Vipaji Zanzibar vyateka Simba, Yanga, Azam
Muktasari:
- Ukitofautisha zamani na sasa ambapo klabu hizo zinachukua idadi kubwa ya wachezaji kutoka Zanzibar, hususan Yanga ambayo kwa sasa ina wengi, pamoja na hilo siyo wote wanaopata nafasi kubwa ya kucheza kwa mafanikio.
KASI za klabu za Simba, Yanga na Azam FC kuweka nguvu kusajili wachezaji wazawa kutoka Tanzania Visiwani kwa miaka ya hivi karibuni, inaweza ikapunguza idadi kubwa ya nyota wanaotoka Bara kupata nafasi katika timu hizo.
Ukitofautisha zamani na sasa ambapo klabu hizo zinachukua idadi kubwa ya wachezaji kutoka Zanzibar, hususan Yanga ambayo kwa sasa ina wengi, pamoja na hilo siyo wote wanaopata nafasi kubwa ya kucheza kwa mafanikio.
Mwanaspoti linakuchambulia sababu ya timu hizo kwenda Zanzibar kusaka vipaji hivyo,jambo ambalo linaweza likawaweka katika wakati mgumu wachezaji wanaotoka Tanzania Bara kupata nafasi kubwa katika timu hizo.
MISINGI WALIYOLELEWA
Wachezaji wa Zanzibar wanalelewa katika misingi sahihi ya soka, jambo linalofanya vipaji vyao wawapo uwanjani kuonekana ni vya mvuto na vya kipekee hasa kwa kucheza soka la kufundishwa na siyo kipaji pekee.
Miongoni mwa mashuhuda wa hilo ni kocha msaidizi wa viungo wa klabu ya Simba, Mohammed Mrishona ‘Coach Xavi’ anasema kuna hatua ya ukuaji wa mchezaji hadi kucheza timu kubwa.
“Kwa Zanzibar hadi mchezaji afikie hatua ya kucheza Ligi Kuu, anapitia hatua zote za ukuaji kuanzia utoto wake, hizo zinawajengea kucheza soka la kufundishwa, kwa sababu kila umri wa wachezaji kuanzia wakiwa wadogo kuna mashindano yake,” anasema.
HAWANA GHARAMA
Ingawa Zanzibar kuna vipaji vikubwa, lakini kukosekana kwa wadhamini kunafanya vipato vya wachezaji hao kuwa chini, hivyo wanapokuja kucheza Bara, inakuwa ni njia yao ya kufanikiwa kiuchumi.
Mshambuliaji wa Mbeya City, Matheo Anton anayetokea Zanzibar anasema:”Kama unacheza soka la Zanzibar bila kufanya kazi nyingine ni ngumu kufanikiwa, binafsi nilikuwa nafanya kazi ya ukondakta huku nikiwa nacheza, maisha yangu yalianza kubadilika kwa mara ya kwanza baada ya kuanza kuichezea Yanga, kisha nikaenda Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, KMC na JKT Tanzania.”
Mchezaji mwingine kutoka Zanzibar ni golikipa wa Simba, Yakoub Suleiman aliwahi kusema: “Ingawa nje ya soka mimi ni askari, lakini ukicheza Zanzibar, soka pekee haliwezi kubadilisha maisha, tukija Bara tunaona matunda ya soka, kwani kuna pesa.”
Mwingine aliyekiri hilo ni katibu wa JKU, Dhadhil Khatib anasema: “Mara nyingi wachezaji wanapotoka Zanzibar kwenda kucheza Bara, wanakuwa na mafanikio makubwa kiuchumi, kwani soka la Bara lina udhamini pia lipo juu zaidi kutokana na linavyotangazwa na inaweza ikawa rahisi kwa wachezaji kwenda nje.”
VIUNGO, MABEKI
Ni nadra timu za Bara kusajili washambuliaji, asilimia kubwa wengi wao ni viungo, mabeki na makipa ukiondoa baadhi yao wanaocheza nafasi za mbele kama Anton, Mohamed Mussa ambaye kwa mara ya kwanza alisajiliwa na Simba Januari, 2023 kutoka Malindi ya Zanzibar, kisha ikaachana naye.
Ukiachana na hao kuna mshambuliaji wa Pamba Jiji, Saleh Karabaka ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao manane JKT Tanzania pia alipita kwa Wanamsimbazi kutokea JKU ya Zanzibar, mwingine ni Nassor Saaduni wa Azam.
Anachosema kocha wa Zimamoto ya Zanzibar, Abdallah Mohammed “Bares” kuhusiana na hilo: “Zanzibar ina vipaji vya hali ya juu ambavyo vimejengwa katika misingi sahihi ya kisoka ndio maana unaona viungo vingi, kutokana na kufundishwa ufundi, ingawa hata washambuliaji wapo.
Anaongeza kuwa, “Bara kwa sasa imeanza kuona kwa ukubwa vipaji vilivyopo Zanzibar ndiyo maana unaweza ukaona katika klabu ya Yanga wapo saba, hilo linatia moyo sana, kuhusu wadhamini angalau kwa sasa kuna nafuu kidogo kwa mdhamini aliyepo kama sikosei ana misimu mitatu na anazidi kuongeza pesa, huko mbele na sisi tutakuwa vizuri kiuchumi katika soka.”
YANGA
Ndani ya kikosi cha Yanga kuna wachezaji Ibrahim Abdullah hamad ‘Bacca’(beki wa kati), Mudathir Yahya Abbas (kiungo),
Shekhan Ibrahim Khamis(kiungo) katolewa kwa mkopo kwenda Singida BS, Abdulnasir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’ (kiungo)
Aboubakar Nidhar Othman ‘Ninju’ (kiungo mkabaji), Muham med Mussa Jecha (beki) na Abdulnasir Assa Muhammed ‘Gamal’ (beki).
Ukiachana na hao kuna wengi walitangulia mbele yao baadhi yao ni aliyekuwa beki na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,(beki) Haji Mwinyi (beki) Juma Makapu (kiungo), Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (beki).
SIMBA
Simba ukiondoa waliyowasajili hivi karibuni kama Karabaka(mshambuliaji), Mussa (mshambuliaji) na miaka ya nyuma kidogo alikuwepo aliyekuwa nahodha na beki Nassor Masoud ‘Chollo’, kiungo Abdulhalim Humoud, lakini kwa sasa yupo golikipa Yakoub Suleiman.
AZAM FC
Katika kikosi cha Azam FC kuna nyota anayetamaniwa na klabu mbalimbali ndani na nje, kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye amekuwa akifanya vizuri, tangu akiwa na Yanga, staa huyo anayetajwa kila kona msimu uliopita wa 2025/26 alifunga mabao 15,asisti tisa , 2024/25 mabao manne, kinara wa asisti 13 na 2023/24 mabao 19, asisti saba, mwingine ni Saadun.
Ukiondoa hao wapo ambao waliichezea Azam na walishaondoka baadhi yao ni kipa Ahmed Salula na beki Abdalla Salum Kheri.