Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kangwanda katika mtego wa Aziz KI, Ahoua


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Klabu ya Yanga inaendelea kuimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, ambapo hadi sasa tayari tumeshuhudia nyota wapya 10, wakitambulishwa, wakiwemo sita wazawa na wengine wanne wa kigeni.


Wachezaji hao ni Juma Issa Abushiri aliyetokea Fountain Gate, Hussein Juma Mihambo, Abdulnasir Assa ‘Gamal’ na Mohamed Mussa wote wakitokea Mashujaa FC, Erick Mwijage (KMC FC) na Suleiman Mbarouk ‘Mpemba D’ aliyetoka JKU FC ya Zanzibar.

Nyota wanne wa kigeni ni Cheikh Ibrahima Toure aliyetokea Al-Jabalain FC ya Saudi Arabia, Albert Kangwanda (Red Arrows FC), Housseine Zakouani (Al-Zulfi SFC) na Peter Shalulile aliyeachana na timu ya Mamelodi Sundowns FC ya Afrika Kusini.

Nyota wa Yanga atakayeangaliwa pia ni kiungo mshambuliaji, Albert Kangwanda aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Red Arrows FC ya kwao Zambia, ambaye kwa msimu wa 2025-2026, alikuwa ni mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Zambia (MVP).

Usajili wa nyota huyo unamfanya kumweka katika mtego wa mastaa wengine mbalimbali waliotoka nchi nyingine wakiwa ndio wachezaji bora (MVP) na kuonyesha kiwango kizuri, wakiwemo, Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Jean Charles Ahoua.

Mwanaspoti linakuletea rekodi mbalimbali zilizowekwa na Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Jean Charles Ahoua katika Ligi Kuu Bara, baada ya kutoka sehemu nyingine wakiwa ndio wachezaji bora (MVP), jambo linalomsubiria Albert Kangwanda.


STEPHANE AZIZ KI

Aziz KI anayetajwa huenda akarejea Yanga kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, aliondoka katika kikosi hicho, Juni 1, 2025 na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco, kisha kuondoka tena Januari 24, 2026 na kusajiliwa na Al-Ittihad SC ya Libya.

Nyota huyo raia wa Burkina Faso, alijiunga na Yanga Julai 15, 2022, akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambapo alikuwa mchezaji bora wa msimu (MVP), akiwa na kikosi hicho kwa msimu wa 2021-2022 na kuwavutia mabosi wa Jangwani kumsajili.

Wakati kiungo huyo anaondoka Yanga, aliacha rekodi za kuvutia kwa kipindi cha misimu mitatu, baada ya kuchangia mabao 86 kwenye mechi 114 za michuano yote, akifunga mabao 54 na kutoa asisti 32, huku kati ya hayo mabao 39 ni ya Ligi Kuu Bara.

Ndani ya misimu mitatu Aziz KI amebeba makombe tisa na kikosi hicho yakiwemo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya Kombe la CRDB, Ngao ya Jamii mara mbili, huku Kombe la Muungano, Toyota na Mapinduzi yote akichukua mojamoja kwa kila shindano.

Mbali na mataji hayo, ila Aziz KI aliondoka nchini akiwa amebeba tuzo tatu za maana kubwa, ikiwamo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, baada ya kufunga mabao 21, akimzidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC aliyefunga 19.

Mbali na ufungaji bora, ila Aziz KI alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu wa 2023-2024 (MVP) wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuonyesha kiwango kizuri, huku kwa misimu mitatu akifunga hat-trick tano zikiwemo nne za Ligi Kuu na moja ya Kombe la CRDB.

Pia, kiwango kizuri kilichoonyeshwa na Aziz KI, kilimfanya kutwaa Tuzo ya kiungo bora wa Ligi Kuu Bara, katika hafla ya tuzo za msimu wa 2023-2024 zilizotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), akiacha rekodi za kuvutia Yanga.


PACOME ZOUZOUA

Nyota mwingine anayeingia katika kundi hili ni Pacome Zouzoua wa Yanga ambaye naye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, alipoibuka mchezaji bora (MVP) na kikosi hicho kwa msimu wa 2022-2023.

Pacome aliyeanza maisha yake ya soka katika timu ya vijana ya Williamsville Athletic Club ya huko kwao Ivory Coast kisha kujiunga na AC Sparta Prague B ya Jamhuri ya Czech, akiwa na ASEC alifunga mabao saba na kuchangia manne kwa msimu huo.

Msimu huo Pacome aliyechezea timu mbalimbali za, SC Gagnoa, Daugavpils, Africa Sports kabla ya kutua ASEC msimu wa 2021-2022, aliwashinda Aubin Kramo aliyewahi kuichezea Simba na Mohamed Zougrana anayeichezea kwa sasa MC Alger ya Algeria.

Kramo ambaye msimu wa 2026-2027, amejiunga na Singida Black Stars akitokea Ittihad Gharyan SC ya Libya, kwa msimu huo wa 2022-2023, alionyesha kiwango kizuri akiwa ASEC Mimosas na kuivutia Simba kumsajili, japo alishindwa kuwika na kuondoka.

Katika msimu wa kwanza 2023-2024, Pacome alicheza mechi 23 za Ligi Kuu Bara kati ya 30 kwa dakika 1430, akihusika kwenye mabao 11 kufuatia kufunga saba na kuasisti 4, huku msimu wa pili ambao ni wa 2024-2025, alihusika na jumla ya mabao 22.

Msimu wa 2024-2025, alicheza mechi 26, kati ya 30, za Ligi Kuu kwa dakika 1,614 na kuchangia mabao 22, baada ya kufunga 12 na kuasisti 10, akibeba mataji matano ya Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la CRDB.

Kwa msimu wa 2025-2026, Pacome alifunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara na kuasisti manne na kuiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tano mfululizo, huku akichukua pia Ngao ya Jamii 2025 na taji la Kombe la Mapinduzi 2026.


JEAN CHARLES AHOUA

Kwa upande wa Ahoua aliyejiunga na Simba Julai 3, 2024, akitokea Stella Club d’Adjame ya Ivory Coast, alikuwa mchezaji bora wa Ligi ya Ivory Coast msimu wa 2023-2024, baada ya kuhusika na mabao 21, akifunga 12 na kuchangia tisa (Assisti).

Ahoua aliyechezea timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kabla ya kukipiga Stella, alijiunga na CR Belouizdad ya Algeria Januari 22, 2026, baada ya kuitumikia Simba kwa mwaka mmoja na nusu, licha ya kubakisha mkataba wake hadi Juni 30, 2026.

Nyota huyo ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na CR Belouizdad, moja ya rekodi anayokumbukwa nayo zaidi ni ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, kwa kufunga mabao 16, ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu.

Kabla ya Ahoua, mara ya mwisho kwa mchezaji wa Simba aliyechukua ni aliyekuwa kiungo, Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, aliyefunga mabao 17, sawa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga aliyeachana na Pyramids ya Misri, Mkongomani Fiston Mayele.

Msimu wa 2024-2025, Ahoua alichangia mabao 25 kati ya 69, yaliyofungwa na Simba katika Ligi Kuu, baada ya kufunga 16 na kuasisti tisa, huku akiiwezesha kumaliza ya pili na pointi 78, nyuma ya mabingwa watetezi Yanga iliyomaliza na pointi 82.  Kwa msimu wa 2025-2026, kiungo huyo aliondoka Simba akichangia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga moja na kuasisti moja na yote ni katika ushindi wa timu hiyo wa 3-0, dhidi ya Fountain Gate, mechi ikipigwa Septemba 25, 2025.


ALBERT KANGWANDA

Kiungo mshambuliaji, Albert Kangwanda ni miongoni mwa nyota wanaosubiriwa kuonyesha kiwango kizuri kama alivyofanya pia msimu wa 2025-2026, akiwa Red Arrows FC ya kwao Zambia, alipoibuka mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Zambia (MVP).

Katika Ligi Kuu ya Zambia (MTN Super League) msimu wa 2025-2026, Kangwanda alionyesha kiwango kizuri akiwa na Red Arrows FC kwa kufunga mabao 13, japo katika mashindano yote alihusika na mabao yake 25, kufuatia kufunga 17 na kuasisti manane.

Licha ya kiwango bora kwa Kangwanda ila anapaswa kufanya vizuri Yanga, kwani mshambuliaji wa mwisho wa Zambia kuchezea kikosi hicho alikuwa ni Kennedy Musonda aliyeondoka Julai 7, 2025 na kujiunga na Hapoel Ramat Gan Givatayim ya Israeli.

Musonda anayeichezea kwa sasa, Hapoel Nof HaGalil FC ya Israeli pia, alijiunga rasmi na Yanga, Januari 13, 2023, baada ya kuachana na Power Dynamos ya kwao Zambia, ambapo kwa msimu wa 2024-2025, alifunga mabao matatu tu ya Ligi Kuu Bara.

Kwa kipindi cha misimu miwili na nusu alichocheza Yanga, Musonda alifunga jumla ya mabao 10, ya Ligi Kuu, baada ya msimu wa 2022-2023 kufunga mawili tu, kisha msimu wa 2023-2024 akafunga matano na msimu wa 2024-2025, alifunga mabao matatu.

Hata hivyo, rekodi hizo za Musonda zilimfanya mshambuliaji huyo kushindwa kuwika na Yanga na sasa Kangwanda ni moja ya usajili bora kutokana na kiwango chake alichoonyesha msimu wa 2025-2026, akitakiwa kupambana ili kutoa jinamizi hilo.

Mbali na kutakiwa kupambana ili kutoa jinamizi hilo baya, ila anapaswa kuonyesha kiwango bora na kufuata viwango vizuri vilivyoonyeshwa na Aziz KI, Pacome na Ahoua waliokuja wakitoka kushinda Tuzo ya MVP na kuendelea kufanya mambo makubwa.

Licha ya kucheza Red Arrows FC, ila Kangwanda ana uzoefu wa kucheza pia timu mbalimbali zikiwemo za Zanaco FC na Kafue Celtic FC zote za kwao Zambia, HNK Gorica ya Croatia, Al-Hilal Omdurman ya Sudan na CSF Spartanii Sportul ya Moldova.