Prime
Ronaldo De Lima kasalitiwa na watoto wake!
Mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Ronaldo De Lima, 49, anajulikana kama mwanasoka aliyefanikiwa sana lakini ni watu wachache wanaojua mbali na soka, R9 ana familia inayojumuisha watoto wanne.
Ndiyo, gwiji huyo wa Brazil aliyeshinda Kombe la Dunia, tuzo ya Ballon d'Or na FIFA, ni baba watoto wanne kutoka katika uhusiano na wanawake watatu tofauti, wawili kati yao akifunga nao ndoa.
Katika toleo hili ambalo ni la tatu kuhusu maisha binafsi ya Ronaldo, tutaangazia watoto hao ila kubwa zaidi ni kuhusu mtoto wake wa kwanza, Ronald, 25, ambaye aliachana na soka na kuwa DJ.
Tunaweza kusema Ronaldo kwa sehemu amesalitiwa na wanawe kwa sababu kwa sasa hakuna hata mmoja anayefuata nyayo zake upande wa soka, wao wanafanya vitu tofauti kabisa kama ifuatavyo;.
Alexander de Lima
Huyu ni mtoto wa pili wa Ronaldo, alizaliwa mwaka 2005 kutokana na uhusiano wake na mhudumu wa mgawaha, Michele Umezu ambaye sasa ni mwanamichezo wa ujenzi mwili (bodybuilder) na mfanyabiashara.
Uhusiano wao ulianza walipokutana Japan wakati Ronaldo akiwa na klabu ya Real Madrid kwenye ziara ya michezo barani Asia, ikiwa ni muda mfupi tu tangu asajiliwe akitokea Inter Milan.
Ilikuwa mwaka 2002, walipokutana kwa mara ya kwanza wakati Ronaldo bado alikuwa katika ndoa na Milene Domingues, mwanasoka wa zamani wa Brazil.
Michele, mzaliwa wa Mato Grosso do Sul, Brazil, alihamia Japan akiwa na miaka 13. Huko alifanya kazi kama mlezi wa watoto, mhudumu wa migahawa na mwanamitindo kwenye matangazo ya kibiashara.
Mwaka 2004, Michele alipata ujauzito ila Ronaldo hakuutambua, ni hadi 2009 aliporejea Brazil na kufanya kipimo cha DNA kilichothibitisha ndiye baba wa Alexander, ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano.
"Wakati wa kipimo cha DNA, tulikuwepo mimi, mtoto wangu, Ronaldo, daktari na wanasheria wetu. Nilikuwa na hofu huenda asingemkubali, lakini hilo halikutokea. Ilikuwa ni hali ya kupendeza sana, nilihisi faraja," Michele aliliambia Jarida la VEJA mnamo 2010.
Kwa sasa, Michele anaendelea na maisha yake kama mwanamke shupavu. Katika ukurasa wake wa Instagram anaposti sana kuhusu mazoezi, mashindano, biashara zake na nyakati maalum akiwa na watoto wake.
Alexander, shauku yake kubwa katika mchezo ipo upande wa ngumi (boxing). Ameamua kujikita katika mazoezi ya ngumi badala ya soka na amekuwa akijifunza zaidi kuhusu mchezo huo huku akiendelea na masomo yake.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, Alexander amehamia New York, Marekani, kwa ajili ya kuendelea na masomo, ila kubwa zaidi ni kufanya mafunzo rasmi ya boxing, akilenga kujijengea jina kwenye mchezo huo.
Maria Sophia & Maria Alice de Lima
Watoto hawa wa kike, Ronaldo aliwapata katika ndoa yake na Maria Beatriz Antony (Bia) iliyodumu kati ya mwaka 2007 hadi 2012. Wawili hao walikutana msimu wa mwisho wa Ronaldo Ulaya wakati akiichezea AC Milan.
Maria Sophia alizaliwa Desemba 24, 2008, mjini Rio de Janeiro, akiwa na uzito wa kilo 3.0 na urefu wa sentimita 49.5. Wakati wa kujifungua, Ronaldo alikuwepo pembeni mwa Beatriz na alionekana mwenye furaha kubwa.
Hata hivyo, awali wawili hao walikanusha kuhusu ujauzito huo lakini mama yake Ronaldo alikuja kuthibitisha habari hizo mnamo Mei 2008 akisema alijisikia furaha sana baada ya kupata habari hiyo.
Maria Sophia ambaye ni mtoto wa kwanza wa kike wa Ronaldo, kwa sasa akiwa na umri wa miaka 17, amejipambanua kama mshawishi wa mitandao ya kijamii (influencer) anayechipukia.
Katika ukurasa wake wa Instagram kila mara huposti picha na video kuhusu maisha yake ya shule, safari na marafiki wake wa karibu.
Anaendelea kuonyesha shauku yake ya kutaka kukua na kujenga himaya katika ulimwengu wa kidijitali akilenga kuonyesha uwezo wake wa kuchuguza na kugundua tamaduni mpya kutoka maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Maria Alice, huyu ni mtoto wa mwisho wa Ronaldo, na ni mtoto wa pili katika ndoa yake na Beatriz Antony. Alizaliwa Aprili 6, 2010, tarehe ambayo tayari ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa mwanasoka huyo.
Hii ni kwa sababu mtoto wa kwanza wa Ronaldo, Ronald, naye pia alizaliwa siku hiyo hiyo, hivyo ndugu hao husherehekea pamoja siku ya kuzaliwa.
Kama ilivyo kwa dada yake, Maria Alice naye anaishi na mama yake lakini mara kwa mara wote humtembelea baba yao na mama wa kambo, Celina Locks huko Hispania wanakoishi.
Sasa akiwa na miaka 15, Maria Alice hupenda kuwashirikisha wafuasi wake maisha yake ya kila siku kupitia mitandao. Bado ni mapema kusema kachagua kufanya nini maishani ila katika soka hayupo kabisa.
Mabinti hawa, wana uhusiano wa karibu na ndugu zao wengine pamoja na baba yao na mara kwa mara huonekana pamoja kwenye matukio ya kifamilia.
Mathalan Septemba 17, mwaka huu, mabinti hao walihudhuria hafla ya uzinduzi wa Casa Rede Ronaldo, mradi mpya wa baba yao unaolenga kuinua michezo. Mbali na hilo, walipiga picha pamoja na mama yao wa kambo, Celina Locks.
Sasa katika toleo lijalo, ndipo tutamuangazia kaka yao, Ronald ambaye aliwahi hadi kuitwa timu ya taifa ya Brazil chini ya miaka 18, kitu alichojivunia Ronaldo De Lima lakini ghalfa akaacha soka na kuwa DJ!.