Wadau wataka suluhu vibali TFF
Muktasari:
- Klabu hizo zimesisitiza kuwa msimamo huo si wa kuikomoa TFF, bali vimechoshwa na mzigo mkubwa wa hasara na madeni yanayovikabili, huku vikilalamika kutopata msaada wowote wa kifedha wa moja kwa moja kutoka shirikisho hilo kusaidia bajeti zao.
GIZANI! Ndivyo unavyoweza kueleza hali halisi ndani ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) baada ya klabu zinavyoshiriki ligi hiyo kufikia hatua ya kuomba kusitisha kushiriki kutokana na ukata na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kila msimu, huku vikilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukaa navyo mezani kusaka suluhu.
Klabu hizo zimesisitiza kuwa msimamo huo si wa kuikomoa TFF, bali vimechoshwa na mzigo mkubwa wa hasara na madeni yanayovikabili, huku vikilalamika kutopata msaada wowote wa kifedha wa moja kwa moja kutoka shirikisho hilo kusaidia bajeti zao.
GHARAMA ZAPANDA JUU
Baadhi ya nyaraka ambazo Mwanaspoti ilionyeshwa na viongozi hao zinadai kuwa ada ya ushiriki wa ligi imepanda kutoka Sh200,000 hadi Sh472,000, huku leseni ya mchezaji wa ndani ikiongezeka kutoka Sh11,800 hadi Sh23,600.
Hali ni mbaya zaidi kwenye usajili wa wachezaji wa kigeni, ambapo ada ya TFF pekee imepanda kutoka Sh3.5 milioni msimu uliopita hadi Sh5.9 milioni hivi sasa.
Ukijumlisha na gharama za kibali cha kufanya kazi na makazi (Work & Residence Permit) kinachofikia Sh7 milioni, klabu inalazimika kutumia hadi Sh12.9 milioni kwa mchezaji mmoja wa kigeni katika ada hizo mbili tu kabla ya kuhesabu mshahara, usafiri, malazi, chakula na bima inayotakiwa ya Sh150,000 kwa kila mchezaji (sawa na Sh6 milioni kwa kikosi cha wachezaji 40).
WASIKIE WADAU
Akizungumzia kadhia hiyo, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka, amekiri kuwa gharama hizo zimekuwa kikwazo kwa timu nyingi ndogo.
"Ndio maana hata sisi msimu uliopita tulipitia changamoto ya kushindwa kuwatumia wachezaji wa kigeni. Sababu kubwa ilikuwa ni changamoto ya vibali ambavyo ni gharama kubwa sana kwa hizi timu ndogo ambazo hazina uwezo mkubwa wa kifedha," amesema Chobanka.
Nao baadhi ya wadau wa soka la wanawake nchini ambao hawakutaka kuwekwa wazi majina yao, wameonyesha kuunga mkono msimamo huo wa klabu huku wakieleza hofu yao kwa timu kama Bunda Girls ambazo hazina pesa za kujiendesha.
"Hivi kwa Sh12 milioni kwa mchezaji mmoja, Bunda Girls watasajili mchezaji wa kigeni kweli? Yaani vibali vinazidi hata ada ya usajili. Pia naiona Ceasiaa ikisubiri tena mpaka mzunguko wa pili au pengine msimu huu isiwatumie kabisa wachezaji wake wa kigeni," amesema mdau mmoja.
Mdau mwingine ameongeza kwa kuomba kuandikwa kwa barua rasmi kwenda kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
"Iandikwe barua kumuomba Waziri asaidie kwa nafasi yake maana hali ni mbaya sana. Mpira umekuwa wa gharama na hata vyama vyetu vya mikoa na wilaya vitakufa. Tunaomba na wadau wengine wajitokeze kuwekeza kwenye soka la wanawake maana mchezo huu umekuwa sana."
Mwanaspoti ilipowatafuta viongozi wa TFF kuzungumzia suala hilo hawakupatikana.