Prime
Kanuni za 'Kichina' za TFF zinavyotishia uhai wa klabu zetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kanuni mpya zinazolenga kudhibiti vitendo visivyokubalika katika mchezo huo, pamoja na kuweka utaratibu wa usajili wa wachezaji wa kigeni ili kupata wenye ubora zaidi.
Kuanzia msimu ujao, timu itakayogomea kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo itapokonywa pointi tano, wakati mchezaji wa kigeni atakayesajiliwa na klabu za ndani atalazimika kuwa ni yule aliyewahi kuitwa kwenye timu za taifa za nchi yake kuanzia ngazi za vijana.
Hizo ni baadhi ya kanuni mpya zitakazoanza kutumika katika msimu wa 2026/27. Lengo ni zuri, lakini halijafanyiwa uchunguzi wa kina wala kujadiliwa kwa mapana na wadau kabla ya kupitishwa, hali inayoweza kusababisha ugumu katika utekelezaji wake.
Tatizo hilo la kutokuwapo kwa ushirikishwaji linazidi kuwa kubwa kwa sababu walio katika mamlaka wanaona kana kwamba hakuna haja ya kuwashirikisha wadau wengine, ama kwa kudhani hawaelewi mpira kuliko walio madarakani au kwa kuamini uongozi ni kutumia mamlaka uliyonayo pekee.
Kwanza kabisa, masuala hayo yalitakiwa yaanzie kwa klabu zenyewe zinazoshiriki Ligi Kuu na Championship, kama kanuni za uongozi (governing regulations) zilizoanzisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPBL) zinavyoelekeza. Kanuni zinaeleza wazi kuwa mabadiliko au utunzi wa kanuni mpya unapaswa kufanywa na Bodi ya Ligi, halafu Kamati ya Utendaji ya TFF ndiyo iyapitisha.
Aidha, Bodi ya Ligi hufanya maamuzi yake kwa kupeleka mapendekezo katika Mkutano Mkuu wa Bodi kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa. Si kwamba TFF ndiyo inapaswa kubuni, kuunda na kupitisha kanuni.
TFF inatakiwa ibakie katika majukumu yake ya msingi ya kuendeleza soka na si kuendesha mashindano ya wachezaji ambao tayari wamehitimu kutoka timu za vijana (ready-made au complete footballers), kwa kuwa hao tayari wamevuka hatua ya maendeleo.
Kwa mfano, suala la kuwataka wachezaji wa kigeni wawe ni wale waliowahi kuitwa kuanzia timu za taifa za vijana hadi timu za wakubwa linawezaje kusaidia maendeleo ya soka la Tanzania? Kanuni hiyo inaweza tu kuongeza ushindani katika Ligi Kuu na Championship, lakini isiwe na manufaa ya moja kwa moja kwa soka la Tanzania, hususan timu za taifa.
Isitoshe, kuchezea timu ya taifa hakumaanishi kwamba mchezaji ana kiwango bora zaidi. Mfano ni Karim Benzema, ambaye kwa muda mrefu hakuitwa na Didier Deschamps licha ya kuwa na kiwango cha juu akiwa Real Madrid.
Kuna nyakati kocha wa timu ya taifa havutiwi na aina ya uchezaji wa mchezaji fulani. Endapo kocha huyo atakuwa na mkataba wa muda mrefu, ni nadra sana kwa mchezaji huyo kupata nafasi ya kuichezea nchi yake. Na kama hakuwahi kuitwa katika timu za vijana, basi nafasi hiyo huwa ndogo zaidi.
Kila wakati kuna kundi fulani la wachezaji wanaoitwa timu za taifa. Angalia wachezaji wazawa wanaocheza Ligi Kuu ya Bara na uhesabu ni wangapi waliowahi kuchezea timu za taifa za vijana, lakini sasa hawapo Taifa Stars. Ni wengi sana.
Kwa hiyo, kanuni hiyo ilistahili kubakia kama ilivyokuwa awali, kwamba mchezaji wa kigeni anayesajiliwa Tanzania awe amecheza ligi ya nchi anayotoka. Nina uhakika jambo hilo lingejadiliwa katika Mkutano Mkuu wa klabu, lisingepita kirahisi na lingeweza kurudishwa kwa waliolitunga ili lifanyiwe maboresho.
Nimeeleza hayo yote ili kuonyesha kuwa mgawanyo wa majukumu uliokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi ni lazima uheshimiwe.
Wenye ligi ndiyo wanapaswa kubuni, kutunga na kupitisha kanuni zitakazowaongoza. Kwa kuwa TFF ndiyo msimamizi wa mpira wa miguu nchini, jukumu lake ni kuangalia kama kanuni hizo zinakinzana na sheria za nchi, sheria za mchezo au maendeleo ya mchezo wenyewe.
Lengo la kuunda Bodi ya Ligi lilikuwa ni kuzifanya klabu zijisimamie na kujidhibiti katika masuala ya haki, kwa kuwa ni rahisi zaidi kuondoa upendeleo au uwezekano wa ofisa kutumiwa na klabu moja dhidi ya nyingine.
TFF ibakie katika jukumu lake la kuendeleza mchezo kwa kujikita katika mafunzo ya makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na viongozi, pamoja na kusimamia timu zote za taifa na maendeleo ya soka la wanawake.
Unapoona kanuni za ajabu kama ya kuikata timu pointi tano, unatambua wazi kuwa zimetengenezwa na watu wasio na uchungu na klabu, wanaoona ni jambo la kawaida kuadhibu timu kwa kuipokonya pointi tano kwa kosa ambalo halijatokea ndani ya dakika 90 za mchezo.
Nina uhakika kama suala hilo lingepelekwa katika Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi, hakuna klabu ambayo ingeikubali. Badala yake, wangejadili namna ya kumwajibisha kiongozi anayekwenda na timu uwanjani, hususan kocha ambaye ndiye meneja wa timu na ndiye anayewajibika moja kwa moja iwapo wachezaji wataathirika na dawa zilizopulizwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo au kuathirika kisaikolojia kutokana na vitendo vya ushirikina.
Klabu zingeweza hata kupendekeza kuwepo kwa ulinzi maalumu wa vyumba vya kubadilishia nguo kwa kuweka askari wa kuvihifadhi kuanzia siku moja kabla ya mchezo hadi wakati timu zinaingia uwanjani. Ninachotaka kusema ni kwamba kama klabu ndizo zingekuwa zinatungua kanuni, zingeweza pia kupata suluhisho halisi la changamoto zinazozikabili.
Pengine baadhi ya wadau wamesema sana kuhusu udhaifu wa Bodi ya Ligi. Huu ni wakati wa klabu kuamka na kutambua kuwa Ligi Kuu ni yao. Hazipaswi kusubiri kutungiwa kanuni na chombo kingine badala ya Mkutano Mkuu wao, baada ya kuzijadili kwa kina na kuwashirikisha wadau mbalimbali, badala ya mtindo wa watu wachache kujifungia na kuibuka asubuhi na kanuni mpya.