhahiri kuwa hayataweza kuvutia wadhamini na hata mauzo ya haki za televisheni hayawezi kuwa ya bei kubwa na matokeo yake ni mzigo kwa waandaaji.

ZENG 03

Mwaka jana wakati fainali hizo zilipofanyika Tanzania, Kenya na Uganda athari ilionekana kubwa katika Ligi Kuu Bara, ambayo iliisha Juni 25, ikichangiwa pia na mzozo baina ya Simba na Yanga.

Siku chache baada ya kuisha, timu ya taifa ikawa inatakiwa iende kucheza mechi za michuano ya awali ya Kombe la Dunia na zile za AFCON ambazo ilipoteza dhidi ya Morocco, Zambia na Niger. Kauli ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ baada ya mechi hizo ilikuwa ni “uchovu, uchovu, uchovu”.

Lakini hatukujua uchovu huo ulisababishwa na nini. Wale wa Misri na wenzake wanajua kuwa uchovu huo ulisababishwa na uwingi wa mechi ambazo wachezaji wanashiriki katika msimu mmoja.

ZENG 02

Kwa hiyo, kufutwa kwa mashindano ya CHAN kunatoa elimu kwa viongozi wa soka wa nchi kuhoji kila uamuzi wa vyombo vya juu ili yatolewe maelezo ya kutosha ya kuwawezesha kupanga mambo yao vizuri. Ni muhimu sana kulinda mashindano ya ndani kwa kuwa ndiyo yanayowezesha vyama vya nchi kuwa imara kifedha, yanayovutia wadhamini  na ndiyo yanayowezesha nchi kutengeneza vizuri program zake za maendeleo.

Viongozi wa mashirikisho ya bara ama kimataifa huanzisha mashindano kwa lengo la kutega wadhamini na kutengeneza haki za matangazo, kitu ambacho pia kinatakiwa kifanywe na viongozi wa soka wa nchi. Kadri tunavyokubali kila kinachoamuliwa na CECAFA, CAF na FIFA tunaathiri mashindano yetu ya ndani.

Ni vizuri Motsepe na wenzake wameona CHAN haina umuhimu na kuamua kuiga wenzetu wa Ulaya kwa kuanzisha Ligi ya Mataifa (African Nations League) ambayo hayataweza kuathiri kwa kiwango kikubwa mashindano ya nchi wanachama huku yakiwa na uwezo mkubwa wa kuingiza fedha kwa kuwa hayana masharti ya aina ya wachezaji wanaotakiwa kuvutia.

Ni dhahiri wale nyota wa Afrika walio Ulaya, Arabuni na hata hapa hapa Afrika, lakini nje ya nchi zao, watashiriki na kuweka msisimko uleule wa AFCON.