Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Singida Black Stars jahazi limeyumba


KAMA kuna timu ambayo huwa inakosa maisha marefu au kutosomeka katika Ligi Kuu Bara, basi ni Singida Black Stars. Historia inaihukumu kuwa inaweza kuwa na nguvu kubwa, kisha ikapotea kwenye mazingira ya kutatanisha na baadaye ikaja kuibuka tena.


Dalili hizo zimeanza tena kwa Singida Black Stars ambayo ikiwa ni misimu miwili tu ikitokea katika ile iliyokuwa inaitwa Ihefu SC, kisha ikaibuka na nguvu kubwa, lakini sasa mambo ni kama yamekuwa yaleyale ikilazimisha kurudi nyuma.

Ndani ya misimu miwili mwanga mzuri wa Singida ulianza kuonekana ikizitisha timu kubwa nchini katika msimu wa kwanza, ikishusha mastaa bora na wenye viwango vikubwa ambao hapo awali walikuwa wamezoeleka kuonekana Simba, Yanga au hata Azam

Sio kushusha wachezaji wenye ubora, lakini walioweza kuibeba timu hiyo na haikushangaza kuona msimu uliopita ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Bara (FA), kwa kuing’oa Simba hatua ya nusu fainali tena kwa kipigo cha aibu cha mabao 3-1. Bahati mbaya ilipoteza mbele ya Yanga kwa mabao 2-0.

Lakini, ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya nne nyuma ya mabingwa, Yanga, Simba na Azam, na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, na kabla ya kuanza kuwasha moto, jamaa walishabeba taji la Kombe la Kagame 2025.

Ndio. Singida BS ilibeba ubingwa wa Kombe la Kagame 2025 kwa kuinyuka Al Hilal ya Sudan, likiwa ndilo taji la kwanza kubwa tangu kuzaliwa kwa timu hiyo na kuonyesha kwamba pengine ndio mwanzo wa kuja kutingisha kwa kuandika rekodi ya kuchukua mataji mengine makubwa.

Na ni ndani ya muda huohuo ikaandika tena rekodi na historia ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, japo kwa sasa imeshapoteza nafasi ya ku-cheza robo fainali baada ya wikiendi iliyopita kupoteza nyumbani mbele ya CR Belouizdad ya Algeria. Singida imebaki na pointi nne.

Mambo yameanza kubadilika ghafla ndani ya Singida ikiwa katikati ya muda ambao wadau mbalimbali walikuwa wanasubiri kuona mwendo wa timu hiyo utakuwaje.


Kupoteza mastaa bora

Singida Black Stars ikiwa vitani kama utani ilianza ‘kugawa’ mastaa  wakubwa  waliotikisa nchini kwa klabu mbalimbali wakienda kuziimarisha klabu hizo ambazo nyingi ndizo shindani kwenye mbio za makombe ya ndani.

Ukiviangalia vikosi vya Simba na Yanga vyote vimenufaika na mastaa wa Singida - tena wale ambao wana viwango vikubwa wakivunwa kirahisi kwa staili ya bure na klabu hizo kisha kwenda kushindania ubingwa, huku yenyewe ikibaki kuwania nafasi ya tatu na ile ya nne msimu uliopita.

Straika aliyemaliza kama kinara wa mabao wa timu hiyo, Jonathan Sowah aliyeingia dirisha dogo la msimu uliopita akifunga mabao 13 kupitia mechi 14 yupo Msimbazi sambamba na kiungo Clatous Chama na beki Nickson Kibabage, wakati beki Frank Assinki, kiungo Mohammed Camara na kipa Hussein Masalanga wapo Yanga mbali na wale waliopo klabu nyingine za Ligi Kuu Bara.

Simba na Yanga ‘zinapoyumba’ zimekuwa zinapiga simu tu na kuchukua staa yeyote zinayemtaka na kwenda kuendelea naye huku yenyewe ikibaki na wachezaji wa kawaida jambo ambalo limekuwa likiwashangaza baadhi ya wadau wa michezo wakijiuliza malengo ya Singida yalikuwa yapi wakati inawatafuta wachezaji hao bora?


Kupoteza makocha bora

Yanga iliyumba kidogo baada ya kuondoka kwa makocha wake msimu uliopita, lakini ilipotua Singida ndani ya muda mchache ilichukua kocha wa maana, Hamdi Miloud. Kocha huyo aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo na Kombe la Shirikisho kadhalika kwa mara ya nne pia.

Baada ya hapo ilishusha makocha wengine kadhaa kabla ya msimu huu kuamua kumrejesha kocha wa zamani wa Yanga aliyeipa mataji ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na kuipeleka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo, Miguel Gamondi.

Ni Gamondi ndiye aliiwezesha pia Singida kutwaa ubingwa wa Kagame Cup 2025, kisha kuiingiza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni rekodi kwa klabu hiyo, na hata kwa kocha huyo kucheza hatua ya makundi mara tatu mfululizo akiwa na timu mbili tofauti. Yaani Yanga na Singida.

Hata hivyo, kocha huo (Gamondi) ameondoka kirahisi Singida, kwani awali alikuwa kwenye rada za Simba wakati akiwa na kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) kilipokuwa kikijiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizofanyika mwaka huu huko Morocco.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimchukua Gamondi kuwa kaimu kocha mkuu wa Stars kuchukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’, lakini kitendo cha kuifikisha timu hiyo hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, ikawa ni tiketi ya kumng’oa jumla kocha huyo na kuondoka Singida.

Makocha hao wote wawili yaani Gamondi na Miloud wanaonekana wangeipa mafanikio makubwa Singida. Ni Gamondi tu aliyeipa ubingwa wa Kagame na kuipeleka makundi, lakini ikapotea kirahisi kwa kutolewa na Singida yenyewe ni kama haijali vile.


Mbio za ubingwa

Mwandishi wa makala haya aliwahi kuzungumza na mmoja wa mabosi wa Singida aliyedai baada ya kuwa kwenye kipindi cha kutengeneza timu msimu huu 2025/26, wanataka mojawapo wa makombe mawili na kama sio ubingwa wa Ligi Kuu Bara, basi uwe ule wa Kombe la Shirikisho. Mpango ulikuwa unakwenda vizuri kwani timu hiyo imeshabeba Kagame Cup 2025 na kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, hilo la kubeba makombe Bara linaweza kukumbana na vikwazo kutokana na namna hali ya kikosi ilivyo kwa sasa, na ni kama kimepoteza silaha kubwa muhimu ambazo zingefanikisha kushinda ndoto hizo mbele ya Simba, Yanga na Azam.

Rekodi zinaonyesha kuwa, Singida ilishinda mara ya mwisho katika Ligi Kuu Bara Septemba 30, mwaka jana, ilipoifunga Mashujaa FC kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na straika Elvis Rupia aliyefunga sekunde chache kabla ya mapumziko.

Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya 14 ikiwa imeshacheza mechi saba, ikishinda mbili na kutoka sare tatu, ikipoteza pia mbili na kuvuna pointi tisa, ikifunga mabao matano na kufungwa sita.

Lakini, kikosi hicho kina mastaa wachache wenye makali waliosalia ambao wana kazi nzito ya kukipa ubingwa kutokana na baadhi kuondoka kwenda kuimarisha vikosi vingine ambao inaaminika kabisa huko ndiko wanakoweza kwenda kubeba ubingwa na sio katika ile timu iliyowaleta nchini.

Wakati huu ambao Singida ilikuwa na timu bora wakati ilipouanza msimu ikiwa pia imefanikiwa kujenga uwanja wake, ikizishinda timu kubwa na kongwe nchini, ilitakiwa kuonyesha kuwa ina kiu ya mafanikio makubwa zaidi uwanjani kwa kuchukua mataji muhimu na kuweka alama isiyosahaulika.


Hatma yake nini?

Namna wachezaji wakubwa wanavyopukutika katika kikosi cha Singida Black Stars inaleta shaka juu ya hatma ya kikosi hicho kwenye maisha yake, hasa kama mambo yataendelea hivi yalivyo kwani mbele ya safari inaweza kujikuta inapoteza hadhi  ya kuwa ndani ya tano bora.

Na ikumbukwe kwamba ikishatoka hapo wadau wa soka itawaachia maswali mengi mazito ambayo hayatakuwa majibu ya moja kwa moja zaidi ya kuwa hisia zisizo na mashiko. Ni vyema ikarejea haraka katika misingiiliyowaaminisha mashabiki na wadau kwamba imekuja kuleta ushindani na kuzipa changamoto Simba, Yanga na Azam kutobweteka. Kila la heri Singida BS.