Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Eng. Hersi aanika Siri Yanga na hatua inayofuata

HERSI Pict


SIKU tatu baada ya kupewa dhamana ya kuendelea kuiongoza tena Yanga kwa kipindi kijacho cha miaka minne, rais wa klabu hiyo, Eng. Hersi Said, leo Agosti 5, 2026, anatarajiwa kutua ndani ya makao makuu ya Mwananchi Communications Limited kikiwa ni chombo cha kwanza cha habari anakitembelea baada ya kuchaguliwa tena.


Hersi aliyeidhinishwa na wanachama wa Yanga kwa kishindo kuendelea kuiongoza klabu hiyo katika mkutano mkuu uliofanyika Agosti 2, 2026 jijini Dar es Salaam, anafanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya Mwananchi Communications Limited na Yanga SC.


Katika ziara yake hiyo, Hersi atatembelea sehemu mbalimbali kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanywa na Mwananchi Communication Limited, kampuni inayochapisha magazeti ya Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen, sambamba na kutoa taarifa za kidijitali ikiwa na makao yake makuu Tabata jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo amekuwa na mafanikio makubwa ya uongozi wake ndani ya Yanga kwa kipindi cha miaka minne iliyopita tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza Juni 2022.

Akizungumzia mafanikio yake hayo, Hersi amesema kipindi cha miaka minne ya uongozi wake kimekuwa cha kihistoria kwa klabu hiyo baada ya kuvunja rekodi mbalimbali ndani na nje ya uwanja, ikiwemo kutwaa mataji 16, kucheza hatua za makundi za CAF mara tatu mfululizo na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza mbele ya wanachama na viongozi wa Yanga katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Agosti 2, 2026, Hersi alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mshikamano wa wanachama, viongozi na mashabiki ambao wameendelea kuiunga mkono Yanga katika kila hatua.

“Imekuwa miaka minne yenye mafanikio kwa klabu yetu ikiweka historia mbalimbali, lakini kipekee tumepata ushirikiano mkubwa wa wanachama na wapenzi wa Young Africans katika kutuunga mkono kwenye uongozi wetu,” alisema Hersi.

HERS 01

MATAJI 16

Hersi alisema katika kipindi hicho cha miaka minne, Yanga imeweka rekodi ya kutwaa mataji 16, idadi ambayo amesema haijawahi kufikiwa na klabu yoyote katika historia ya soka la Tanzania.

Alifafanua kuwa, mataji hayo yanajumuisha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tano mfululizo, Kombe la Shirikisho (CRDB Federation Cup) mara nne, Ngao ya Jamii mara tatu, Mapinduzi Cup, Muungano Cup pamoja na mataji ya kimataifa ya Toyota Cup nchini Afrika Kusini na Rayon Sports Cup nchini Rwanda.

“Huenda ikawa ni historia, katika kipindi cha miaka minne tumeweza kubeba mataji 16, rekodi ya juu kuliko zote katika historia ya mpira wa taifa letu,” alisema.


REKODI ZA UWANJANI

Mbali na mataji, Hersi alisema takwimu za timu hiyo ndani ya uwanja zinaonyesha ubora uliodumu kwa misimu minne mfululizo.

Kwa mujibu wa rais huyo, Yanga imecheza mechi 120 za Ligi Kuu kati ya msimu wa 2022-2023 hadi 2025-2026, ikishinda mechi 101, kutoka sare 12 na kupoteza mechi saba pekee.

Matokeo hayo yameiwezesha klabu hiyo kukusanya pointi 315, ambazo amesema ni rekodi mpya katika historia ya ligi nchini.

“Hakuna timu katika historia ya mpira wa miguu Tanzania iliyowahi kukusanya pointi nyingi kiasi hiki,” alisisitiza.

Katika kipindi hicho, Yanga imefunga mabao 286 huku ikiruhusu mabao 51 pekee, ikiwa na tofauti ya mabao 235.

HERS 02

MOTO WA FA

Hersi alisema Yanga imeendelea kutawala Kombe la Shirikisho (FA) kwa kutwaa ubingwa mara nne mfululizo na kuweka rekodi nyingine ambayo bado haijavunjwa.

Alisema katika kipindi cha misimu mitano, timu hiyo imecheza mechi 28 za mashindano hayo, ikishinda mechi 27 mfululizo kabla ya rekodi hiyo kusimama katika mchezo wa mwisho wa msimu uliopita.

“Ni rekodi ambayo haijawahi kutokea nchini na hata katika mataifa mengi ya Afrika,” alisema.


KIMATAIFA

Katika mashindano ya CAF, Hersi alisema uongozi wake umeandika ukurasa mpya wa historia kwa kuifikisha Yanga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza mwaka 2023 baada ya kusubiri kwa miaka 25.

Alisema tangu wakati huo, Yanga imefanikiwa kucheza hatua ya makundi mara tatu mfululizo, rekodi ambayo pia haijawahi kufikiwa na klabu yoyote ya Tanzania.

Mbali na hilo, alikumbushia safari ya kihistoria ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2023, ambapo Yanga ilikosa ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.


NGUVU MPYA TIMU ZA VIJANA

Hersi alisema mafanikio hayo hayajaishia kwenye timu ya wakubwa pekee, bali pia kwenye programu ya maendeleo ya vijana.

Alisema ndani ya miezi sita tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa kukuza vipaji, Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa wa mashindano ya chini ya miaka 13.

Aidha, timu ya Yanga chini ya miaka 17 ilitwaa ubingwa wa taifa mwaka 2026, huku kipa wa timu hiyo akimaliza mashindano akiwa na ‘clean sheet’ saba katika mechi 14 na mshambuliaji wa timu hiyo kuwa mfungaji bora kwa mabao 20 katika mechi hizo.

Hersi alisema mafanikio yaliyopatikana yametokana na umoja ndani ya klabu na kusisitiza kuwa mshikamano ndiyo silaha muhimu ya kuendelea kutwaa mataji.

“Tunapaswa kuwa kitu kimoja tukiwa ndani ili tukashindane tukiwa nje. Hatupaswi kuwa washindani ndani kwa sababu tutapunguza nguvu zetu za kupambana na wapinzani wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa maandalizi ya msimu mpya tayari yameanza na akaonyesha matumaini ya kutwaa ubingwa wa sita wa Ligi Kuu Bara mfululizo.

“Kwa kazi ambayo tumeshaanza kuifanya kwa ajili ya msimu unaofuata, panapo majaliwa, tukikutana hapa mwaka ujao tutaleta taji letu la sita na kuweka historia ambayo hakuna mtu ameifikia,” alisema.

HERS 03

MADENI

Hata hivyo pamoja na Hersi kufanya mambo makubwa kwa kipindi cha miaka minne, bosi huyo sasa ana madeni kadhaa ambayo mashabiki na wanachama wa Yanga wanayasubiri kutoka kwake.

Kwa mashabiki na wanachama wa Yanga wanasubiri ahadi ya uwanja mpya ambao uongozi wa timu hiyo ulisema kuwa utaanza ujenzi wake hivi karibuni na unatarajiwa kukamilika mwaka mmoja ujao.

Pili mashabiki wanatamani kuiona timu hiyo ikifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikiwezekana ichukue ubingwa huo mkubwa zaidi kwa upande wa soka Afrika.

Kuchukua ubingwa huo kunaweza kuifanya Yanga ikawa timu yenye mafanikio makubwa zaidi ndani na nje ya nchi, ikiwa imeshafika robo fainali ya michuano hiyo lakini fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.