Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rui Pinto: Mwamba nyuma ya sakata la Man City huyu hapa

PINTO Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo kwa sasa inasubiri hukumu ambayo inaweza kuwa mbaya katika soka duniani ikiwamo kushushwa daraja au madaraja, kupigwa faini kubwa au kupokonywa pointi katika ligi inayoendelea sasa.

LONDON, ENGLAND: UAMUZI  wa tume huru ya Ligi Kuu England iliyoikuta Manchester City na makosa ya kukiuka kanuni 114 kati ya 115 za kifedha za ligi mashindano hayo umefungua ukurasa mpya wa moja ya sakata kubwa zaidi kuwahi kuikumba klabu hiyo.

Timu hiyo kwa sasa inasubiri hukumu ambayo inaweza kuwa mbaya katika soka duniani ikiwamo kushushwa daraja au madaraja, kupigwa faini kubwa au kupokonywa pointi katika ligi inayoendelea sasa.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Manchester City, Khaldoon Al Mubarak, amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya taarifa kwamba klabu imekutwa na hatia akisema: “Wakati baadhi ya watu wamekuwa wepesi kufikia hitimisho lao wenyewe, na huku kukiwa na kelele nyingi zinazotuzunguka, hakuna kilichobadilika. Tumewahi kukabiliana na changamoto pamoja na kuzishinda. Bado kuna watu wengi wanaotaka kudhoofisha kasi ya maendeleo ya klabu yetu. Hatutawapa fursa hiyo. Tuna nyakati kadhaa za kusisimua tunazozitarajia baada ya mapumziko haya ya kimataifa.”

Lakini, nyuma ya sakata linaloihusu klabu hiyo kuna jina lililowahi kuonekana mbali kabla ya kesi hiyo kufikia hatua hii; Rui Pinto, mtu aliyekuwa chanzo cha mamilioni ya nyaraka zilizovuja kupitia tovuti yake ya Football Leaks, ambapo kwa miaka mingi amekuwa mwenye sura mbili; kwa baadhi ya watu ni mhalifu aliyepata taarifa kwa njia zisizo halali ilhali wengine wanamuona kama mtoa taarifa aliyefichua mambo ambayo umma ulikuwa na haki ya kuyajua. Sasa, baada ya Manchester City kupatikana na hatia katika karibu mashtaka yote iliyokuwa ikikabiliwa, jina lake limerudi tena kwenye mjadala wa soka la dunia.


PINT 01

NYARAKA ZILIZOTIKISA SOKA

Athari ya Pinto kwa Manchester City ilianza miaka kadhaa iliyopita, baada ya nyaraka na barua pepe alizopata na kuwapa waandishi wa habari wa vyombo tofauti zilizoibua uchunguzi wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na Chama cha Soka England (FA) kuhusu City, uchunguzi ulioifanya  klabu hiyo kufungiwa kushiriki michuano ya Ulaya kwa miaka miwili. Hata hivyo, City ilikata rufaa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ikabatilisha uamuzi huo mwaka 2020.

Hata hivyo hilo halikufunga mjadala, kwani wiki iliyopita ilikuwa na hatia katika makosa 114 ya kanuni za kifedha za Ligi Kuu England. City imepanga kukata rufaa na adhabu bado haijawekwa wazi.

Kwa Pinto, hata hivyo, uamuzi huo ulikuwa uthibitisho wa umuhimu wa kazi aliyoifanya miaka iliyopita. Baada ya habari hiyo, aliandika kwenye X kwamba ulikuwa “uamuzi wa kihistoria kwa soka la England”, akidai kwamba ulikamilisha kazi aliyokuwa ameifanya kupitia Football Leaks.

Pinto, mwenye umri wa miaka 37, alikulia Vila Nova de Gaia, karibu na Porto nchini Ureno na kwa wengi waliomfahamu uwezo wake mkubwa wa kujifunza mwenyewe na kuchambua taarifa tata kilikuwa kipaumbele katika maisha yake.

PINT 02

Mwaka 2015, Pinto alihamia Budapest, Hungary, ambako alikuwa akifanya biashara ya vitu vya zamani na ni huko ndipo alianza kuchapisha taarifa kwenye blogu akitumia jina la bandia “John” akidai kwamba alikuwa akipewa na watu wa ndani ya soka waliokuwa wamekasirika.

Mambo yalibadilika haraka, kwani kufikia mwishoni mwa 2018 alikuwa amelipatia nyaraka jarida la Ujerumani la Der Spiegel na washirika wake zilizofikia milioni 70. Huo ukawa mwanzo wa mfululizo wa ufichuzi uliobadili namna umma ulivyotazama biashara ya soka.


PINT 04

SIRI ZILIZOFICHULIWA

Mtandao wake Football Leaks ulihusu kila kitu kuanzia mikataba ya wachezaji hadi kodi, uhamisho na kanuni za kifedha za klabu. Baadhi ya taarifa zilikuwa na vipengele vya kushangaza katika mikataba ya wachezaji. Kulikuwa na madai kwamba Real Betis ilikuwa na kipengele kilichomzuia Rafael van der Vaart kuvaa viatu vyekundu.

Liverpool nayo ilidaiwa kuwa na kipengele kilichomruhusu Roberto Firmino kuuzwa kwa Pauni 98 milioni, lakini siyo kwa Arsenal na kulikuwa pia na taarifa kuhusu madai ya Real Madrid kupunguza hadharani ukubwa wa ada iliyolipwa kwa Tottenham Hotspur kumnunua Gareth Bale.

Lakini, nyuma ya taarifa hizo za kuvutia kulikuwa na uchunguzi mzito zaidi. Football Leaks ilifichua taarifa kuhusu masuala ya kodi yaliyowahusu Cristiano Ronaldo, Jose Mourinho na Mesut Ozil, mipango ya European Super League (iliyokuja kufa kabla haijaanza), mizania sahihi ya matumizi ya fedha (financial fair play -FFP) ya Manchester City na PSG, pamoja na madai ya ubakaji yaliyomhusu Ronaldo.

PINT 07

Hata hivyo, siyo madai yote yaliyothibitishwa. Bayern Munich ilikanusha kuhusika katika mipango ya European Super League, UEFA ikaachana na kesi yake dhidi ya PSG, huku Ronaldo akikanusha madai ya ubakaji na kutowahi kushtakiwa na polisi.

Kadiri taarifa zilivyozidi kutoka, Pinto mwenyewe alianza kukabiliwa na matatizo ya kisheria na mojawapo wa maeneo yaliyokuwa na utata mkubwa ilikuwa Benfica, klabu kubwa zaidi nchini Ureno. Mwaka 2017, barua pepe zilizovuja zilionekana kuibua madai ya vitendo vya rushwa ndani ya klabu hiyo. Benfica ilikanusha madai hayo na imeendelea kusema kwamba hayakuwa na msingi.

Pinto naye amewahi kukataa kuwa ndiye aliyekuwa nyuma ya baadhi ya taarifa hizo. Hata hivyo, kesi yake ya kwanza iliendelea hadi mahakamani. Mchakato huo ulidumu miaka mitatu na ulikuwa na mvutano mkubwa kiasi kwamba Pinto alifika mahakamani akiwa amevaa jaketi la kuzuia risasi.

PINT 03

Mwaka 2023, mahakama ya Lisbon ilimkuta na hatia katika makosa tisa; matano ya kuingia kinyume cha sheria katika mifumo ya TEHAMA, matatu ya kuchapisha mawasiliano binafsi na moja la kujaribu kuilaghai Doyen Sports Investments (mfuko wa uwekezaji binafsi uliokuwa na makao yake Malta, ambao ulifadhili usajili wa wachezaji na kusimamia mwelekeo wa taaluma za wanasoka kupitia mifumo ya kifedha).

Katika hukumu alihukumiwa kifungo cha miaka minne, lakini kilichosimamishwa.

Jaji Margarida Alves alisema mahakama iliona wazi kwamba Pinto alikuwa akitarajia kupata fedha katika jaribio hilo. Pia alikataa hoja kwamba shughuli za Pinto zinaweza kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa taarifa, akisema uhuru huo hauondoi haki ya watu wengine ya kulindwa faragha zao.


PINT 05

KWA NINI BADO ANA WAFUASI?

Pamoja na hukumu hiyo, Pinto aliendelea kuwa na wafuasi waliomuona kama mdukuzi aliyekuwa akiwawajibisha watu wenye nguvu.

Miongoni mwa waliomtetea alikuwa Ana Gomes, aliyekuwa mwanachama wa Bunge la Ulaya kutoka Ureno aliyedai Pinto alikuwa amefichua mambo kuhusu klabu kubwa za Ureno na kwamba mchango wake kwa umma ulipaswa kuzingatiwa.

Mawakili wake nao walimuita “mtoa taarifa mkuu wa Ulaya”. Mtazamo huo ulipata nguvu zaidi baada ya Pinto kuhusishwa na Luanda Leaks, uchunguzi uliohusisha nyaraka kuhusu shughuli za kifedha za bilionea wa Angola, Isabel dos Santos.

Isabela alishakanusha kufanya kosa lolote. Kwa wafuasi wa Pinto, Luanda Leaks ilionyesha kwamba shughuli zake hazikulenga tu kulipiza kisasi katika ushindani wa klabu za soka.

Pinto alikabiliana tena mahakamani mwaka 2025 katika kesi iliyohusishwa zaidi na taarifa binafsi zilizochapishwa kwenye blogu ya Mercado Benfica kati ya 2016 na 2019. Safari hii alikabiliwa na mashtaka 241, yakiwemo ya kuingia kinyume cha sheria katika mafaili, kuingilia mawasiliano binafsi na makosa ya mtandao. Pinto alikanusha kuwa ndiye aliyekuwa nyuma ya blogu hiyo. Hatimaye, aliachiliwa huru dhidi ya mashtaka yote mwezi Aprili 2026.

Wakati huohuo, nyaraka alizokuwa nazo ziliendelea kuvutia wachunguzi wa kimataifa. Mwezi Januari 2024, Pinto alikutana mjini Paris na wachunguzi kutoka Ufaransa, Ujerumani na Ubelgiji na kuwapa fursa ya kufikia makubaliano juu ya tuhuma alizohusishwa nazo  alipokamatwa mwaka 2019. Alisema bado kulikuwa na mambo mengi ambayo hayajachunguzwa.


PINT 06

“MAPAMBANO YATAENDELEA”

Pinto bado anaendelea kufuatilia soka, hasa FC Porto, huku pia akifuatilia kwa karibu kinachoendelea kuhusu Manchester City na mwaka 2024 aliliita sakata la City “kesi yenye mlipuko mkubwa.” Baada ya uamuzi wa tume huru dhidi ya City, alidai kwamba kupitia Football Leaks, kazi yake ilikuwa imechangia kufikisha mambo hayo kwenye uangalizi wa umma.

Lakini, safari ya Pinto haijaishia kwenye Football Leaks. Baada ya kuhukumiwa mwaka 2023, aliandika ujumbe mfupi: “Ni mwisho wa sura moja. Mapambano yataendelea.”

Miaka mitatu baadaye, huku Manchester City ikiwa katikati ya moja ya vita kubwa zaidi za kisheria katika historia yake, jina la Rui Pinto limeibuka tena. Mtu ambaye alianza kuchapisha nyaraka kwa jina la “John” akiwa Budapest sasa anaonekana tena kwenye hadithi inayohusu moja ya klabu kubwa zaidi duniani.