NIONAVYO: Weledi ni muhimu katika usimamizi wa wanamichezo
DUNIA ya leo inabadilika kila uchao. Hapo zamani motokaa ilikuwa inatengenezwa na kukamilika katika kiwanda kimoja kiwe ni cha Ford Motors, General Motors na kadhalika. Gari lilitoka kiwandani likiwa limekamilika kwa kazi ya kiwanda hicho. Sasa hivi vipande mbalimbali vya gari hutengenezwa sehemu mbalimbali duniani na kisha kuweza kuunganishwa na kampuni husika mmoja.
Mwanamichezo wa kisasa ni kama mfano wa motokaa ya kisasa; analelewa na watu tofauti kwa malengo tofauti. Katika nchi zilizoendelea mwanamichezo atakuwa na mtaalamu wa lishe, mtaalamu wa saikolojia, mtaalamu wa mawasiliano na uhusiano na jamii n.k.
Pamoja na mengi ya mahitaji haya kutolewa na klabu bado wachezaji binafsi huajiri wasaidizi binafsi kwa ajili ya kuwashauri katika masuala mbalimbali kama utunzaji wa fedha na uwekezaji.
Wanamichezo wana wasimamizi kwa ajili ya kuwalea, kuwaendeleza, kuwaelekeza na kusimamia maslahi yao.
Tumekuwa na kawaida ya kusema mwanamichezo fulani ana kipaji hivyo anaweza kuendelea hata bila kusimamiwa. Hilo si kweli; hata Lionel Messi na kipaji chake kikubwa asingeweza kufika alikofika kama si kupelekwa Hispania ambako alianza kulelewa na wazazi na klabu ya Barcelona na pia kuendelezwa na kuelekezwa na wataalam wa kule Hispania. Usimamizi ni muhimu.
Mwanamichezo anapokuwa mdogo anaweza kulelewa na wazazi, walimu au ndugu zake ili abaki kwenye misingi na nidhamu ya mchezo anaoupenda au ambao ana kipaji chake. Hapa atafundishwa kufanya mazoezi na mbinu nyepesi zinazohusu mchezo huo. Kwa mazingira ya kwetu hili jukumu walimu wa shule na wazazi wanaweza kulimudu hivyo halihitaji mtu kuwa milionea ili kulea kipaji cha mtoto au mwanafunzi wake. Usimamizi ni muhimu.
Kadri anavyokua, malezi, mafundisho na maelekezo yanaanza kuhitaji uelewa na weledi zaidi. Hapa mwanamichezo huhitaji kuangaliwa mbinu na nidhamu yake ya kimichezo pia mwanamichezo huhitaji kuanza kutambua nafasi yake katika jamii na namna ya kutunza taswira yake.
Mfano tuna vijana katika soka ambao wanakuwa na mitindo ya mavazi au hata nywele ambayo wameiokota kwenye runinga bila ya kujua maana yake. Mchezaji anafunga bao, anaonyesha ndani fulana yenye maandishi ambayo si mazuri kwake na kwa jamii; anaharibu taswira yake na taswira ya timu. Kumbe angekuwa na mtu wa karibu wa kumshauri hilo lisingetokea.
Kadhalika, mwanamichezo anatakiwa kuwa na watu wanaoangalia anachoandika au kutolea maoni mtandaoni. Cristiano Ronaldo alipopata mtoto iliwachukua muda wasaidizi wake wakifikiria namna nzuri na mtandao upi wautumie kuutaarifu umma kuhusu tukio hili. Wanajua maisha binafsi ya mchezaji yanagusa pia hisia na mtazamo wa umma, na mtazamo wa umma una nafasi katika maendeleo na thamani ya mchezaji. Sio rahisi kwa mchezaji wa Bongo kuwa na utitiri wa wataalam wa mitandao lakini inawezekana kuwa na washauri au wanafamilia ambao wana uelewa wa nafasi ya mwanamichezo katika jamii na wakaweza kumsaidia katika mambo yake. Usimamizi ni muhimu.
Tumeshuhudia mara nyingi ikitokea migogoro kati ya wanamichezo na waajiri au wadhamini. Mara nyingi, hasa kwetu imetokana na wanamichezo kuwa na haraka au kukubali presha ya kusaini mkataba kabla ya kuelewa kilichomo ndani ya mkataba. Kwa uzoefu wangu wa kuingia mikataba ya wachezaji na klabu, nakumbuka eneo la ubishi mara nyingi huwa ni kipengele cha pesa hata kama mkataba una zaidi ya vipengele 20. Mkataba unaweza kuwa na vipengele 19 vibaya, lakini mwanamichezo kwa kutoelewa au kwa kutopata usimamizi mzuri akasaini mkataba huo kwa kuridhika na fedha tu. Usishangae mwanamichezo anaweza kusaini mkataba ulioandikwa kwa lugha ya Kireno bila ya kuwa na mwanasheria au mkalimani wa lugha hiyo asiyoielewa kwa ufasaha. Matokeo yake, mchezaji anaweza kutumiwa kinyume cha matakwa yake, akacheza akiwa na msongo wa mawazo na kushindwa kufikia malengo aliyokusudia. Tuliwahi kufanya mazungumzo ya kumsajili mchezaji Kelvin Yondani zaidi ya mwongo mmoja uliopita nyuma. Yondani hakuwahi kuja ofisini kwangu peke yake. Hakuwahi kuja na mwanasheria. Alikuwa akija na kaka yake na kamwe hawakukubali kuongea na mtu yeyote akiwa peke yake. Kama kaka yake hakuwepo, basi siku hiyo hakuna biashara iliyokuwepo. Kuwepo kwa kaka kulikuwa kunamuondolea mchezaji msongo wa kushughulika na masuala ya ajira. Kamwe hakutoka nje ya mstari huo wa kinidhamu aliojiwekea. Hakuwa na fedha nyingi, lakini alijua umuhimu wa kuwa na msimamizi. Usimamizi ni muhimu.
Utunzaji wa fedha na uwekezaji pia ni sehemu ambayo wanamichezo wana mahitaji ya ushauri. Uzoefu wa hapa ndani na dunia kwa ujumla unaonyesha kuwa wanamichezo ambao hawana familia au washauri wazuri kwa mambo ya mapato, matumizi na uwekezaji huwa na mwisho mbaya wa maisha yao. Si vema kuwataja hapa lakini orodha ni ndefu kutoka kwa Mike Tyson, Frank Bruno hadi Diego Maradona. Umri na muda wa kucheza ni mfupi sana, lakini gharama yake ni kubwa hivyo ni muhimu sana kwa wanamichezo kuwa na washauri katika masuala mbalimbali hili muda mfupi wa kucheza uwe na faida mpaka uzeeni mwao.
Mwanamichezo na hasa wachezaji wetu wanaoibukia wasisubiri kuanza kukamua mamilioni ya fedha ndiyo waanze kutafuta wasimamizi. Familia, shule, klabu na wote wanaomzunguka mwanamichezo wana nafasi muhimu katika kumjengea mwanamichezo utamaduni wa kutafuta ushauri na usimamizi utakaomkuza na kumfanya awe bora na kuwa na maisha bora pia baada ya kuacha kucheza. Usimamizi ni muhimu.
Miaka ya kutumika kama mchezaji si mingi, ni kati ya miaka 15 hadi 20 kwa walio na bahati ya kubaki kwenye kiwango, kujitunza na kuepuka majeraha. Miaka hiyo michache ikitumika vizuri inaweza kuwa nguzo ya maisha bora ya mchezaji katika kipindi chote cha uchezaji na hata baada ya kutundika daruga. Kesho inatengenezwa na maono na matendo ya leo.
Mwandishi wa makala hii ni mzoefu katika miradi ya maendeleo, utawala na biashara katika michezo na nyanja nyingine. Ametumikia nyadhifa mbalimbali katika vilabu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), CAF na FIFA. Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.