Pesa imetumika kulipa makocha wa kufutwa kazi
Muktasari:
- Jambo hilo lilimfanya kuwa kocha wa tatu kufutwa kazi kwenye Ligi Kuu England na alikuwa wa pili kwenye kikosi cha Forest licha ya kwamba kwa wakati huo timu hiyo ilikuwa imecheza mechi nane tu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Ange Postecoglou alifutwa kazi Nottingham Forest baada ya muda usiozidi dakika 20 tangu kikosi hicho kilipochapwa 3-0 Chelsea.
Jambo hilo lilimfanya kuwa kocha wa tatu kufutwa kazi kwenye Ligi Kuu England na alikuwa wa pili kwenye kikosi cha Forest licha ya kwamba kwa wakati huo timu hiyo ilikuwa imecheza mechi nane tu.
Tajiri mmiliki wa Forest, Evangelos Marinakis, ambaye aliwahi kutibuana na kocha Nuno Espirito Santo, ambaye kwa sasa anainoa West Ham United, aliamua kumfuta kazi Postecoglou baada ya kuiongoza timu hiyo kwa siku 39.
Mambo ni moto kwenye Ligi Kuu England. Lakini, wakati klabu zikiamua kuwapiga vibuti makocha wake, jambo hilo limekuwa likiwaingiza kwenye matumizi ya ziada ya pesa ambazo wanazitumia kwenye kuwalipa fidia makocha hao kwa kuvunja mikataba yao.
Kutokana na hilo, hizi hapa klabu za Ligi Kuu England, ambazo zimetumia pesa nyingi kulipa fidia makocha iliyowafukuza kazi na kufanya pesa hizo kuingia kwenye hesabu zao za matumizi.
1. Chelsea - Pauni 40milioni
Miamba hiyo ya Stamford Bridge ndiyo iliyotumia pesa nyingi kwenye kulipa fidia ya kuvunja mikataba ya makocha wake, ilipofanya hivyo kwa Frank Lampard, Thomas Tuchel, Graham Potter, Mauricio Pochettino kwa miaka ya karibuni, bila ya kuwahusisha makocha wengine kama Jose Mourinho.
Lampard alilipwa Pauni 2 milioni, Tuchel (Pauni 15milioni), Potter alilipwa Pauni 21.5 milioni, wakati Pochettino alilipwa Pauni 10 milioni.
2. Tottenham - Pauni 38 milioni
Katika zama za Daniel Levy, Spurs ilifanya mabadiliko ya makocha kadhaa katika kikosi chake, huku ikilazimika kuwalipa fidia wale iliyowafukuza. Mourinho alipofutwa kazi alilipwa Pauni 16 milioni, wakati Nuno Espirito Santo aliweka kibindoni Pauni 14 milioni.
Antonio Conte, naye aliwahi kuinoa timu hiyo na alipofutwa kazi, alilipwa Pauni 25 milioni, huko Postecoglou alilipwa fidia ya Pauni 4 milioni.
3. Man United - Pauni 24.5 milioni
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Manchester United imewafuta kazi makocha Ole Gunnar Solskjaer na Erik ten Hag na kuwaingiza kwenye gharama kubwa za kuvunja mikataba yao.
Wakati Man United inamfuta kazi kocha, Solskjaer ilimlipa fidia ya Pauni 10 milioni, wakati Mdachi Ten Hag, alipoonyeshwa mlango wa kutokea huko Old Trafford, alilipwa fidia ya Pauni 14.5 milioni.
4. Everton - Pauni 20.6 milioni
Makocha Carlo Ancelotti, Rafael Benitez, Frank Lampard na Sean Dyche ni miongoni mwa waliowahi kuingia kwenye rekodi ya kuonyeshwa mlango wa kutokea wakati alipofanya kazi Goodison Park na jambo hilo liiingiza timu hiyo kwenye hasara kubwa ya kulipa fidia, huku nusu ya pesa hiyo ililipwa kwa Benitez, Pauni 10.5 milioni. Lampard aliweka kibindoni Pauni 7.1 milioni.
5. Wolves - Pauni 13.5 milioni
Makocha Nuno Espirito Santo, Bruno Lage, Julen Lopetegui na Gary O’Neil, wameingia kwenye rekodi ya kufutwa kazi huko Wolves na kuifanya timu hiyo kuwa miongoni mwa klabu zilizotumia pesa nyingi kwenye kulipa fidia ya kuvuta makocha wake kwenye Ligi Kuu England.
Mgawo huo wa fidia, haukuwa wa pesa za kutosjha kwa kocha mmoja, lakini kiwango cha jumla kimeifanya Wolves kuwa kwenye orodha ya timu hiyo.
Timu nyingine zilizotumia pesa nyingi kulipa fidia za makocha iliyowafuta kazi ni Nottingham Forest, Pauni 10.5 milioni, West Ham United, Pauni 8.5 milioni, Newcastle United, Pauni 8 milioni, Aston Villa, Pauni 7 milioni na Leeds United, Pauni 6.5 milioni.