PUMZI YA MOTO: Tutarajie msimu wa Ligi kwisha Julai
Muktasari:
- Kombe la Mapinduzi litaisha Januari 13, na siku tatu baadaye yaani Januari 16 itaanza kambi ya timu ya taifa kujiandaa na Chan halafu Februari ndiyo mwezi wa Chan yenyewe. Kwa hiyo msimu wetu utarudi tena kuanzia Machi Mosi.
NAAM Ligi Kuu Bara imesimama hadi Machi Mosi, 2025. Hii ni kwa sababu ya kupisha Kombe la Mapinduzi, kambi ya timu ya taifa kujiandaa na Chan na mwisho Chan yenyewe.
Kombe la Mapinduzi litaisha Januari 13, na siku tatu baadaye yaani Januari 16 itaanza kambi ya timu ya taifa kujiandaa na Chan halafu Februari ndiyo mwezi wa Chan yenyewe. Kwa hiyo msimu wetu utarudi tena kuanzia Machi Mosi.
Kwa kawaida msimu hutamatika Mei au Juni mwanzoni. Maana yake tutakuwa na miezi mitatu ya kuhakikisha msimu unaisha. Hapo nazungumzia Machi, Aprili na Mei.
Sasa hebu pata picha kuna Ligi kKuu ambayo ipo katikati - bado mechi zaidi ya 250. Kuna Kombe la Shirikisho ambalo limeshachezwa mzunguko wa kwanza pekee. Kuna Kombe la Muungano ambalo safari hii kutakuwa na timu nane. Kuna mechi za kimataifa, kalenda ya Fifa, kufuzu Kombe la Dunia. Na mwisho kuna mashindano ya klabu Afrika endapo Simba na Yanga zitasonga mbele.
Haya yote yafanyike ndani ya miezi hii mitatu, itawezekana kweli? Hapo ndipo kwenye msingi wa hoja yangu kwamba ligi yetu itakuwa kama ya Misri ambayo huendelea hadi mwezi wa nane.
UGUMU WAKE
Hadi ligi inasimama mzunguko wa kwanza wote ulikuwa umeshakamilika, huku baadhi ya timu zikiwa tayari zimeuanza mzunguko wa pili. Ligi Kuu inatarajiwa kurudi kuanzia Machi Mosi.
Machi 17 na Machi 24 kutakuwa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia. Tanzania itakuwa na mechi mbili; dhidi ya Jamhuri ya Kongo Machi 17 na dhidi ya Morocco Machi 24.
Kawaida yetu lazima kuwe na angalau kambi ya wiki moja kabla ya mechi hizi. Kwa hiyo tutarajie Stars kuingia kambini kuanzia Machi 10. Hii ina maana kwamba kunaweza kuwa na raundi mbili tu zimechezwa tangu ligi irudi.
Mwezi huohuo lazima kutakuwa na mechi za raundi ya pili za Kombe la Shirikisho ambazo zitakuja baada ya mechi za timu ya taifa. Hadi hapo mwezi wa tatu utakuwa umeisha.
Mwezi wa nne tutarajie ligi kuendelea, mwezi ambao pia utakuwa na Kombe la Muungano. Taarifa za awali zinasema safari hii kutakuwa na timu nne za Bara na nne za Zanzibar, maana yake kutakuwa na timu nane.
Hata kama mechi zitachezwa kwa mtoano mashindano hayo hayawezi kuchezwa chini ya wiki mbili endapo kweli kutakuwa na timu nane. Mwezi huohuo pia utakuwa na Kombe la Shirikisho.
Maana yake katika wiki nne za Aprili, wiki moja tu inaweza kuwa ya Ligi Kuu. Na kama itakuwa hivyo maana yake ligi itakuwa haijafika hata raundi ya 20 na Aprili imeisha. Tutabaki na Mei tu, huku tuna mechi zaidi ya 200 zinatusubiri.
Haiwezekani mechi hizi zote kuchezwa ndani ya Mei na hata Juni, hata kama tutakimbizana namna gani. Tukumbuke hapo pia Kombe la Shirikisho bado litakuwa halijafika nusu fainali. Na bado mashindano ya Afrika kwa klabu endapo Simba na Yanga zitaenda mbali.
TAHADHARI
Kwa misimamo ya Bodi ya Ligi kupitia kauli ya mtendaji wake mkuu, Kasongo Almasi, ligi itaisha Mei. Hii ina maana kwamba ratiba itakapotoka itakuwa na mechi zilizobanana sana - yawezekana hata tatu kwa wiki.
Hii itawasaidia bodi kulinda ratiba yao, lakini itaua viwango vya wachezaji. Hakutakuwa na muda wa wachezaji kupumzisha miili na kuisaidia kurudi kwenye hali ya kawaida. Hili si jambo lenye faida kwa mpira na kwa wachezaji wetu.
Sisi sote tunaona mazingira yaliyosababisha mtafaruku huu. Hatuna lawama za moja kwa moja kwa Bodi ya Ligi. Kwa hiyo hakuna haja ya bodi kufanya zaidi ya kawaida kiasi cha kutesa wachezaji ili kuilinda ratiba.
Acha ligi iendelee hata ikifika Oktoba tutajua cha kufanya lakini tusitese wachezaji. Nchi yetu ni kubwa sana kijiografia na timu zimegawanyika katika mikoa mbalimbali.
Kuzipanga mechi kila baada ya siku tatu ni kuwapa mateso makubwa wachezaji wa timu ambazo haziwezi kusafiri kwa ndege.
Bodi ya Ligi watulize munkari, walete ratiba yenye kutoa nafasi kwa wachezaji kupumzika ili kurudisha nguvu baada ya mechi.
Mwaka huu kutakuwa na Afcon kule Morocco, timu yetu ya taifa inawategemea wachezaji wanaocheza kwenye ligi ili kushiriki mashindano hayo.
Tukiwawekea ratiba yenye kuwatesa tutawachosha na watashindwa kutusaidia kwenye Afcon. Hasara itakuwa kwetu wenyewe. Tujiandae kupokea na kukubali kuchelewa kumalizika kwa ligi, ili kujipunguzia presha ya kuandaa ratiba kwa pupa na hamaki.