Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dira ya taifa 2050 itakavyoimarisha michezo kwa afya na ustawi wa wananchi

DIRA Pict

Muktasari:

  • Michezo siyo burudani pekee, bali ni nyenzo pia ya kuboresha afya ya mwili na akili, kukuza maadili, kuimarisha umoja wa kitaifa, kuibua vipaji na kuongeza tija katika uzalishaji, ikiwa ni njia muhimu ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050, inalenga kujenga Tanzania yenye wananchi wenye afya bora, uchumi imara, jamii jumuishi, mazingira salama na maendeleo endelevu, japo ili kufanikisha maono hayo sekta ya michezo ni moja ya nguvu zake muhimu.

Michezo siyo burudani pekee, bali ni nyenzo pia ya kuboresha afya ya mwili na akili, kukuza maadili, kuimarisha umoja wa kitaifa, kuibua vipaji na kuongeza tija katika uzalishaji, ikiwa ni njia muhimu ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

Wakati Dira ya Taifa 2050, ikibeba maono makubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapiga hatua katika mambo mbalimbali, zipo mbinu zinazoweza kutumika ili kuimarisha michezo kwa afya na ustawi wa wananchi, kama ambavyo Mwanaspoti linavyoelezea.

DIR 01

USHIRIKI WA WANANCHI

Ikiwa kutakuwa na ushiriki wa wananchi kwa wingi katika michezo na mazoezi ya mwili, itakuwa ni moja ya njia muhimu ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, unene kupita kiasi na kuboresha pia afya ya jamii.

Magonjwa mengine ni saratani zinazohusiana na mtindo wa maisha na magonjwa ya moyo na mazoezi hayo yataongeza nguvu kazi yenye afya kwa jamii, kupunguza gharama za matibabu na kuongeza pia uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.

DIR 03

UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU

Dira hiyo itahamasisha uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya michezo ili kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa sawa za kushiriki zaidi, zikiwemo viwanja vya michezo, kumbi za mazoezi, mabwawa ya kuogelea, njia za kutembea na kukimbia.

Kuanzishwa kwa wingi viwanja vya mazoezi, kuanzia ngazi za vijiji, kata, halmashauri na miji, itasaidia miundombinu hiyo kuwezesha wananchi kufanya mazoezi kwa usalama na urahisi na kuongeza ushiriki wa jamii yote kupenda kushiriki michezo.


MICHEZO SHULENI

Ikiwa Dira itaweka msisitizo katika michezo ya shule na vyuo kama msingi wa kujenga taifa lenye afya na rasilimali watu wenye ushindani, itasaidia kuunganisha kikamilifu mfumo wa elimu na kuwajengea wanafunzi afya bora, nidhamu na uzalendo.

Kupitia mashindano ya shule na vyuo, vipaji vitaibuliwa mapema na kuendelezwa kwa mfumo unaowezesha vijana kwa ujumla kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa, jambo litakalosaidia kupata kizazi bora cha sasa na baadaye chenye ushindani.


KUBORESHA AFYA YA AKILI

Katika dunia inayokabiliwa na ongezeko la msongo wa mawazo, huzuni na changamoto nyingine za afya ya akili, michezo ni sehemu muhimu ya kujenga furaha, kuongeza kujiamini, kuimarisha uhusiano wa kijamii na kuboresha pia ustawi wa kijamii.

Ushiriki katika michezo pia utapunguza tabia hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu na vitendo vya ukatili miongoni mwa vijana, jambo ambalo kwa sasa limekuwa likishika kasi na kupunguza nguvu kazi ya taifa ya kuleta maendeleo.

DIR 02

USHIRIKI JUMUISHI

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itakuza ushiriki jumuishi katika michezo kwa kuhakikisha wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa za kushiriki, huku Serikali na wadau mbalimbali wakiweka mazingira rafiki juu ya hilo.

Serikali na wadau wataweka mazingira rafiki, sera na miundombinu inayozingatia usawa na ujumuishaji na hatua hii itaimarisha mshikamano wa kijamii, kupunguza ubaguzi na kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na mchango wa michezo.


UKUAJI WA UCHUMI

Michezo itachangia ukuaji wa uchumi kupitia ajira na biashara, ambapo Dira ya 2050 itahamasisha uwekezaji katika klabu za michezo, akademi, viwanda vya vifaa vya michezo, huduma za tiba ya michezo, utangazaji, masoko na utalii wa michezo.

Hatua hii muhimu itazalisha ajira kwa makocha, waamuzi, wataalamu wa afya ya michezo, waandaaji wa matukio, wanamichezo na wajasiriamali mbalimbali, jambo litakaloongeza kasi ya uchumi na kuzidisha kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.

DIR 05

MFUMO ENDELEVU WA UTAMBUZI

Dira hiyo itakuza maendeleo kwa kuanzisha mfumo endelevu wa utambuzi, malezi na ukuzaji wa wanamichezo na vipaji vitatambuliwa tangu ngazi ya jamii na shule, kisha kuendelezwa kupitia vituo maalumu vya mafunzo na akademi za michezo.

Mfumo huo utaiwezesha Tanzania kupata wanamichezo wenye uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano ya kikanda, Bara la Afrika na dunia, huku wakiiwakilisha nchi kwa heshima kwa kuitangaza na kuongeza mapato kupitia michezo yote ya kulipwa.


MATUMIZI YA TEKNOLOJIA

Matumizi ya teknolojia yataimarisha pia maendeleo ya michezo na afya ya wananchi kwa kutumia mfumo wa kidijitali ambao utatumika kusajili wanamichezo, kufuatilia maendeleo ya vipaji, kupanga mazoezi na kuboresha huduma za tiba michezoni.

Aidha, teknolojia itarahisisha utoaji wa elimu ya afya, mazoezi na lishe kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali, jambo litakalosaidia wanamichezo kushiriki na kuleta ushindani na kuzidisha kuitangaza Tanzania kimataifa.

DIR 04

USHIRIKIANO WA SERIKALI

Dira ya 2050 itaimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu na wadau wa maendeleo katika kuendeleza michezo na kuchochea ongezeko la uwekezaji, ubunifu na uendelevu wa programu za michezo.

Kwa upande wa sekta binafsi itahamasishwa kufadhili mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, kujenga miundombinu na kuwekeza katika maendeleo ya wanamichezo kupitia uwajibikaji kwa jamii na kuongeza ufanisi kwa wanamichezo kiujumla.


KUIMARISHA MAADILI

Michezo itatumika kama nyenzo ya kuimarisha maadili, uzalendo na mshikamano wa kitaifa na kupitia mashindano mbalimbali, wananchi watajifunza kuheshimu sheria za nchi yetu husika, kufanya kazi kwa pamoja, kushindana kwa haki na kuvumiliana.

Pia, michezo itakuwa chombo muhimu cha kuunganisha watanzania wote bila ya kujali tofauti za kijamii, kiuchumi, kidini au kikabila, ikiwa ni hatua nyingine muhimu ya kuendelea kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kukuza utamaduni wetu.


UTAWALA BORA

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itasisitiza uongozi bora na utawala wenye uwazi katika sekta mbalimbali za michezo ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa rasilimali, matumizi sahihi ya fedha, uwajibikaji na utoaji huduma bora kwa wanamichezo.

Utawala bora ni mfumo mzuri wa uongozi unaozingatia uwazi, uwajibikaji, usawa, ushirikishwaji wa wananchi na utawala wa sheria, ukihakikisha rasilimali zote za umma zinatumika kwa ufanisi mzuri ili kuleta maendeleo, haki na ustawi wa jamii.


UTAFITI NA UBUNIFU

Ikiwa utafiti na ubunifu vitaimarishwa, vitasaidia maendeleo ya michezo, kwa sababu taasisi za elimu ya juu na vituo vya utafiti vitafanya tafiti zaidi kuhusu afya ya wanamichezo, lishe zao, tiba ya michezo, sayansi ya mazoezi na teknolojia.

Kwa jumla, Dira 2050 inatoa fursa kubwa ya kuifanya michezo iwe sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa, kupitia uwekezaji katika miundombinu, ukuzaji wa vipaji, ushiriki jumuishi, matumizi ya teknolojia, utawala bora na ushirikiano wa wadau.

Utekelezaji madhubuti wa mikakati hii utaifanya Tanzania iwe ni taifa ambalo michezo sio burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo endelevu, afya bora, umoja na ushindani wa kimataifa, kuongeza ajira na ustawi wa wananchi kiujumla.