Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marcus Rashford, amejikuta El Prat, tuendelee kumuombea

PAZIA Pict


EL Prat, uwanja wa pili kwa ukubwa Hispania na ni uwanja wa pili kwa kuwa ‘busy’ Hispania, Jumanne mchana walikuwa wanampokea mgeni mwingine anayeanza kutangatanga kutoka Manchester. Marcus Rashford.


Alizaliwa Manchester, akakulia katika vitongoji vya Fallowfield, Withington na Wythenshawe. Akacheza Manchester United kwa muda mrefu wa maisha yake. Ghafla akiwa na miaka 26 akajikuta akienda kwa mkopo pale Birmingham katika klabu ya Aston Villa.


Sasa katika umri wa miaka 27 amejikuta akiwa miongoni mwa abiria wa Uwanja wa Ndege wa EL Prat kucheza katika klabu yake kubwa ya tatu maishani Barcelona. Ghafla maisha yameenda kasi kwa Marcius Rashford.

Ghafla hatujui alikotoka wala anakokwenda. Kutoka Manchester United kwenda Barcelona siyo jambo la kudharau. Ametoka timu kubwa amekwenda timu kubwa. Hata hivyo, tuna maswali ya msingi kwa Rashford.

Kifupi ametoka katika mkopo mmoja na kwenda katika mkopo mwingine. Wakati anaingia katika kikosi cha kwanza hatukuwahi kufikiria kama siku moja Rashford anaweza kuishi maisha haya. Alikuwa anaonekana anakwenda kuwa mchezaji mwenye hadhi ya kuitwa ‘World Class player’.

PAZ 01

Kama kwenda Hispania basi tuliamini angeuzwa kwa dau ambalo lingeweka rekodi ya uhamisho wa dunia. Labda kwenda Real Madrid kwa dau la Pauni 160 milioni. Ni kama ambavyo Madrid wakijaribu kwa Bukayo Saka sasa hivi.

Hata hivyo, maisha yake ya soka yameyumba. Pale Manchester United, alikuwa hatabiriki. Kuna msimu angekuwa wa moto, kuna msimu angekuwa wa baridi. Kuna msimu alikuwa wa moto kiasi na Manchester United walipeleka mshahara wake hadi Pauni 300,000 kwa wiki.

Mkataba wake ulikuwa unakaribia kwisha na Rashford alikuwa wa moto sokoni. United wasingemruhusu aende kokote baada ya msimu ule. Hata hivyo, baada ya kusaini mkataba ule akarudi kuwa mchezaji wa kawaida tu.

PAZ 02

Wakati fulani kulikuwa na mjadala kuhusu nafasi yake. Wakati Jose Mourinho akifundisha Manchester United alisikika akisema kwa uzoefu wake wa kuwajua wanasoka Rashford alipaswa kucheza kama winga wa kushoto na sio mshambuliaji wa kati.

Ilizuka mijadala mingi kwa wachambuzi wetu kina Gary Neville, Roy Keane, Jamie Carragher na wengineo. Mwishowe hadi leo hatujui kama Mourinho alikuwa sahihi au hapana kwa sababu kuna siku Rashford anakuwa mkali, kuna siku anakuwa mchezaji wa kawaida tu.

Na kuna maisha mengine yanachanganya sana. Pale mazoezini Carrington makocha wamelalamika kuhusu tabia za Rashford. Alianza Erik Ten Hag, kisha sasa hivi Ruben Amorim. Anaonekana kama vile mvivu na ambaye hapendi kujituma.

PAZ 03

Amorim ndiye aliyefungua boksi la Pandora kwa kuamua kumpeleka Rashford kwa mkopo Aston Villa. Na sasa ameamua kumpeleka kwa mkopo Barcelona, huku kukiwa na kipengele cha kumuuza moja kwa moja.

Nje ya uwanja Rashford ni mtu mwema tu. Kuna wakati alikuwa na kampeni ya kusambaza chakula shuleni kwa watoto ambao hawakuwa na uwezo. Labda kwa sababu utotoni mama yake mzazi, Melanie Maynard alikuwa anafanya kazi ngumu peke yake bila ya mzazi mwenzie kwa ajili ya kuwalisha Rashford na ndugu zake.

Mgawanyo wa mawazo ulitokea hapo. Katika viwanja vya mazoezi pale Carrington makocha walikuwa wanamtafsiri tofauti na namna ambavyo jamii ilikuwa inamtafsiri huku mtaani. Hata hivyo, kitu cha msingi kilikuwa zaidi uwanjani.

PAZ 04

Hata sasa hivi tunavyozungumza ni kwamba mashabiki wa United hawajasimama sana upande wa Rashford. Labda kama Manchester itaendelea kuwa na washambuliaji wachovu kama Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee ndipo mashabiki watamkumbuka Rashford.

Lakini kama United itasajili washambuliaji wakali zaidi ya Rashford basi anaweza kusahaulika mapema tu. Na baada ya hapo kitakachobaki ni kujadili maisha yake Nou Camp yatakwenda vipi. Nini kinaenda kumtokea?

Kuna wachezaji ambao wanakuwa wakali katika kipindi fulani cha mwanzo cha maisha yao, lakini kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo ambavyo wanashindwa kueleweka. Wapo wachezaji wengi wa namna hii. Wanakuja kisha wanakataa.

Mfano ni rafiki yetu, Philippe Coutinho. Naye alikimbilia hapo hapo Barcelona baada ya kuwa mchezaji mzuri Liverpool. Baada ya hapo kilichomtokea wote tulijua. Ni aina ya wachezaji ambao hawajawahi kufika kileleni kabisa katika maisha yao ya soka, ili wakimaliza tuweze kuwaelezea walikuwa wachezaji wa aina gani.

PAZ 05

Kina Ronaldo di Lima licha ya kuondoka mapema katika soka. Akanenepa katika umri wa miaka 29 tu lakini tunajua namna ambavyo walifika katika vilele vya ubora wao. Sijui kama Rashford atarudi na kuanzia katika msimu ule ambao Manchester United waliamua kumpa Pauni 300,000 kwa wiki.

Hatima ipo mikononi mwake. Akigeuka kulia kuna Lamine Yamal. Akigeuka kushoto kuna Rapinha. Nyuma yake kuna kina Gavi na Pedri. Hana kisingizio pindi linapokuja suala la ndani ya uwanja. Labda arudishe tabia zile zile alizozionyesha wakati akiwa na kina Teg Hag.

Na atakosa kisingizio kabisa kwa sababu wakati akiwa na Manchester United angeweza kudai alikuwa anacheza na wachezaji wa kawaida. Lakini sasa anakwenda kucheza na wachezaji wenye ubora mwingine ambao unaweza kumfanya kuwa bora zaidi.

Mwisho wa msimu tutaona kama Barcelona wataweza kumchukua jumla. Hadi sasa katika mkopo wake huu unamfanya awe mchezaji wa pili kutoka England kucheza Barcelona. Wa kwanza alikuwa Gary Lineker wakati ule alipotoka kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia mwaka 1986 pale Mexico alipata nafasi ya kuhamia Catalunya.

Wachezaji wengi wa Kiingereza kwao huwa ni Madrid. Kina Jonathan Wooddgate, Michael Owen, David Beckham, na hata sasa hivi wana Jude Belingham. Nataka kuona kama Rashford anaweza kuendeleza kijiwe kingine cha Waingereza ndani ya Hispania.

Inabidi awe makini maana kwa tabia zake za kupenda kula bata pale atakuwa amekutana na Lamine Yamal ambaye kwa siku za karibuni amejipambanua kuwa ni nje ya uwanja anapenda starehe. Na tunavyomjua Rashford pia ni mchezaji wa aina hiyo.