Okwi ni mtumbuizaji mzuri hajasubiri aibu
Muktasari:
- Pengine amejifunza kwa baadhi ya nyota waliowahi kufanya vizuri lakini mwisho wao ukawa mbaya baada ya kulazimisha kucheza huku umri ukiwa umewakataa.
KUNA usemi maarufu ambao tunaweza kuutumia kumuelezea Emmanuel Okwi baada ya nyota huyo wa Uganda kuamua kustaafu rasmi soka la kulipwa.
Nao ni “mtumbuizaji mzuri anafahamu muda gani sahihi wa kushuka jukwaani.”
Katika umri wa miaka 33, Okwi ameamua kushuka kutoka katika jukwaa la soka la kulipwa na sasa anavining’iniza ukutani viatu vyake na anageuka kuwa mtazamaji kama sisi tu ambao tulikuwa tunamtazama yeye.
Wengi wanaweza kushangaa kwa nini Okwi ameamua kustaafu soka la ushindani akiwa na umri wa miaka 33 tu ambayo huwa haionekani kuwa kikwazo kwa wachezaji wengi hadi ikawaachanisha na soka lakini kwa mshambuliaji huyo wa Uganda kijiwe kinaamini amefanya jambo sahihi.
Okwi alianza kucheza soka la ushindani mapema sana. Katika umri wa miaka 16 tu tayari alishakuwa mchezaji tegemeo wa Sports Club Villa pale Uganda na akiwa na miaka 18 tu akaja Bongo kuitumikia Simba.
Licha ya kuanza kutumika mapema, Okwi ni mchezaji ambaye katika klabu zote alizowahi kuzichezea hakuwa mkaa benchi bali alipata nafasi ya kucheza kikosini huku nyingi zikimfanya awe tegemeo.
Na kwa staili ya uchezaji wake, Okwi alikuwa ni mchezaji ambaye alilazimika kukimbia kilomita nyingi uwanjani kwa vile mara nyingi hushambulia kutokea pembeni hivyo alitumia nishati nyingi.
Inawezekana angeweza kucheza kwa miaka miwili au mitatu mbele lakini yeye ndio anaufahamu zaidi mwili wake hivyo ameona bora aamue kujiweka kando hivi sasa badala ya kusubiri kustaafu kwa aibu.
Pengine amejifunza kwa baadhi ya nyota waliowahi kufanya vizuri lakini mwisho wao ukawa mbaya baada ya kulazimisha kucheza huku umri ukiwa umewakataa.