Sheria, kanuni zinavyokiukwa bima kwa wachezaji - 2
Muktasari:
- Kwa upande wake, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kupitia kanuni za leseni za klabu za mwaka 2022 kifungu cha 28, ibara ya 3, linazitaka klabu kuhakikisha wachezaji wanapata huduma kamili za matibabu, ikiwamo bima ya afya.
WAKATI wachezaji wa Ligi Kuu Bara wakiwa katika hatari za kiafya na kiuchumi kwa kutokuwa na bima za afya, uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini uwepo wa utekelezaji duni wa sheria.
Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara 2025 zilizotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Sura ya VI: Tiba na Bima, Kanuni ya 21 (Bima) inasema:
"Kila klabu ina wajibu wa kuwawekea wachezaji wake na maofisa wa benchi la ufundi bima ya matibabu na fidia kutokana na ajali michezoni. Klabu itakayokiuka kanuni hii itakuwa imepoteza sifa ya kuwa klabu ya Ligi Kuu na usajili wa wachezaji wa timu yake hautathibitishwa na haitashirikishwa katika Ligi Kuu."
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2023, kifungu cha 5, inaeleza kuwa bima ya afya ni lazima kwa kila mtu, huku waajiri wakitakiwa kuwachangia waajiriwa wao katika skimu za bima ya afya.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kupitia kanuni za leseni za klabu za mwaka 2022 kifungu cha 28, ibara ya 3, linazitaka klabu kuhakikisha wachezaji wanapata huduma kamili za matibabu, ikiwamo bima ya afya.
CAF pia inaweka wazi kuwa huduma hizo lazima zijumuishe uchunguzi wa afya wa kila mwaka na bima ya afya ya kina kwa wachezaji wote wenye mikataba.
Kwa kiwango cha kimataifa, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) halijaweka kanuni inayowalazimisha moja kwa moja klabu zote duniani kuwawekea wachezaji bima ya afya katika mazingira yote ya ushindani.
Hata hivyo, kupitia kanuni zake, FIFA imeweka wajibu mahsusi unaohusu wachezaji wanaoitwa kujiunga na timu za taifa, ikielekeza kuwa klabu ambayo mchezaji amesajiliwa inawajibika kuhakikisha mchezaji huyo analindwa na bima dhidi ya ugonjwa na ajali katika kipindi chote anapokuwa ameachiliwa kuitumikia timu ya taifa.
Vilevile, bima hiyo inapaswa pia kugharimia majeraha yoyote atakayopata akiwa kwenye mechi za kimataifa alizoitwa kushiriki.
Pia inaeleza endapo mchezaji wa kulipwa atapata jeraha la ajali akiwa kwenye mechi ya kimataifa ya timu ya taifa na kushindwa kucheza kwa muda, FIFA inaweza kuifidia klabu husika kwa mujibu wa masharti na utaratibu uliowekwa katika mpango a ulinzi wa klabu (FIFA Club Protection Programme).
Hata hivyo, fidia hiyo hailengi kuchukua nafasi ya wajibu wa klabu kuweka bima, bali ni utaratibu wa kuilinda dhidi ya hasara za kifedha zinazotokana na majeraha ya mchezaji akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa.
Kauli ya TFF
Kwa upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rais wake, Wallace Karia anasema sheria zipo wazi lakini baadhi ya klabu hazitekelezi kanuni ya uwepo wa bima ya afya.
Karia anasema katika msimu ujao wa 2026/27 hakuna timu itaruhusiwa kuanza bila kutimiza takwa hilo la kikanuni na kisheria.
Karia anasema: "Zipo klabu ambazo hazitii kanuni ya uwepo wa bima ya afya, lakini msimu ujao hakuna timu itaruhusiwa bila kutimiza takwa hilo."
Mkurugenzi wa Sheria na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, anasema shirikisho hilo limekuwa likizikumbusha klabu kuhakikisha zinatekeleza kanuni mbalimbali, ikiwamo bima ya afya. Hata hivyo, anakiri kuwa baadhi ya klabu bado zimekuwa nzito kutekeleza hilo.
Vilevile, anasema baadhi ya wachezaji na wasimamizi wao hawazingatii suala hilo wakati wa kuingia mikataba.
“Wachezaji wakiingia mikataba hawazingatii kulisimamia hili, wengine hawajui kabisa kwamba klabu zao zinatakiwa kuhakikisha hili linatekelezeka. Wakipata shida wakija huku ndipo wanatambua kuna haki zao wanazikosa,” anasema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha anasisitiza kuwa bima ni haki ya msingi kwa wachezaji wote na serikali inapaswa kuhakikisha sheria zinatekelezwa.
“Wachezaji wote, siyo wa mpira wa miguu pekee wanatakiwa kuwa na bima za afya, ni muhimu si tu kwa wao bali hata kwa familia zao,” anasema.
Kwa upande wake, Abeid Kasabalala, Katibu Msaidizi wa taasisi inayosimamia haki za wachezaji (Spata), anasema wao kama wasimamizi wa wachezaji na haki zao wamefanikisha uwepo wa kanuni.
“Shida ni kwamba, kila klabu huwa na uwezo wake. Wapo ambao wamiliki wa timu zao hawana kipato cha kukamilisha takwa hilo, lakini sisi kama viongozi huwa tunapigia kelele kila mara juu ya utekelezwaji wa sharia,” anasema na kuongeza:
“Kazi yetu ni kuwakumbusha kwani wanaoumia ni wachezaji ambao wanapambania timu hizo ili kufikia malengo yao, hivyo lazima walindwe na kupewa elimu ya umuhimu wa bima za afya.”