Sakata la Tambwe, TFF ijipange kukomesha uhuni huu
Muktasari:
Hilo ni moja tu kati ya matukio ya mshambuliaji huyo ambaye pia alikutwa na hatia ya kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic na kufungiwa mechi 10.
LUIS Suarez alipokuwa Liverpool alinaswa na kamera akitoa maneno ya kibaguzi dhidi ya beki wa zamani wa Manchester United, Patrice Evra.
Kwa tukio hilo, Suarez alifungiwa kuitumikia Liverpool kwa michezo minane.
Hilo ni moja tu kati ya matukio ya mshambuliaji huyo ambaye pia alikutwa na hatia ya kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic na kufungiwa mechi 10.
Kamera zilihusika kwa njia moja ama nyingine kubaini makosa ya mshambuliaji huyo mtukutu ambaye sasa amehamia Barcelona ya Hispania.
Mario Balotelli hivi karibuni aliandika maneno ya kibaguzi katika ukurasa wake wa Twitter akafungiwa mchezo mmoja na kupigwa faini.
Unaweza kujiuliza kwa nini FA imhukumu Balotelli kwa kosa la nje ya uwanja?
Ni kwa sababu hawataki kuiharibu bidhaa yao ya Ligi Kuu England ambayo inawaingizia kiasi kikubwa cha fedha kila msimu.
Kuna matukio mengi ya aina hiyo katika Ligi ya England ambayo yamewahusisha wachezaji, makocha na viongozi wa mbalimbali, FA imekuwa kali kwa kuchukua hatua kila kosa linapotokea.
Hivi karibuni katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kumekuwa na matukio yanayofanana na hayo au zaidi ya hayo.
Tukio la karibu ni la mchezaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe ambaye adaiwa kupata unyanyasaji mkubwa katika mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Ruvu Shooting.
Inadaiwa kuwa, Tambwe alibaguliwa na kuitwa mkimbizi na mabeki wa Ruvu Shooting, pia amepigwa viwiko, amekabwa na mabeki hao na kufanyiwa unyama mkubwa ambao mwingine si vizuri kuuandika hapa.
Kwa kauli yake, Tambwe anasema vitendo alivyofanyiwa na wachezaji wa Ruvu Shooting ni vya kinyama na anavilaani kwa nguvu zote.
Lakini pia beki wa Ruvu Shooting, George Michael Aidan naye anadai kuwa Tambwe alimng’ata kidoleni na kama haitoshi anadai mshambuliaji huyo alimwita (yeye George) Al- Shabaab.
Bado hizi ni tuhuma nzito ambazo zinaweza kuzidi kumshtua mpenzi yeyote wa soka.
Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi zinatakiwa kuzifanyia kazi na kuondoa dhana iliyojengeka kwa wengi kwamba soka ni mchezo wa kihuni.
Kama shirikisho hilo liliweza kumhukumu Athuman Idd ‘Chuji’ kwa kutumia picha ya gazeti hili, pale alipowaonyesha mashabiki wa Simba kidole cha kati, kwa nini leo hii inashindikana kwa kutumia picha za video?
Hata kwa kuyapa uzito matukio hayo, utagundua kuwa hili la mchezo wa Yanga na Ruvu Shooting lina nguvu zaidi kuliko lile la Chuji.
Kuna taarifa kwamba Azam TV inakabidhi mikanda au ‘CD’ mitatu ya kila mchezo wanaouonyesha kwa Bodi ya Ligi Kuu, hatua gani zimeshachukuliwa mpaka sasa kupitia mikanda hiyo.
Kwa kutumia mikanda hiyo, TFF na Bodi ya Ligi Kuu wangeweza kubaini kile kilichokuwa kikiendelea kati ya Tambwe na mabeki wa Ruvu Shooting. Pia kwa kuwatumia wataalamu wa alama za maneno wangeweza kubaini kile kilichokuwa kinazungumzwa na wachezaji hao na kuweza kuwachukulia hatua stahiki.
Mbali na tukio hilo, kuna matukio mengi ambayo TFF na Bodi ya Ligi wangeweza kuyatolea ufafanuzi kwa kuwahukumu waamuzi, wachezaji na hata viongozi wanaovurunda katika Ligi Kuu.
Leo hii mchezaji wa Ligi Kuu anaweza kumpiga simu mwandishi wa habari na kumtukana na asichukuliwe hatua yoyote hata kama amerekodiwa na ushahidi wa kutosha upo.
Mchezaji anaweza kupigana nje ya uwanja na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu lakini TFF isimchukulie hatua za msingi.
Kwa kuachiwa kwa matukio hayo ndiyo maana mengine yanaendelea kutokea na kufanya mchezo wa soka kuwa vita na siyo sehemu ya kuonyeshana ufundi na kutoa burudani kwa watazamaji.
Kwa kutochukua hatua, TFF inaharibu ‘brand’ yake na kuifanya kuonekana kuwa ya ovyo. Ndiyo maana kuna wakati inashindwa kuiuza Ligi Kuu na kuwa na wadhamini wa uhakika tofauti hali ilivyo katika nchi nyingine.
Tuiondoe Ligi Kuu kule ilikokuwa zamani na tuipeleke kisasa, nakumbuka wakati Ligi Kuu ilipokuwa ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza kulikuwa timu zilizosifika kwa kupiga viatu mfano, Nyota Nyekundu, Plisner na Sigara.
Kuna wachezaji waliokuwa wakipewa majina kutokana na uchezaji wao wa kibabe kama vile Salum Kabunda ‘Ninja’ kutokana na uwezo wake wa kucheza rafu.
Mabeki wengi wa JKT Ruvu ni wachezaji wazuri ambao wanaweza kuitumikia Taifa Stars, kwa kukumbwa na tuhuma hizi za Tambwe je, hivi ndivyo wanavyoweza kufanya katika kuliwakilisha taifa lao katika michuano ya kimataifa?
Kuna timu au wachezaji ambao bado wana mtazamo wa kizamani. Itakuwa vizuri kama TFF na Bodi ya Ligi zitautumia mchezo wa Yanga na Ruvu Shooting kuwa kielelezo cha uchunguzi wa vitendo vya kihuni na kuwahukumu wote watakaokutwa na hatia.
Naamini kama TFF ikiamua kulifanya hili inawezekana kwani kila kitu kipo katika mikono yao.