Prime
PUMZI YA MOTO: Yanga ilicheza ngoma ya Simba, ikadodesha Wiki ya Mwananchi

SIKU ya Mwananchi, tamasha kubwa la Yanga kumtambulisha wachezaji wao, limefanyika tena kwa mara ya tano lakini safari hii likiwa na muitikio mdogo sana.
Hii ni tofauti na matamasha Yao yote yaliyopita ambayo muitikio ulikuwa mkubwa na shamrashamra zilikuwa kubwa pia.
Kuna mengi yanayoweza kushusha mzuka wa mashabiki kiasi kulipoozesha tamasha, kwa mfano taarifa za kuondoka kwa nyota wao Fiston Mayele na kukosa nyota wa uhakika wa kuliuza tamasha.
Pia kauli ya mmoja wa watu wa wageni wao, Kaizer Chiefs, aliyesema wao wanoijua zaidi Simba kuliko Yanga...hiyo inakera na inaweza kusababisha baadhi ya mashabiki lia lia wasitamani kuiona kabisa hiyo Kaizer Chiefs yenyewe.
Lakini kubwa kuliko zote ni mkakati kabambe wa Simba kuhakikisha Yanga hawapati muda wa kuzungumziwa katika wakati wote wa kuelekea tamasha lao.
Simba walitengeneza mfululizo wa matukio ambayo yalimeza stori ya tamasha la Yanga na kuteka mazungumzo katika vijiwe vyote vya soka, iwe vyao Simba wenyewe na hata vya Yanga.
Kwa muda mrefu, watu wa Yanga, kuanzia viongozi hadi watengeneza ushawishi wao walikuwa na pilika pilika za kujadili kinachoendelea Simba kuliko tamasha lao.
1. Sakata la Chama
Iwe kweli au mtego, sakata la Chama liliwateka watu wa Yanga na kusahau kabisa kwamba wanatakiwa kuhamasisha watu wao kwa ajili ya tamasha.
Wasemaji wao, wahamishaji wao na wale vijana wa mitandao ya kijamii, wote walikuwa bize kumzungumzia Chama.
Habari zilisema Chama hataki kwenda Uturuki kuungana na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya kabla ya msimu hadi aongezewe maslahi.
Yanga wakalibeba hilo zima zima na kulifanya ajenda, badala ya kuelekeza nguvu zao kwenye kulitangaza tamasha lao.
2. Tweet za Mo
Mwekezaji wa Simba naye alicheza sana na akili za Yanga. Alikuja na mkakati wa kutoa matamko yenye utata kupitia mitandao ya kijamii ambayo yaliwasisimua zaidi Yanga na kuwapotezea dira.
Nakaribia kukata tamaa kilikuwa kifungu cha maneno kilichowashughulisha zaidi Yanga kuliko tamasha lao.
Inajulikana kwamba matatizo ya mtani mmoja ni sherehe mtani mwingine...kwa hiyo hiyo ilikuwa habari njema kwa Yanga. Lakini hawakuwa makini kubaini kwamba labda ulikuwa mtego.
Kabla hawajakaa sawa akaibuka Barbara naye na tweet zake za mafumbo...akapiga mule mule.
Yanga wakajikuta wanapata raha kama ya mtumia dawa za kulevya, anastarehe huku anajiangamiza.
Siku zinazidi kwenda na tamasha linakaribia...lakini wao hawashtuki.
3. Uzinduzi wa jezi milimani Kilimanjaro
Hili nalo likawa pigo jingine kwa Yanga. Huwezi amini walihangaika kufukua mafaili ya zamani kupata picha ambazo wao pia walipeleka jezi mlimani.
Wakasahau kwamba wao walipeleka jezi, siyo walizindua. Wakasahau kwamba wao wana tamasha linakuja.
Wakaacha kucheza ngoma yao, wakaanza kucheza ngoma ya Simba...wakawa wameingia kwenye mtego.
Na Simba walivyokuwa makini...wakapeleka kibegi cha jezi mlimani na kuhakikisha kinazungumziwa njia nzima.
Matokeo yake safari ya kibegi ikawa kubwa kuliko ya tamasha. Hatimaye kikafika kileleni...jezi zikazinduliwa.
Yanga na watu wote wakaanza kuzichambua jezi za Simba...kosa jingine. Tamasha limekaribia lakini hakuna anayelikumbuka.
Siyo Ally Kamwe, siyo Privadinho wala Haji Manara...wote wako bize na jezi za Simba!
Kama kuna watu wa kulaumiwa, basi Yanga wajilaumu wenyewe.
Hawakuwa na mkakati madhubuti wa kujaza uwanja...na walizidiwa sana maarifa na wapinzani wao, Simba.
Angalia kilichotokoea, tamasha lilipofika, Simba wakakaa kimya...hakuna tweet za Mo wala Barbara. Chama yuko Uturuki na anawang'ong'a kupitia mitandao (mlisema hafiki Uturuki hapa ni wapi?) na jezi zimeshazinduliwa zipo dukani.
Yanga hawana cha kuongelea kwa sababu muda mrefu walikuwa bize na mambo ya Simba.
Matokeo yake tamasha limekuja kimya kimya na likafanyika kimya kimya.
Nadhani safari nyingine Yanga wajifunze kuwa makini zaidi na mitego ya Simba.
Waulize akili zao kwenye mambo yao badala ya kuhangaika na mambo ya Simba...yanawapotezea uelekeo.
Hali kama hii huitwa umajinuni (obsession) yaani unakuwa na hisia na kitu hadi kinakutoa nje ya reli.
Rudi nyuma hadi mwaka 2010 kwenye nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kati ya Barcelona na Inter Milan.
Fainali ya mwaka huo ilipangwa kufanyika uwanja wa Santiago Bernabeu wa Real Madrid.
Kocha wa Inter Milan wakati huo, Jose Mourinho, alitumia maneno mawili kuzielezea timu hizo na hamu ya ubingwa...dream na obsession, yaani ndoto na umajinuni.
Ndoto ni ile hali ambayo mtu amekuwa nayo siku zote kufanikisha jambo lake au siku moja kuwa katika hali fulani.
Umajinuni ni ile hali ya kutaka jambo liwe kama unavyotaka wewe kutokana na kulipenda sana.
Akasema,
"For Inter it's a dream because they haven't been in the Champions League final since 1965. But for Barcelona it's an obsession, because they won last season.
But this time they want to go and win at Santiago Bernabeu because they are obsessed with Real Madrid."
Kwamba kwa Inter Milan fainali na hatimaye ubingwa ilikuwa ndoto ya klabu kwa sababu hawajawahi kufika hatua hiyo tangu mwaka 1965.
Lakini kwa Barcelona haikuwa ndoto kwa sababu wao ndiyo walikuwa mabingwa watetezi.
Shida yao ilikuwa kwenda kushinda ubingwa Santiago Bernabeu kwa sababu ya umajinuni wao kwa Real Madrid.