Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu nne za kuiaga mapema KMC Ligi Kuu

Muktasari:

  • Lile shangwe la msimu wa 2018-2019 kushiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya nne iliyofanya 2019-2020 kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, sasa imegeuka. Kuna huzuni viunga vya Kinondoni.

WASWAHILI wanasema 'Maji yakimwagika hayazoleki.' KMC inachofanya hivi sasa ni kujaribu kuyazoa maji iliyomwaga mapema jambo ambalo linawawia vigumu kupambana nalo.

Timu hiyo yenye maskani yake Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiutumia Uwanja wa KMC Complex kwa mechi zake za nyumbani, imebakiwa na mechi 14 pekee za kujitetea isishuke daraja msimu huu.

Mechi hizo 14 zina pointi 42, yaani ni mara tano ya zile ilizo nazo sasa baada ya kucheza mechi 16.

Mtihani mkubwa ilionao KMC ni kuhakikisha haiangushi pointi katika msako huo ili kuwa salama zaidi, vinginevyo itarudi Ligi ya Championship ilipotoka misimu saba nyuma.

Vijana hao wa Kinondoni, walipanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2018-2019, tangu hapo imekuwa na mwendo wa kupanda nafasi ndani ya ligi na kushuka, lakini inaendelea kusalia katika ligi hiyo.

Lile shangwe la msimu wa 2018-2019 kushiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya nne iliyofanya 2019-2020 kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, sasa imegeuka. Kuna huzuni viunga vya Kinondoni.

KMC ilikuwa vizuri zaidi katika msimu wa kwanza ambapo nafasi ya nne iliyomaliza, imekuwa ndoto kwao hadi sasa ambapo inacheza katika nafasi za mbali sana, Msimu wa 2019-2020, 2022-2023 na 2024-2025 ilikuwa ya 13, huku 2021-2022 ikikamata nafasi ya 10. Kidogo 2023-2024 ilipanda hadi nafasi ya tano. Msimu uliopita 2024-2025, ikamaliza ya kumi.

Safari hii, maji marefu. Zimebaki mechi 14, ina hatua chache zaidi za kushuka daraja kuliko zile za kubaki na hapa kuna sababu tatu za timu hiyo kuiaga mapema.

Kabla hatujaenda mbali, Kanuni ya 6(2) ya Ligi Kuu Bara inaeleza kuwa: "Timu mbili (2) za mwisho, zilizoshika nafasi ya 15 na 16 kwenye Ligi Kuu zitashuka moja kwa moja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (Championship) msimu unaofuata."

Kwa sasa timu mojawapo kati ya hizo ni KMC iliyopo nafasi ya 16 na pointi nane, juu yake kuna Tanzania Prisons iliyokusanya pointi 13.


USHAMBULIAJI, ULINZI BUTU

Katika timu yoyote, ili ipate ushindi lazima ifunge mabao, lakini pia ili kuzuia isipoteze, basi ilinde vizuri nyavu zake. Kwa KMC hayo yote yana changamoto.

Ukiangalia orodha ya timu zenye mabao machache zaidi katika Ligi Kuu Bara msimu huu, KMC inashika nafasi ya kwanza ikifunga matano.

Lakini pia katika orodha ya timu zilizoruhusu mabao mengi zaidi, KMC inaongoza kwa nyavu zake kutikiswa mara 25. Takwimu zote hizo muhimu zinawakataa.

Mbaya zaidi, KMC ni kinara wa kujifunga ikifanya hivyo mara tatu, lakini pia ina nyota watatu pekee waliofunga katika ligi msimu huu, Daruesh Saliboko mwenye mabao matatu, Rashid Chambo (1) na Jammy Simba (1). Kwa timu inayosaka mafanikio, hii haipo sawa.


WASTANI WA POINTI

Msimu uliopita, KenGold iliyoshuka daraja kwa kushika nafasi ya mwisho ikimaliza ligi na pointi 16, kipindi kama hiki ilikuwa na pointi sita pekee baada ya kucheza mechi 16 ikishinda moja na sare tatu. Mzunguko wa pili ikakusanya pointi kumi, habari yao ikaishia hapo.

KMC hivi sasa ina pointi nane baada ya mechi 16 ikishinda mbili sawa na sare, huku ikipoteza 12. Kwa wastani ina uwezo wa kukusanya pointi mbili kila mechi.

Kwa hesabu za haraka, KMC katika mechi 14 zilizobaki, inaweza kukusanya pointi saba kama itaendelea na mwendo huo. Kwa maana hiyo, jumla itakuwa nazo 15 katika mechi 30 za msimu huu.

Rekodi zinaonesha, katika Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2021-2022 ambapo timu 16 zimekuwa zikishiriki ligi hiyo, timu iliyomaliza na pointi 32 kushuka chini lazima iwe katika mstari wa kushuka daraja.

Hapo kuna mawili, ishuke moja kwa moja, au ipambane kubaki kupitia mechi za mtoano (playoff). Hali hiyo imeshawahi kuikuta KMC katika msimu wa 2022-2023 ambapo ilikwenda kucheza mtoano na Mbeya City, ikabaki ligi kuu wakati Mbeya City ikashuka kufuatia kukutana na kipigo kingine kutoka kwa Mashujaa iliyokuwa Championship.


UKAME WA USHINDI

Kucheza mechi 16, halafu ukashinda mbili pekee, hiyo ni dalili mbaya kwenye timu. KMC ipo katika hali hiyo kufuatia kushinda mechi ya kwanza ya msimu kwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa Septemba 17, 2025, kisha ikaichapa Mashujaa bao 1-0, Februari 3, 2026.

Kutoka Septemba 17, 2025 hadi Februari 3, 2026, zimepita siku 139 ndipo KMC imepata ushindi wa pili. Kumbuka hapo kati kulikuwa na vipigo sita mfululizo tangu itoke kushinda mechi ya kwanza, ikajipoza na sare moja, ikaja kupigwa tena mbili mfululizo.

Timu hiyo imefundishwa na makocha wawili, alianza Marcio Maximo, akashinda mechi moja pekee, ushindi mwingine ameupata Abdallah Mohamed 'Baresi' ambaye yupo sasa.


MSIKIE KOCHA BARESI

Kwa sasa KMC ipo chimbo ikitengeneza silaha zake za kuja kufanya mapinduzi kwani haina mechi yoyote ya mashindano hadi Aprili 3, 2026 itakapoifuata Mbeya City. Mara ya mwisho KMC kucheza mechi ya mashindano ilikuwa Februari 22, 2026 ikafungwa nyumbani mabao 2-0 na Azam katika ligi, kabla ya hapo, Februari 19, 2026 iliondoshwa hatua ya 64 bora na Bandari Tanzania katika Kombe la FA.

Ikiwa na muda mwingi wa kujiandaa, Kocha wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, amesema mechi tano zijazo za Ligi Kuu Bara kwa kikosi hicho zitakuwa za uamuzi mgumu wa kuamua hatima yao.

Baresi amesema kutokuwa na mechi yoyote kwa mwezi huu ni jambo nzuri kwa sababu wana muda mzuri wa kufanyia kazi makosa mbalimbali yaliyojitokeza, huku wakiboresha maeneo ya kujilinda na ushambuliaji.

“Kadri unavyozidi kupoteza ndivyo ambavyo pia morali ya wachezaji inapungua, tuna muda mzuri wa kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika mechi zetu zilizopita, ili turudi imara na kutoka sehemu tuliyopo,” amesema Baresi.

Katika mechi hizo tano zijazo za KMC, itacheza dhidi ya Mbeya City (Aprili 3, 2026, ugenini), Singida Black Stars (Aprili 8, 2026, ugenini), Tanzania Prisons (Aprili 14, 2026, nyumbani), Yanga (Aprili 19, 2026, nyumbani) na Fountain Gate (Aprili 28, 2026, nyumbani).

Rekodi za KMC misimu nane

2025-2026

Mechi: 16

Pointi: 8

Nafasi: 16 (ligi inaendelea)


2024-2025

Mechi: 30

Pointi: 35

Nafasi: 10


2023-2024

Mechi: 30

Pointi: 37

Nafasi: 5


2022-2023

Mechi: 30

Pointi: 32

Nafasi: 13 (ilicheza mtoano)


2021-2022

Mechi: 30

Pointi: 35

Nafasi: 10


2020-2021

Mechi: 34

Pointi: 48

Nafasi: 5


2019-2020

Mechi: 38

Pointi: 46

Nafasi: 13


2018-2019

Mechi: 38

Pointi: 55

Nafasi: 4 (ilishiriki Caf)