Prime
Simba haina budi kumsikiliza Kigwangalla
Pengine lengo lilikuwa ni kumfedhehesha na baadaye kumnyamazisha asizungumzie tena kile anachoona ni sahihi na kukosoa kisichofaa katika mchakato wa mabadiliko wa klabu ya Simba.
Lakini bomu zito alilorushiwa linaonekana kumpa hamasa ya kuzungumza siku hadi siku, akipinga mwenendo wa mabadiliko hayo na jinsi yalivyokumbatiwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kongwe kutoka Mtaa wa Msimbazi.
Ni Hamisi Kigwangalla, mbunge wa Nzega, mkoani Tabora na waziri wa zamani ambaye anajielezea ni shabiki na mwanachama wa Simba Sports Club.
Wakati fulani alipokosoa mwenendo wa mchakato huo, Mohamed Dewji, ambaye anachukuliwa kama mwekezaji wa Simba anayemiliki asilimia 49 licha ya fedha hizo kutolipwa na badala yake kuwekwa akaunti ya (escrow), alisema maoni hayo alitoa kwa sababu ya hasira kwa sababu alimnyima mkopo wa pikipiki.
Hiyo hakuichukulia kama katazo la kuzungumzia mchakato huo, bali limemfanya aendelee kuuzungumzia kila wakati anapopata nafasi.
Katika siku za karibuni kwenye ukurasa wake wa mtandaoni, Kigwangallah ameeleza kuna wanachama wanamshawishi achukue fomu katika uchaguzi ujao ili agombee nafasi ya mwenyekiti wa Simba.
Lakini anasema hawezi kugombea kwa sababu ya mambo mawili; kwanza hajioni kama atawezana na siasa za sasa za mpira wa miguu kuiongoza klabu kubwa kama Simba; anasema sababu ya pili ni imani yake tatizo la Simba si mtu mmoja (kama inavyodaiwa kuwa tatizo ni mwenyekiti wa sasa, Murtazar Mangungu).
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni daktari, anasema tatizo kubwa kwa klabu hiyo iliyoanza mchakato wa mabadiliko miaka minane iliyopita, ni uongozi na umiliki. Anasema klabu inatakiwa iwe na muundo unaopaswa kumpa mwenyekiti, Bodi ya Wakurugenzi na wanachama mamlaka, uwajibikaji na heshima.
“Simba inahitaji mfumo wa uongozi ulio wazi, mgawanyo wa mamlaka na dhana ya kuchungana (cxhecks and balance), uwajibikaji na bodi yenye nguvu inayowakilisha masilahi ya klabu na wanachama,” anasema katika ukurasa wake.
Anasema Simba haina budi kuweka sawa muundo wa umiliki, akisema si sawa kwa klabu kubwa ya wanachama kama Simba kuwa na mwekezaji mmoja ili kuondoa mtu mmoja kutawala klabu yote, akitaka asilimia 49 za hisa zilizotengwa kwa wawekezaji ziuzwe kwa wawekezaji kuanzia watatu, na yuko tayari kununua baadhi ya hisa.
“Kura ya veto (nguvu ya kura ya turufu) kwenye masuala ya msingi isiwe mikononi mwa mwekezaji mmoja. Itokane na angalau nusu ya hisa zote zinazomilikiwa na wawekezaji,” anasema mbunge huyo.
Anashauri mwekezaji wa sasa apewe asilimia 15 za hisa, wa pili pia apewe kiasi hicho wakati wa tatu achukue zitakazobaki katika hizo asilimia 49, yaani asilimia 14.
Na mwishoni anadokeza: “Kama thamani ya asilimia 49 ni TZS bilioni 20, kampuni yangu ya HK Group iko tayari kununua kwa cash (fedha taslimu), asilimia 9-15 ya hisa zitakazobaki.
“Aidha niko tayari kuleta mwekezaji mwingine mwenye uwezo wa kununua cash (kwa fedha taslimu) asilimia 15 hadi 20 wakati wowote ule ambao Simba na mwekezaji wa sasa watakapokuwa tayari kukaa mezani tufanye biashara.”
Hizi ni habari mpya kwa Simba, kumbe kuna watu wengi ambao wanaweza kununua sehemu ya asilimia 49 na kuwa wawekezaji, wakati inaonekana kama Dewji pekee ndio suluhisho la matatizo ya kiuchumi ya klabu.
Kigwangallah hatofautiani na maelekezo ya kikanuni ambayo klabu hiyo imepewa na ambazo ndizo zinaongoza umiliki wa taasisi za wananchi au wanachama.
Hata hivyo, Kigwangalla anakosea kidogo anaposema Simba na mwekezaji watakapokubali, kwa kuwa hadi sasa mwekezaji bado hajapatikana licha ya awali kumpa ushindi wa zabuni ya kununua hisa hizo kabla ya mamlaka za nchi kuzuia mchakato kukamilishwa kwa jinsi hiyo.
Haiwezekani mwekezaji wa sasa ashiriki katika maamuzi yanayohusu mabadiliko ya mfumo na muundo halafu baadaye awe mmoja wa wamiliki.
Na hili ni kosa ambalo hata Yanga wamelifanya la kutounda kamati ambayo ingesimamia mabadiliko hadi yakamilike badala ya kuuachia uongozi uliochaguliwa miaka minne iliyopita.
Dewji alitakiwa akae mbali, huku Mangungu akijishughulisha na uendeshaji klabu hadi mabadiliko yakamilike, zabuni itangazwe ya kutafuta wawekezaji na wale watakaoshinda waweke fedha zao na kukaa kando kuiachia Bodi ya Wakurugenzi iongoze Simba mpya na wao kupewa taarifa ya maendeleo wakati wa kikao cha wanahisa.
Kama ambavyo habari zinasema Dewji huwa anataka viongozi wasaini nyaraka anapotoa fedha kama mkopo, ndivyo inavyotakiwa ifanyike kwa wakati huu wa kuelekea mwishoni mwa mabadiliko.
Kigwangalla ni kati ya Wanasimba wachache wanaoweza kujitokeza kuelezea hisia zo kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya Simba.
Lakini inawezekana wako wengi ambao wanasita kujitokeza kutokana na klabu hizo kubwa kuendeshwa kwa mihemko, ikitumia wanachama wenye kelele kudhalilisha wale walio na mawazo tofauti.
Na matokeo ya uwanjani yanapokuwa mazuri, basi uongozi huona ndio mazingira mazuri ya kuendeleza uendeshaji usioakisi nia iliyokuwepo ya kuigeuza Simba kuendeshwa kisasa na kujitegemea kiuchumi.
Lakini Kigwangallah hajaishia kukosoa tu, bali ameonyesha njia ya kufika huko ambako Simba ilidhamiria kufika na jawabu la wawekezaji wengine walio tayari kuwekeza fedha wakati wowote.
Watu kama hawa ni muhimu kuwasikiliza na kufanyia kazi maoni yao, badala ya kuwatolea majibu mepesi kama hayo ya kuwa na hasira za kukosa mkopo wa pikipiki.
Ni lazima klabu kubwa kama Simba ikaachana na tabia ya kizamani ya kutumia makomandoo kuwafedhehesha watu wenye mawazo tofauti na badala yake wawavute karibu, kuwahoji kuhusu mawazo yao ili wachangie kile wanachoona kinafaa.