Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viwanja pesa: Man United yauza nyasi za Old Trafford, Barca na almasi za Camp Nou

VIWANJA Pict

Muktasari:

  • Vipande hivyo vyenye ukubwa wa sentimita 7 kwa 7 vimehifadhiwa ndani ya visanduku vya vioo na kuanza kuuzwa wiki hii kwa wanachama na mashabiki wenye tiketi za msimu, baada ya nyasi mpya kuwekwa uwanjani hapo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeanza kuuza vipande vya nyasi za Uwanja wa Old Trafford kwa mashabiki wake, kila kipande kikiuzwa kwa pauni 125 (takriban Sh400,000 za Tanzania).

Vipande hivyo vyenye ukubwa wa sentimita 7 kwa 7 vimehifadhiwa ndani ya visanduku vya vioo na kuanza kuuzwa wiki hii kwa wanachama na mashabiki wenye tiketi za msimu, baada ya nyasi mpya kuwekwa uwanjani hapo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14.

Old Trafford una urefu wa mita 105 na upana wa mita 68. Kwa hesabu za kawaida, iwapo eneo lote la kuchezea lingeuzwa kwa bei hiyo, klabu hiyo ingeweza kukusanya hadi pauni182 milioni.

Hata hivyo, Manchester United si klabu ya kwanza kutumia sehemu za uwanja wake wa zamani kama kumbukumbu za kuuzwa kwa mashabiki. Klabu mbalimbali zimewahi kuhifadhi na kuuza nyasi, viti na vifaa vingine baada ya kubadilisha au kuhamia viwanja vipya.

Hizi ni baadhi ya kumbukumbu za viwanja zilizowahi kuuzwa kwa namna isiyo ya kawaida katika historia ya soka.


VIWANJ 01

1. Barcelona - Almasi za Camp Nou

Barcelona ilikwenda mbali zaidi kwa kugeuza sehemu za nyasi za Uwanja wa Camp Nou kuwa almasi.

Klabu hiyo ilitengeneza almasi zinazozalishwa kwa njia endelevu kwa kutumia kaboni iliyotolewa kwenye udongo wa uwanja huo, uliotumika kwa mechi yake ya mwisho Mei 2023.

Bei ya almasi hizo ilianzia euro 2,500 kwa almasi ya karati 0.5, huku zikitengenezwa almasi 57 pekee za karati moja, kila moja ikiuzwa kwa euro 15,000.

Mashabiki pia waliweza kununua bangili zilizopambwa kwa almasi, nembo za klabu pamoja na mikufu ya dhahabu. Viti na vipande vya nyasi pia vilikuwa sehemu ya mkusanyiko huo wa kumbukumbu za uwanja.


VIWANJ 02
VIWANJ 02

2. Real Madrid- Makabati ya vyumba vya kubadilishia nguo

Real Madrid iliwapa mashabiki nafasi ya kumiliki makabati yaliyowahi kutumiwa na baadhi ya mastaa wakubwa wa soka duniani.

Makabati 24 yaliyotumika katika vyumba vya kubadilishia nguo vya Santiago Bernabeu kati ya mwaka 2001 na 2022 yaliuzwa, kila moja likiwa na jina na picha ya mchezaji aliyewahi kulitumia.

Bei ya kuanzia ilikuwa pauni 10,000, huku kila kabati likiambatana na cheti cha kuthibitisha uhalisi wake na maelezo ya wachezaji waliowahi kulitumia.

Miongoni mwa mastaa waliowahi kutumia makabati hayo ni Cristiano Ronaldo, David Beckham na Zinedine Zidane.

Nembo kubwa ya Real Madrid yenye urefu wa futi 10, iliyokuwa nje ya eneo la vyumba vya kubadilishia nguo, pia iliwekwa mnadani kwa bei ya kuanzia pauni 12,000.


VIWANJ 03

3. Wembley- Milango ya kihistoria

Milango maarufu ya Royal Tunnel ya Uwanja wa Wembley iliokolewa kwa bahati baada ya kukaribia kubomolewa pamoja na uwanja wa zamani.

Milango hiyo mikubwa ya mbao ilitengenezwa mwaka 1923 na ilitumiwa kuwapokea viongozi wa kifalme pamoja na magwiji wa soka katika uwanja huo, ukiwamo mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1966.

Wakati uwanja huo ulipobomolewa mwaka 2000, milango hiyo ilikuwa imesalia siku mbili tu kabla ya kuharibiwa. Hata hivyo, iliokolewa na baadaye kuuzwa kwa mnada mwaka 2011.

Mfanyabiashara wa Chile, Jorge Yarur Bascunan, aliinunua kwa pauni 5,875 pekee kabla ya kuisafirisha kwa zaidi ya kilomita 11,000 hadi Santiago, mji mkuu wa Chile.

Kwa sasa, milango hiyo imehifadhiwa katika Makumbusho ya Fundacion Museo de la Moda.


VIWANJ 04

4. West Ham- Mashine ya kutoa mapovu

Mashabiki wa West Ham walipewa nafasi ya kununua vifaa mbalimbali vya Uwanja wa Upton Park baada ya klabu hiyo kuhamia Uwanja wa Olympic.

Mbali na viti vilivyouzwa kwa pauni 50, mashabiki waliweza kushindana kwa zabuni kununua milingoti ya magoli, milango ya kuingilia, mabango, makombe na hata kiti cha benchi la ufundi.

Hata hivyo, kifaa kilichovutia zaidi kwa namna yake kilikuwa mashine ya kutengeneza mapovu iliyouzwa kwa pauni 20. Mashine hiyo ilikuwa ikitumika wakati wa kupigwa kwa wimbo wa klabu hiyo, ‘I’m Forever Blowing Bubbles’.

Vifaa vingine vilivyouzwa ni baiskeli ya mazoezi iliyokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kitanda cha matibabu ya viungo na mashine ya faksi iliyowahi kutumiwa na makocha wa zamani.

Fedha zilizopatikana zilitengwa kwa ajili ya akademi ya vijana ya klabu hiyo.


VIWANJ 05

5. Millwall - Viti vya benchi la ufundi

Mashabiki wa Millwall walipewa nafasi ya kumiliki sehemu halisi za Uwanja wa The Den wakati mipango ya kuufanyia maboresho ilipoanza.

Miongoni mwa vifaa vilivyowekwa mnadani ni viti vya benchi la ufundi vya timu ya nyumbani na wageni.

Mashabiki pia waliweza kununua mabango ya uwanjani, makombe, vifaa vya maeneo ya mapumziko, ramani na michoro ya mpangilio wa viti.

Ngao ya Timu Bora ya Raundi ya Kombe la Johnstone’s Paint msimu wa 2015/16 pamoja na kombe lenye nembo ya Millwall pia viliuzwa.

Ofisa Mkuu wa Biashara wa klabu hiyo, Luke Wilson, alisema kila kifaa kilikuwa na historia ya klabu, akieleza kuwa kumiliki kiti cha benchi la ufundi ni ndoto ya kila shabiki.


VIWANJ 06

6. Manchester City - Milango ya vyumba vya kubadilishia nguo

Manchester City iliuza vifaa vya Uwanja wa Maine Road kipande baada ya kipande ilipohama mwaka 2003.

Klabu hiyo iliweka mnadani kila kitu, kuanzia viti, milango ya kuingilia, samani za ofisi hadi nyasi za uwanja, ambazo ziliuzwa kwa pauni 10 kwa kila futi ya mraba.

Milango ya vyumba vya kubadilishia nguo ilikuwa miongoni mwa vifaa vilivyowavutia mashabiki waliotaka kuhifadhi kumbukumbu za uwanja huo, ambao ulikuwa makao ya City tangu mwaka 1923.

Mnada huo ulikusanya takriban pauni 400,000, fedha zilizotolewa kwa ajili ya shughuli za hisani.

Maine Road ilibomolewa mwaka uliofuata, huku eneo hilo baadaye likigeuzwa kuwa makazi ya watu.


VIWANJ 07

7. Tottenham - Viti vya White Hart Lane

Mashabiki wa Tottenham walipewa nafasi ya kumiliki sehemu ya Uwanja wa White Hart Lane baada ya uwanja huo maarufu kubomolewa mwaka 2017.

Mashabiki wenye tiketi za msimu waliweza kununua viti vyao halisi vya plastiki vya rangi ya bluu vilivyokunjika kwa pauni 50 kila kimoja, vikiwa vimehifadhiwa ndani ya masanduku maalumu.

Viti hivyo viliondolewa wakati klabu hiyo ilipojiandaa kuuaga uwanja huo baada ya mechi yake ya mwisho ya nyumbani dhidi ya Manchester United.

Ingawa huenda havikuwa kumbukumbu za kifahari, kwa mashabiki waliotumia miaka mingi kuwashuhudia mashujaa wao wakiwa wameketi kwenye viti hivyo, kuvimiliki kulikuwa njia ya kuhifadhi sehemu ya historia ya klabu.


VIWANJ 08

8. Everton - Mabenchi ya mbao ya Goodison Park

Everton iligeuza kumbukumbu za Uwanja wa Goodison Park kuwa bidhaa za gharama baada ya kuanza kuuza viti vya uwanja huo wa kihistoria.

Mashabiki wa klabu hiyo walipewa kipaumbele cha kununua viti hivyo kabla ya vilivyosalia kuuzwa kwa umma.

Kila kiti kiliwekwa kwenye kisanduku maalumu cha kuoneshea na kuambatanishwa na cheti cha kuthibitisha uhalisi wake.

Viti vya mbao viliuzwa kwa pauni 145, huku vya plastiki na vile vyenye sponji vikiuzwa kwa pauni 125, bila kujumuisha gharama za usafirishaji.

Klabu hiyo iliripoti kupata mwitikio mkubwa wa wanunuzi katika awamu ya kwanza ya mauzo.

Hata hivyo, Goodison Park hautapotea kabisa kwani uwanja huo wa kihistoria unatarajiwa kuwa makao ya timu ya wanawake ya Everton na huenda ukatumika pia kwa mechi za akademi baada ya timu ya wanaume kuhamia uwanja mwingine.


VIWANJ 09

9. Sunderland-  Mitambo ya milango ya kuingilia

Mashabiki wa Sunderland walionesha jinsi vifaa vya zamani vya uwanja vinavyoweza kuwa na thamani kubwa baada ya mtambo mmoja wa mlango wa kuingilia wa Uwanja wa Roker Park kuuzwa kwa pauni 800.

Takriban watu 150 walijaza chumba cha mnada, wakionesha kuvutiwa na kifaa hicho kizito cha kihistoria.

Mtambo huo ulielezwa kuwa wa aina ya Deluce’s Patent Rush Preventative, uliotengenezwa na kampuni ya WT Ellison and Co ya Irlams o’ th’ Height, Salford.

Kifaa hicho kilikuwa kizito kiasi kwamba kilihitaji watu watatu kukibeba.

Vifaa vingine vilivyohusishwa na historia ya Roker Park pia viliuzwa, vikiwamo madirisha ya Vaux Ales, bango la zamani la Metro na vikombe vya Vaux.


VIWANJ 10

10. Liverpool -Bango la This Is Anfield

Bango maarufu la ‘This Is Anfield’ la Liverpool lilionesha jinsi kumbukumbu za uwanja zinavyoweza kuuzwa kwa fedha nyingi.

Bango hilo liliwekwa kwa mara ya kwanza kwenye handaki la wachezaji wakati wa utawala wa kocha Bill Shankly mwaka 1972.

Liliwekwa mnadani kwa makadirio ya bei ya pauni 10,000 hadi 15,000, lakini wanunuzi walishindana kwa kiasi kikubwa hadi zabuni ya ushindi kufikia pauni 115,000.

Baada ya kujumuisha kamisheni na kodi, gharama ya mwisho ilifikia pauni 149,500.

Mnunuzi huyo ambaye jina lake halikutajwa awali, baadaye alifahamika kuwa ni mwekezaji katika Hoteli ya Arc iliyopo karibu na uwanja huo.

Bango hilo sasa linatarajiwa kurejea Anfield, huku mipango ikiwa ni kulizindua katika hoteli hiyo pamoja na nyota wa zamani wa Liverpool na wanafamilia wa Shankly.


VIWANJ 11
VIWANJ 11

11. Reading - Nguzo za taa za Elm Park

Mashabiki wa Reading walipewa nafasi ya kununua sehemu za Uwanja wa Elm Park baada ya klabu hiyo kuondoka kwenye makao yake ya kihistoria mwaka 1998.

Elm Park ulikuwa uwanja wa klabu hiyo kwa zaidi ya karne moja na ulikuwa na nafasi ya pekee katika mioyo ya vizazi vya mashabiki wa Reading.

Baadhi ya vifaa vilivyokuwa havihitajiki vilipowekwa mnadani baadaye mwaka huo, mashabiki walijitokeza kwa wingi kutafuta kumbukumbu za uwanja huo.

Miongoni mwa vifaa vilivyovutia ni nguzo za zamani za taa za uwanjani na hata kiti cha mapumziko cha mwenyekiti wa klabu hiyo, John Madejski.

Mnada huo ulikuwa fursa ya mwisho kwa mashabiki kumiliki sehemu ya uwanja huo wa kihistoria.