Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majeraha yatesa wachezaji, bima ikibaki kuwa ndoto - 1

BIMA Pict

Muktasari:

  • Utafiti wa Mwananchi unaonyesha kati ya timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo msimu wa 2025/26 ni nane pekee zilizotoa bima ya afya kwa wachezaji wake, huku kwa upande wa Zanzibar hali ikiwa mbaya zaidi.

KATIKA soka, afya ya mchezaji ni nguzo muhimu ya mafanikio ya timu yoyote. Hata hivyo, hali halisi katika Ligi Kuu Bara inaonyesha taswira tofauti kwani utekelezaji duni wa kanuni za bima ya afya umeacha pengo linalowaweka wachezaji katika hatari ya kiafya na kiuchumi.

Utafiti wa Mwananchi unaonyesha kati ya timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo msimu wa 2025/26 ni nane pekee zilizotoa bima ya afya kwa wachezaji wake, huku kwa upande wa Zanzibar hali ikiwa mbaya zaidi.

Hali hii inaashiria ukubwa wa tatizo lililopo na namna ambavyo sheria zilizowekwa zinavyopuuzwa kwa kiwango kikubwa.

BIM 01

USHUHUDA WA WAATHIRIKA

Gerald Mdamu ni miongoni mwa waathirika kutokana na kutotekelezwa kwa sheria. Mwanasoka huyu aliyevitumikia vilabu vya Mwadui FC na Police Tanzania FC akiwa mshambuliaji alipata ajali iliyosababisha miguu yote miwili kuvunjika.

Aliacha kucheza soka, huku akipitia kipindi kigumu cha matibabu ya muda mrefu.

“Wachezaji wanachukulia poa suala la bima ya afya ila wataona umuhimu wake wakati wa matatizo, kama klabu niliyokuwa naitumikia ingekuwa na huduma hii huenda leo nisingekuwa hapa, nimefika hapa kwa sababu ya kuchelewa kupata matibabu,” anasema.

Kiungo wa Coastal Union, Greyson Gwalala, anaeleza jinsi alivyopata jeraha la goti lililomuweka nje kwa mwaka mzima huku akilazimika kutumia fedha zake binafsi kwa matibabu.

Anasema gharama zilifikia hadi Sh5 milioni kiasi ambacho kilizidi uwezo wake na kumlazimu kutegemea msaada wa watu binafsi.

Gwalala anasema awali klabu ililipia gharama za matibabu lakini baadaye kuna mshabiki alimshika mkono kwa asilimia kubwa.

“Hapa Coastal Union hakuna bima kwa wachezaji, hivyo sheria ikisimamiwa utakuwa msaada mkubwa,” anasema.

Kutokana na aliyoyapitia anasema: "Niliona umuhimu wa bima. Kama ningekosa mtu wa kunisaidia basi ningekuwa sichezi mpira kwa sababu gharama za matibabu kwangu zilikuwa kubwa kuliko uwezo wangu.”

BIM 05

Anasema: "Maisha ya mchezaji yako hatarini, wakati wowote ule anaweza kupata majeraha, kwa hiyo bima ni suala la muhimu zaidi."

Changamoto hiyo si ya mtu mmoja. Wachezaji wengi wamejikuta wakibeba mzigo wa matibabu pindi wanapopata majeraha kazini, hali inayokiuka haki zao za msingi kama wafanyakazi.

BIM 02

HALI NDANI YA KLABU

Kutoka Yanga, mmoja wa wachezaji wakongwe anasema hajawahi kupewa bima ya afya tangu asajiliwe miaka minne iliyopita, ingawa alipata jeraha la goti na kufanyiwa upasuaji kwa gharama za klabu.

Singida Black Stars inakiri kukosa bima msimu mzima baada ya kampuni yao ya awali kumaliza mkataba. Klabu hiyo inaeleza awali ilikuwa na bima, lakini haikuwa ya kiwango cha kugharimia majanga makubwa kama majeraha yaliyohitaji upasuaji.

Ofisa habari wa klabu hiyo, Hussein Masanza anasema: "Endapo mchezaji atapata majeraha makubwa basi tunaingia gharama kumpatia matibabu na kuhakikisha anapona kabisa."

Kwa upande wake, Pamba Jiji FC inasema wachezaji wake hawana bima licha ya kuwa ni takwa la kisheria.

BIM 06

Daktari wa timu hiyo, Dishon Chacha, anasema klabu hulazimika kusubiri bajeti ndipo itoe matibabu, hali inayoweza kuchelewesha huduma muhimu kwa mchezaji.

Timu nyingine zilizotajwa kutokuwa na bima katika msimu huo ni Fountain Gate FC, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji FC, ambazo wachezaji wanapopata changamoto hutegemea msaada wa timu au fedha zao wenyewe.

KMC FC nayo inakiri kutokuwa na bima kwa wachezaji na watumishi wake, huku ikisema wachezaji wamekuwa wakitibiwa katika hospitali ya Magomeni na kesi kubwa kupelekwa hospitali kubwa zaidi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka anasema: “Nikiri kwamba hatuna bima kwenye timu yetu, tunatambua kwamba ni takwa la kikanuni lakini bado uongozi ulikuwa kwenye kutafuta njia mwafaka wa kulipatia ufumbuzi hili.”

Fountain Gate FC pia inasema bado haijapata bima kwa wachezaji wake, ingawa imeingia mkataba na hospitali moja kubwa jijini Arusha ambayo inawatibu wachezaji na watumishi wa timu hiyo.

“Kuna mambo mengi ya kuzingatia katika bima hasa kwa wachezaji, licha ya kwamba hawana bima haina maana kwamba hakuna mfumo mzuri wa kuwapatia matibabu. Uongozi tumeingia mkataba na hospitali moja kubwa jijini Arusha, ambayo kila mchezaji akipata shida anakwenda pale hakuna sababu ya kuwa na pesa anatibiwa na klabu inalipa kila kitu,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kelvin Herry.

BIM 03

WALIO NA BIMA

Hata hivyo, kuna mifano michache ya kuigwa. Simba SC, Azam FC, Mbeya City FC, Tanzania Prisons, TRA United, Mashujaa FC na Namungo FC zimeweka mifumo ya bima kwa wachezaji wao.

Simba SC kupitia msemaji wake, Ahmed Ally anaeleza kuwa kila mchezaji na familia yake wanapata huduma ya bima.

"Kila mchezaji aliye ndani ya klabu hii ana bima yake binafsi lakini pia na watoto wake wawili na mke wake. Hazikuishia kwa wachezaji na makocha pekee, hata sisi watumishi wa Simba tumepatiwa,” anasema.

Hata hivyo, anasema matibabu ni ya ndani ya nchi pekee na siyo nje.

BIM 07

Athumani Amiru, mmoja wa viongozi wa klabu ya Mashujaa FC anasema bima ni suala la lazima kwani wengi wao ni wafanyakazi.

"Kesi za mchezaji kupata majeraha ambayo bima haiwezi kumsaidia ni chache lakini ikitokea huwa tunalifanyia kazi kwa kumtibia mpaka atakapopona," anasema.

Ofisa habari wa TRA United, Christina Mwagala anasema wachezaji wao wote wana bima ya afya kwa kuwa ni takwa la kikanuni.

Mchezaji wa JKT Tanzania, David Bryson anasema hupatiwa bima mwanzoni mwa msimu.

BIM 04

ILIVYO ZANZIBAR

Kwa Zanzibar, Katibu wa ZFF, Hussein Ahmada anasema sheria zipo kimya katika suala la bima ingawa wanaendelea kuhakikisha wachezaji wanapimwa afya kila mwanzo wa msimu.

“Sisi kama wasimamizi wakuu wa wachezaji kwa upande wa Zanzibar, nikiri tumeshindwa kuunda sheria ambazo zitasimamia klabu kutimiza kwa upana suala la afya. Moja kati ya mipango yetu ni kuhakikisha wachezaji wanaanza kuwa na bima za afya.”

Anasema walishakaa na wadau kuzungumzia suala hilo lakini bado halijakamilika, lakini wanahakikisha kila mwanzo wa msimu wachezaji wanapata vipimo.

“Sijawahi kupata kesi ya mchezaji aliyewahi kushindwa kupata matibabu au majeraha makubwa, ingawa naamini wapo na wameamua kuacha soka,” anasema.

Kamishna wa Michezo Zanzibar, Ameir Mohamed anasema Serikali inategemea mashirikisho kusimamia suala hilo, huku akibainisha kuwa wachezaji wengi wameacha mpira kutokana na majeraha na kushindwa kupata matibabu ya kutosheleza.

Katibu wa JKU, Khatib Shadhil Khatibu anasema wachezaji wa kikosi hicho wanapatiwa bima ya afya.

“Wachezaji ambao tunao hapa wengi ni wanajeshi kwa hiyo bima ni jambo la lazima, ingawa tunao wachache ambao ni raia wa kawaida ambao nao wanapata nafasi ya huduma katika hospitali yetu,” anasema.

Katibu wa timu ya Mlandege FC, Hussein Ahmada anasema: “Tumeanza utaratibu wa bima mwaka jana kwa kufuata kanuni za CAF kwa sababu tulishiriki michuano ya kimataifa na ilitulazimu tuwe nazo.”