Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NGOZI: Kuolewa, kuzaa sio mwisho wa ndoto kucheza

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mmoja wa nyota waliowahi kutawala bara hilo, Ngozi Okobi Okeoghene ameibua mijadala mbalimbali kuhusu nafasi ya wanasoka wa kike baada ya kuolewa na kupata watoto.

WAKATI fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake zikiendelea nchini Morocco kuna simulizi za mastaa mbalimbali ambazo zimekuwa zikivutia wafuatiliaji wa soka la wanawake Afrika.

Mmoja wa nyota waliowahi kutawala bara hilo, Ngozi Okobi Okeoghene ameibua mijadala mbalimbali kuhusu nafasi ya wanasoka wa kike baada ya kuolewa na kupata watoto.

Okeoghene alifunga ndoa na mfanyabiashara wa masuala ya nyumba na ardhi Ahmed Okeoghene Desemba 9, 2017 katika Jimbo la Delta, Nigeria, ndoa ambayo wengi waliamini ingempoteza mwana soka huyo kwenye karia yake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mwaka 2024 wakati Nigeria inabeba taji lake la 10 la michuano ya WAFCON, Ngozi hakuwa sehemu ya kikosi hicho kwani wakati huo alibarikiwa kupata mtoto wake wa kwanza wa kiume.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 alijikuta akikosolewa na baadhi ya mashabiki waliodhani kuwa baada ya kuwa mama uwezo wake wa kucheza soka ungekuwa umepungua.

Kwenye moja ya mahojiano na chombo kimoja cha habari anasema: “Nigeria, mashabiki wengi wanaamini mwanamke anapoolewa anakuwa mzee. Mwanamke akijifungua wanaona hana tena nguvu ya kufanya kile alichokuwa akifanya.”

Kauli hiyo imefungua mjadala mkubwa kuhusu changamoto zinazowakabili wachezaji wanawake Afrika, ambao mara nyingi hukutana na shinikizo la kuchagua kati ya maisha ya familia na ndoto zao.

Kwa Okobi-Okeoghene, tatizo hilo limekuwa kubwa kiasi cha kuathiri hata maamuzi ya wachezaji wengine.

“Wanatufanya tujisikie vibaya kuhusu sisi wenyewe. Wasichana wengi wanaogopa kuolewa kwa sababu wanafikiri wakiolewa hawataitwa tena kwenye timu ya taifa,” anasema.

Lakini nyota huyo mwenye mataji manne ya WAFCON akiwa na Nigeria amesisitiza kuwa kuwa mke au mama hakumaanishi mwisho wa maisha ya mchezaji.

“Kuwa mchezaji wa soka hakunizuii kuwa mke. Hakunizuii kuwa mwanamke mwenye kazi na mwanamichezo. Uzazi haupaswi kuwa mwisho wa hadithi ya mtu yeyote,” anasema.

Okeoghene anasema wanawake hawapaswi kulazimishwa kuchagua kati ya familia na soka kwani kila kitu kina nafasi yake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Nyota huyo anayeitumikia Ottawa Rapid FC ya Ligi Kuu ya Wanawake Canada, kabla ya ligi hiyo aliwahi kukipiga Levante Badalona ya Hispania, Washington Spirit ya Marekani na klabu mbalimbali duniani.

Okeoghene ambaye amejumuishwa kwa mara nyingine tena kwenye kikosi cha Super Falcons kinachowania nafasi ya kutetea taji lake, ni moja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa katika historia ya Nigeria akiisaidia nchi yake kutwaa mataji manne ya WAFCON (2010, 2014, 2016 na 2018) na kucheza katika Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA.

Alirejea uwanjani mwishoni mwa mwaka 2024 na  Januari mwaka 2025 alisaini mkataba na Ottawa Rapid FC unaotamatika mwishoni mwa mwaka 2026.


SAFARI YA KUREJEA

Baada ya kujifungua mtoto wake, Okeoghene alikabiliwa na changamoto ya kurejesha kiwango chake cha kimwili ili kurudi kwenye ushindani.

Alianza mazoezi miezi mitano baada ya kupata mtoto, lakini alikiri haikuwa safari rahisi.

“Mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ilikuwa ngumu na ilinichukua muda mrefu kujirudisha. Wenzangu walinisaidia sana hasa kipindi cha mwanzo,” anasema.

Kwa mujibu wa mchezaji huyo, uzazi haukuondoa uwezo wake wa kucheza soka bali ulihitaji muda kurejesha nguvu na kiwango cha utimamu wa mwili.

Okeoghene alirejea kwenye programu ya timu ya taifa ya Nigeria chini ya kocha Justin Madugu kwa michezo ya kirafiki dhidi ya Cameroon, Senegal na maandalizi ya WAFCON.

“Ninapenda kuiwakilisha nchi yangu wakati wowote. Hii ni timu yangu, mimi si mtu wa nje hivyo nitapambana kwa ajili ya nchi hii,” anasema.


AFRIKA INA SAFARI NDEFU

Kauli ya Okeoghene imekuja wakati ambapo soka la wanawake duniani linaendelea kuweka mifumo ya kuwalinda wachezaji wanapopata ujauzito.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeweka kanuni zinazohakikisha wachezaji wanawake wanapata mapumziko ya uzazi yenye malipo na kulindwa dhidi ya ubaguzi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Katika Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa FIFA (FIFA Regulations on the Status and Transfer of Players - RSTP), Ibara ya 18(7) na Ibara ya 18quater kinamlinda mchezaji wa kike haadhibiwi kwa sababu ya kupata ujauzito na kwamba anaweza kuendelea na taaluma yake ya soka bila kupoteza haki zake za ajira.

Inaeleza kuwa mkataba wa mchezaji wa kike hauwezi kusitishwa kwa sababu ya ujauzito. Ikiwa klabu itavunja mkataba kwa sababu hiyo, FIFA inachukulia kitendo hicho kuwa ni kuvunja mkataba bila sababu, hivyo klabu inaweza kuwajibishwa kwa kulipa fidia na pia inaweza kupewa adhabu za kinidhamu.

Hata hivyo, changamoto bado ipo katika mataifa mengi ya Afrika ambako ligi za wanawake hazijafikia kiwango cha kitaalamu kinachoweza kuhakikisha haki hizo zinatekelezwa kikamilifu.

Okeoghene alitoa mfano wa uzoefu wake alipokuwa akicheza Sweden, ambako alimwona mchezaji mwenzake akiendelea na mpango wa mazoezi wakati wa ujauzito na kurejea akiwa na nguvu zaidi baada ya kujifungua.

Kwa mtazamo wake, tofauti kubwa ipo kwenye mfumo na namna jamii inavyowaangalia wanawake wanapokuwa na familia.


ANATAMANI MTOTO

Mbali na changamoto hizo, Okeoghene amesema familia yake imekuwa nguzo kubwa katika kurejea kwake.

Alisema mume wake hakutaka aache soka kwa sababu tu amepata mtoto, bali alimpa msaada na sapoti ili aendelee kufuatilia ndoto zake.

“Kuna wakati nachoka sana baada ya mazoezi, lakini yeye yupo kunisaidia. Anataka nifanye kile ninachokipenda,” anasema.

Kwa sasa mtoto wake amekuwa chanzo cha motisha kwake.

“Kila siku ninapomuona mwanangu inanipa nguvu ya kufanya zaidi. Nataka aone nikicheza mpira tayari anakimbia na mpira, hivyo anahitaji kujifunza kutoka kwangu,” anasema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wakati Nigeria ikianza harakati za kutetea taji lake la WAFCON na kutafuta ubingwa wa 11, ujumbe wa Okeoghene umebeba maana kubwa zaidi ya soka.

Ni ujumbe unaolenga kubadili fikra kwamba mwanamke akianzisha familia basi ndoto zake zinaishia hapo.

Kwa nyota huyo wa Super Falcons, mwanamke anaweza kuwa mama, mke na bado akaendelea kuwa mwanamichezo bora.