Sifa muhimu zinazomjenga Mwanasoka wa kisasa
Muktasari:
- Siyo kila mchezaji atanunuliwa na kupewa mkataba tu, bali inahitajika kuwa na vitu kadhaa ambavyo soka la kisasa linavihitaji kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa wa soka duniani.
KATIKA medani ya soka hivi sasa kumepoa, huku klabu nyingi duniani, ikiwamo za hapa nchini, zikiwa katika hekaheka za usajili wa wachezaji wapya wanaotarajiwa kuwa katika viwango bora.
Siyo kila mchezaji atanunuliwa na kupewa mkataba tu, bali inahitajika kuwa na vitu kadhaa ambavyo soka la kisasa linavihitaji kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa wa soka duniani.
Utendaji kazi na utimamu wa mwanasoka uwanjani hutegemea mchanganyiko wa mambo mbalimbali, ikiwamo ukakamavu na uvumilivu, kasi na wepesi, nguvu na ustahimilivu pamoja na kunyumbulika.
Mafunzo thabiti na mchanganyiko wa mazoezi ya nguvu, mazoezi ya kuimarisha mfumo wa upumuaji, moyo na mishipa ya damu, misuli na mifupa ni muhimu kwa utendaji kazi na kuzuia majeraha ya michezo.
Kuimarika kwa kandanda si tu kufanya vyema siku ya mechi, bali ni kuhusu kujenga msingi wa kimwili unaowaruhusu wachezaji kufanya vyema ndani ya klabu na katika timu ya taifa bila kuchoka.
Katika viwango vya juu zaidi vya uchezaji, utendaji wa mchezaji huendeshwa na mbinu sahihi za mafunzo na mazoezi yaliyoegemezwa kisayansi, chini ya usimamizi wa walimu wenye weledi.
Leo tutapata ufahamu kuhusu mambo hayo yanayochangia uwezo wa juu wa wachezaji, hatimaye kutimiza majukumu mengi bila kuchoka wala kupata majeraha ya mara kwa mara.
UKAKAMAVU NA UVUMILIVU
Ukakamavu na nguvu humwezesha mchezaji kutawala kimwili huku akipunguza hatari za majeraha yatokanayo na michezo, ikiwamo kuchanika kwa misuli.
Kuboresha ukakamavu wa mchezaji ni kufanya mazoezi yatakayoyaimarisha makundi mbalimbali ya misuli mwilini. Mazoezi ya nguvu kuu ni pamoja na kuchuchumaa, kunyanyua na kupumua.
Mwili mkakamavu ndio wenye uwezo wa juu wa kucheza muda mrefu, kuvumilia pale unapojeruhiwa au kutoumia kirahisi na kuwa na uwezo wa kupona haraka wakati wa majeraha.
KASI NA WEPESI
Kandanda huchezwa kwa kasi ya juu, huku kukiwa na mabadiliko ya haraka kutoka kwenye kujilinda hadi kushambulia, mashambulizi ya nguvu na kasi, pamoja na kukimbia kwa kasi ili kuufikia mpira kwanza.
Kukimbia na kuongeza kasi ni miongoni mwa faida muhimu zaidi ambazo mchezaji anaweza kuwa nazo, pamoja na uwezo wa kukabiliana haraka na mabadiliko ya hali uwanjani.
Kuboresha kasi kunahitaji mseto wa mafunzo ya kiufundi, nguvu za juu zaidi pamoja na mazoezi ya mbio yaliyopangwa kwa uangalifu, ikiwamo kuchomoka pale inapohitajika.
Mazoezi ya kuongeza kasi yanaweza kuboreshwa kwa kutumia vifaa na mitambo maalumu inayowezesha kasi ya mchezaji. Ni mara chache wachezaji hufikia kasi yao ya juu zaidi, lakini hukimbia mara kwa mara kwa milipuko mifupi wawapo uwanjani.
Wakati wepesi ni uwezo wa kubadilisha mwelekeo haraka, jambo hili ni muhimu kwa kila nafasi katika soka, ikiwamo makipa na walinzi. Huwapa uwezo wa kuwakabili washambuliaji na viungo wenye sifa nzuri ya wepesi.
Wepesi huwaruhusu wachezaji kudumu muda mrefu na kufanya kazi kwa ufanisi wakati wa uchezaji wa kasi huku wakilinda lango lao na kushambulia bila kuchoka. Kuboresha wepesi kunahusisha mafunzo ya uratibu wa neva, misuli na maungio. Hufanyika kwa mazoezi ya uwanjani pamoja na yale binafsi ya nyongeza yanayofundishwa na wakufunzi binafsi (special trainer).
NGUVU NA USTAHIMILIVU
Nguvu ya mchezaji wa kandanda ni uwezo wa kuchanganya nguvu na kasi ili kufanya harakati za kuchomoka kwa nguvu, kunyumbulika bila kupoteza mwelekeo na kukaba kwa nguvu.
Nguvu ni uwezo wa kuzalisha nishati haraka kwa kuchanganya ustahimilivu na kasi. Wachezaji wa kandanda wanahitaji nguvu nyingi ili kuharakisha utendaji kazi, kuruka au kufanya mabadiliko ya haraka.
Mafunzo ya nguvu katika soka yanahusisha mazoezi yanayobadilika na ya kulipuka ambayo huchochea nyuzi za misuli ili kupata nguvu na kufunguka kwa ufanisi.
Kandanda ni mchezo unaohitaji ustahimilivu mkubwa. Mara nyingi wachezaji hukimbia umbali wa kati ya kilomita 10 hadi 13 katika kila mchezo na wanahitaji kudumisha viwango vya uchezaji kwa muda wote wa mechi.
Kuboresha ustahimilivu wa mchezaji kunahitaji mafunzo ya uvumilivu ambayo lazima yaakisi mahitaji ya mechi za soka. Mchanganyiko wa mazoezi mepesi (aerobics) na magumu (anaerobics) ni msingi wa ustahimilivu.
KUHAMA, KUNYUMBILIKA
Uhamaji au kunyumbulika huhakikisha kuwa wachezaji wanaweza kupitia safu kamili ya mwendo bila vizuizi, jambo linaloimarisha utendaji na kupunguza hatari ya kuumia.
Kukaza katika sehemu muhimu kama nyonga au vifundo vya miguu kunaweza kupunguza uwezo wa mchezaji kukimbia, kunyumbulika, kubadilisha mwelekeo au hata kupiga mashuti kwa ufasaha.
Kuboresha uhamaji wa mchezaji kunahitaji mazoezi ya kupasha mwili na kunyoosha viungo kwa nguvu. Pia inahitajika kuzingatia mazoezi lainishi ya uponaji mara baada ya mazoezi au mechi.
Mazoezi yanayotegemea nguvu na mwendo huuwezesha mwili kufikia mwendo kamili kupitia viungo, misuli na tishu unganishi.
Mazoezi yanayolenga nyonga, vifundo vya miguu na uti wa mgongo wa kifua lazima yawe sehemu ya utaratibu wa kila mwanasoka.
SIFA ZA ZIADA KIMWILI, KIAKILI
Uimara na uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu kwa dakika 90 hutokana na utendaji bora wa mifumo 11 ya mwili, ikiwamo moyo, damu na mishipa ya damu, mfumo wa upumuaji, fahamu, misuli na mifupa.
Vilevile, pamoja na sifa za kisaikolojia na kiakili, uratibu sahihi wa mazoezi, lishe na mapumziko ni muhimu. Ulinzi wa afya ya mchezaji ni jambo la msingi katika kulinda mifumo ya mwili.
Mchanganyiko huu huwaruhusu wachezaji kudumisha nguvu katika mchezo wote, kufanya ujuzi kwa usahihi na kupunguza hatari ya kuumia.
Ujuzi wa kiufundi na akili, uwezo wa kudhibiti mpira, kupiga pasi, kupiga chenga na kufunga kwa usahihi chini ya shinikizo ni muhimu kwa timu. Mchezaji mwenye utulivu wa kiakili ni rahisi kufanikisha haya. Ujuzi wa mbinu, kuelewa mchezo, kufanya maamuzi ya busara na kujiweka vyema uwanjani vinahitaji utulivu wa hisia, kisaikolojia na akili. Uelewa wa maelekezo ya walimu ndio huleta matokeo chanya.
CHUKUA HII
Utendaji kazi na utimamu wa mwanasoka unaweza kubebwa pia na faida ya kuwa na vina vya urithi vinavyoweza kujenga mwili wenye ustahimilivu dhidi ya majeraha na uponaji wa haraka pale anapopata majeraha.