Nyota 10 waliopo sokoni NBA
Muktasari:
- Licha ya kuwa nyota wakubwa tayari wamesaini mikataba mapema mwezi Julai, bado kuna wachezaji wachache waliobaki sokoni ambao wana mvuto na uwezo wa kuongeza thamani kubwa katika vikosi vya timu mbalimbali msimu ujao.
LAS VEGAS, MAREKANI: SOKO la wachezaji huru katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) linaelekea ukingoni huku shughuli nyingi za uhamisho zikitarajiwa kupungua kwa kasi kabla ya timu na viongozi wake kwenda mapumzikoni.
Licha ya kuwa nyota wakubwa tayari wamesaini mikataba mapema mwezi Julai, bado kuna wachezaji wachache waliobaki sokoni ambao wana mvuto na uwezo wa kuongeza thamani kubwa katika vikosi vya timu mbalimbali msimu ujao.
Hawa siyo tena wale wachezaji wa kiwango cha juu kama LeBron James au Jayson Tatum, bali ni mchanganyiko wa wachezaji waliobobea, waliopitia klabu nyingi, waliorejea kutoka majeruhi, wazoefu wanaotafuta nafasi ya mwisho, pamoja na wale walio chini ya masharti ya “restricted free agent” ambao bado hawajafikia makubaliano na timu zao.
1. Malcolm Brogdon – Umri: 32
Malcolm Brogdon bado ana thamani kubwa sokoni, hasa kwa timu zinazotafuta kiongozi wa wachezaji wa benchi au point guard wa akiba. Akiwa amecheza msimu uliopita na Washington Wizards, Brogdon alionyesha kiwango kizuri kwa kufunga wastani wa pointi 12.7 na kutoa pasi 4 kwa mchezo. Uongozi wake uwanjani na uamuzi wake vinamfanya kuwa chaguo la kuvutia kwa timu zinazotaka wachezaji waliokomaa na wenye utulivu.
2. Josh Giddey (Huru)
Giddey bado hajaafikiana na Chicago Bulls wala kupata ofa ya maana kutoka timu nyingine, jambo linaloashiria kuwa huenda Bulls wana mpango wa kumrudisha kwa kuoanisha ofa yoyote itakayowasilishwa. Msimu uliopita, Giddey alifunga wastani wa pointi 14, rebound 8 na asisti 7, akionyesha uwezo mkubwa wa kuwa mchezaji anayeweza kucheza nafasi nyingi (versatile). Kinachozuia uhamisho wake ni dau kubwa analotaka, linalokadiriwa kuwa takribani dola 30 milioni kwa msimu. Hii ni vita ya soko kati ya thamani anayojiona nayo na uhalisia wa bajeti za timu.
3. Quentin Grimes
Grimes aliondoka Dallas Mavericks kimya kimya, lakini alipowasili Philadelphia alibadilika kuwa mshambuliaji wa uhakika, akifunga wastani wa pointi 21.9 kwa mchezo. Mabadiliko haya yalizua maswali mengi juu ya uamuzi wa Dallas kumuachia, hasa ukizingatia walikuwa na upungufu wa watu wa safu ya nyuma. Kama restricted free agent, thamani yake sokoni imeongezeka, japokuwa ana muda mfupi tu wa kuonyesha kiwango hicho. Timu zitahitaji kumtathmini kwa umakini kabla ya kumwekea dau.
4. Al Horford – Umri: 38
Mchezaji mkongwe, lakini bado ni wa msaada mkubwa hasa kwa timu zinazotafuta ‘stretch big man’ yani yule anayejua kucheza ndani na nje ya paint. Baada ya Celtics kuachana naye kwa sababu ya mshahara mkubwa, Horford sasa anazingatia zaidi familia na utulivu kuliko fedha.
Warriors wameonyesha nia, lakini umbali wa San Francisco kutoka Boston au Miami huenda ukawa kikwazo. Uwezo wake wa kuongoza wachezaji chipukizi na uzoefu wa michezo mikubwa ni hazina isiyopaswa kupuuzwa.
5. Jonathan Kuminga (Huru)
Kuminga bado ni chipukizi mwenye uwezo mkubwa wa kukua na kuwa nyota. Lakini nafasi yake ndani ya kikosi cha Golden State Warriors bado ni ya shaka, jambo linalomsukuma kutamani kuondoka. Hakuna timu iliyoleta ofa kubwa ya kumsaini moja kwa moja, na hilo linaweza kumlazimu kusubiri “sign-and-trade” au kubaki kwa msimu mmoja zaidi kabla ya kuingia sokoni tena. Hii ni vita kati ya matarajio yake binafsi na uhalisia wa matumizi ya Warriors.
6. Damian Lillard – Umri: 35
Dame hatacheza msimu wa 2025-26 kutokana na jeraha la tendon ya Achilles na anatarajiwa kurudi akiwa na umri wa miaka 36. Lakini jina lake bado lina mvuto mkubwa katika soko. Hivi sasa hana haraka ya kusaini kokote, akielekeza zaidi kwenye maisha ya familia. Baada ya miaka mingi ya kushindwa kutwaa taji la NBA, Lillard anaweza kuchukua muda kuchagua kwa makini timu anayotaka kujiunga nayo kabla ya kustaafu. Mchezaji mwenye njaa ya mafanikio na uzoefu.
7. Chris Paul – Umri: 40
Hajachoka bado. Alicheza mechi zote 82 msimu uliopita akiwa na Spurs na bado ana uwezo wa kuwa point guard wa akiba mwenye ushawishi mkubwa. CP3 tayari amejikusanyia utajiri mkubwa na kwa sasa anatafuta timu iliyoko karibu na familia yake. Dalili zote zinaonyesha kuwa atajiunga na mojawapo ya timu za Los Angeles iwe Clippers au Lakers. Wengi wangependa kuona Paul akirejea Clippers, mahali alipowahi kuipandisha hadhi klabu hiyo kwa kiwango kikubwa.
8. Gary Payton II – Umri: 32
Anajulikana kwa uwezo wake wa kulinda, huo ni urithi kutoka kwa baba yake Gary Payton (The Glove). Payton II amepitia majeraha lakini bado ana nguvu, anaweza kuruka na kutoa ulinzi wa kiwango cha juu kwenye perimeter. Kwa sasa, Warriors hawana mpango wa kumbakisha, lakini timu nyingine zitamnyemelea kwa kuwa ni chaguo la uhakika kwa bajeti ya kawaida. Alilipwa dola 9 milioni msimu uliopita, na anaweza kukubali mkataba wa thamani hiyo au chini kidogo. Ni suala la muda tu.
9. Cam Thomas – (Huru)
Akiwa na wastani wa pointi 24 kwa mchezo msimu uliopita, Thomas ni mfungaji halisi. Lakini bado hajafikia makubaliano na Brooklyn Nets, kwani inadaiwa yapo mapishano makubwa ya malipo kati ya pande mbili. Akiwa na umri mdogo na uwezo wa kufunga kutoka kona yoyote ya uwanja, Thomas ni lulu inayosubiri tu kupokewa na timu yenye bajeti nzuri na mpango wa kumjenga kama nyota wa siku zijazo.
10. Russell Westbrook – Umri: 36
Westbrook ni mmoja wa wachezaji waliokuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa miaka mingi, lakini sasa hali imebadilika. Alicheza kwa Lakers, Clippers na Denver Nuggets katika miaka mitatu iliyopita, lakini hakuna hata moja iliyomrudisha. Changamoto kwake ni kushindwa kuwa na ufanisi mzuri katika kutumia nafasi za mitupo ya mbali.