RB Leipzig inavyotengeneza mastaa Ulaya, ikivuna minoti
Muktasari:
- Lakini, mfumo wa timu hiyo wa usajili wa wachezaji wadogo, kuwalea hadi kufikia viwango vya juu na kisha kuwauza kwa fedha nyingi, umegeuka kuwa karata ya kipekee ya kuvuna mkwanja kwa klabu hiyo changa ya Ujerumani.
MUNICH, UJERUMANI: RB Leipzig inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) ilianzishwa 2009, wakati Yan Diomande, miongoni mwa wachezaji wake wa hivi karibuni kuuzwa kwa mamilioni ya fedha akiwa na umri wa miaka mitatu.
Lakini, mfumo wa timu hiyo wa usajili wa wachezaji wadogo, kuwalea hadi kufikia viwango vya juu na kisha kuwauza kwa fedha nyingi, umegeuka kuwa karata ya kipekee ya kuvuna mkwanja kwa klabu hiyo changa ya Ujerumani.
Kwa RB Leipzig, mamilioni yanaendelea kumiminika klabuni na yataendelea kufanya hivyo.
Kutoka Red Bull, lakini kwa chenga.
RB Leipzig inahusishwa na dhana ya “chenga” tangu ilipoanzishwa. Herufi RB zinawakilisha Red Bull, kampuni kubwa ya kimataifa inayotengeneza vinywaji vya kuongeza nguvu. Hata hivyo, ili kuepuka kuvunja kanuni za Bundesliga, jina hilo rasmi pia linaelezwa kumaanisha RasenBallsport, yaani mchezo wa mpira kwenye nyasi. Ni kama chenga nyingine!
Zaidi ya hapo, RB Leipzig ni kama mdogo wa Red Bull Salzburg, klabu ambayo iliwahi kuwa kituo cha kukuza kipaji cha Erling Haaland. Leipzig na Salzburg zimekuwa zikifanya kazi kama mfumo wa kupitishia na kukuza wachezaji Ulaya.
Katika msimu wa 2016/17, RB Leipzig ilifika “peponi” baada ya kutimiza lengo lake kubwa la kwanza kupanda hadi Bundesliga. Ulikuwa wakati mwafaka kwa klabu hiyo kuanza kuionyesha dunia siri za mfumo wake wa kibiashara na kisoka.
Keita, mwanzo wa biashara kubwa
Baada ya kuingia kwenye ligi ya wakubwa, klabu hiyo iliimarisha zaidi mfumo wake wa kusaka vipaji vidogo ambavyo bado havikuwa vinajulikana sana. Hapo ndipo safari ya kuzalisha nyota na kufanya biashara kubwa ilipoanza.
Mauzo makubwa ya kwanza yalikuja mapema. Katika msimu wa 2018/19, RB Leipzig ilimuuza Naby Keita kwenda Liverpool kwa Euro 60 milioni, ambapo kiungo huyo wa kimataifa wa Guinea hakufanikiwa sana akiwa Anfield, licha ya matarajio makubwa yaliyokuwepo.
Mwaka mmoja baadaye, mchezaji mwingine aliyekuwa akifahamika kutoka La Liga, Matheus Cunha, aliyekuwa na umri wa miaka 20, alisajiliwa na Hertha Berlin baada ya kulipa Euro 18 milioni. Hata hivyo, sherehe kubwa ya mamilioni ilikuwa bado haijaanza huko RB Leipzig.
Katika msimu wa 2020/21, licha ya changamoto za janga la corona, Leipzig ilimuaga nyota wake mkubwa, Timo Werner, aliyesajiliwa na Chelsea kwa Euro 53 milioni. Baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wake wa kwanza Chelsea, Werner hakufikia kiwango kilichotarajiwa kutokana na gharama iliyolipwa, na huko London ikawa mwanzo wa kushuka kwake kisoka.
Upamecano na Konate, wawili kwa mpigo
Kwa Leipzig msimu wa 2021/22 ulikuwa wa mabeki wenye nguvu waliokuwa wakivutia klabu kubwa barani Ulaya, ambapo Bayern Munich ilimnunua Dayot Upamecano kwa Euro 42 milioni.
Wakati huohuo, Leipzig walimuuza Ibrahima Konate kwenda Liverpool kwa Euro 40 milioni. Mabeki hao wote walikuwa na umri wa miaka 22 wakati wa kuuzwa.
Msimu uliofuata haukuwa na kelele nyingi sana, licha ya Ademola Lookman kuuzwa kwenda Atalanta kwa Euro 16 milioni. Lakini ilikuwa wazi kwamba mambo makubwa zaidi yalikuwa yanakuja.
Gvardiol na Szoboszlai, benchi la dhahabu
Katika msimu wa 2023/24, klabu hiyo ilimuuza beki wa kimataifa wa Croatia, Josko Gvardiol kwenda Manchester City ya Pep Guardiola kwa Euro 90 milioni. Beki huyo alikuwa na umri wa miaka 21 na alionekana kuwa miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa baadaye.
Pia kiungo wa Hungary mwenye nguvu, ubora na uwezo mkubwa wa kupiga pasi, Dominik Szoboszlai, mwenye umri wa miaka 22, alichukuliwa na Liverpool baada ya kulipa Euro 70 milioni.
Hadi sasa, kiungo huyo ni sehemu muhimu ya kikosi cha Liverpool. Lakini wimbi la fedha kwa klabu hiyo halikuishia hapo, kwani Mfaransa Christopher Nkunku aliyekuwa ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa Bundesliga alihamia Chelsea kwa ada ya Euro 60 milioni.
Olmo aondoka kwa Euro 61 milioni
Msimu wa 2024/25 ulikuwa na ladha ya Kihispania, baada ya kutumia miaka mitano yenye mafanikio RB Leipzig, Dani Olmo alijiunga na Barcelona, ambayo ililipa Euro 61 milioni kumnasa kiungo huyo ambaye alikwenda kukiwasha Hispania na kuisaidia Barca kutwaa ubingwa msimu uliopita.
Nyota huyo mwenye pasi 'rula' pia alikwenda kukiwasha katika Kombe la Dunia 2026 lililopita ambako alibeba ubingwa.
Simons na Sesko, utajiri mwingine
Msimu uliopita haukuwa tofauti sana kwa Leipzig, ambapo mshambuliaji wa kimataifa wa Slovenia, Benjamin Sesko aliyekuwa akiendelea kung'ara kama treni hadi Manchester United ilipolipa Euro 76 milioni kumsajili katika jitihada zake za kurejea kwenye njia ya kushinda mataji.
RB Leipzig pia ilimlea na kumpa nafasi Xavi Simons, aliyewahi kuwa sehemu ya akademi ya Barcelona, na nyota huyo hatimaye aliishawishi Tottenham Hotspur iliyolipa Euro 65 milioni kumnunua.
Diomande avunja rekodi
Na sasa katika dirisha la usajili linaloendelea Ulaya winga Yan Diomande amekuwa mchezaji mojawapo katika orodha ya mastaa waliotua na kuondoka Leipzig, ingawa ni katika muda mfupi.
Uhamisho wake wa Euro 125 milioni kwenda Real Madrid umekuwa mkubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo. Pia, Leipzig haijawahi kumuuza mchezaji mwenye umri mdogo kiasi hicho kwa kiasi kikubwa kama hicho.
Winga huyo wa Ivory Coast ameifanya biashara nyingine kubwa ya majira haya. Pia kumbuka kwamba kuna Lois Openda aliyejiunga na Juventus kwa Euro 42 milioni. Inavyoonekana mfumo wa RB Leipzig wa kusaka vipaji vyenye umri mdogo, kuvikuza na kuviuza kwa mamilioni haupumziki.