Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga kwenye mtego huu CAF


SAFARI ya kutafuta utawala mpya wa soka la klabu barani Afrika inaanza rasmi Alhamisi, Agosti 6, 2026, wakati Shirikisho la Soka Afrika (CAF) litakapofanya droo ya hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika katika makao yake makuu jijini Cairo, Misri.


Ni droo ambayo itafungua rasmi pazia la msimu wa 2026-2027 wa mashindano ya klabu Afrika, huku zaidi ya timu 120 kutoka mataifa mbalimbali ya bara hilo zikisubiri kujua safari yao itaanzia wapi na dhidi ya nani.

Kwa Tanzania, macho yote yataelekezwa Cairo wakati wawakilishi wake watakapofahamu wapinzani wao katika harakati za kutafuta mafanikio mapya kwenye soka la Afrika.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itawakilishwa na mabingwa wa Ligi Kuu, Yanga pamoja na mabingwa wa Kombe la CRDB, Simba SC, huku Azam FC na Singida Black Stars wakiipeperusha bendera ya nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Zanzibar, KVZ imefuzu Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwa bingwa wa ligi kuu, wakati KMKM itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikibeba Kombe la FA.

CAF imepanga droo mbili tofauti siku hiyo ambapo droo ya Kombe la Shirikisho itaanza saa 9:00 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, kabla ya kufuatiwa na droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika saa 10:00 jioni.

Kwa klabu zote zinazoshiriki, hii ni hatua inayoweza kuamua ukubwa wa mlima zitakaopanda kuelekea hatua ya makundi.

Kupata mpinzani mwenye uzoefu mdogo kunaweza kurahisisha safari ya kufika hatua inayofuata, lakini kukutana mapema na vigogo wa Afrika kunaweza kufanya ndoto za baadhi ya timu kufifia kabla hata ya mashindano kuingia hatua ya makundi.

WABABE WATAWALA DROO

Msimu huu unatarajiwa kuwa mmoja wa misimu yenye ushindani mkubwa zaidi kutokana na mkusanyiko wa klabu zenye historia kubwa pamoja na zile zinazoinukia kwa kasi.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutakuwa na majina makubwa kama Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates, Zamalek, Pyramids FC, TP Mazembe, Esperance de Tunis, Club Africain, MC Alger, ASEC Mimosas na Petro de Luanda.

Pia kutakuwepo RS Berkane, Djoliba AC, Stade Malien, Gor Mahia, Medeama SC, Horoya AC, Rivers United, FC Nouadhibou, Vipers SC, APR FC, Power Dynamos na nyingine nyingi zinazotarajiwa kuongeza ushindani mkubwa.

Yanga na Simba wataingia katika mashindano hayo wakiwa miongoni mwa timu zinazotazamwa kwa karibu kutokana na mafanikio yao ya miaka ya karibuni katika mashindano ya CAF.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, ushindani nao unatarajiwa kuwa mkubwa baada ya kushirikisha timu zenye historia kubwa kama Al Ahly, Raja Casablanca, USM Alger, CR Belouizdad, Kaizer Chiefs, Ceramica Cleopatra, CS Sfaxien, Azam FC, Singida Black Stars, Red Arrows, Tusker, Kitara, Rayon Sports, Hafia, Nations FC na nyingine nyingi.


YANGA, SIMBA KAZI NZITO

Kwa Tanzania Bara, matumaini makubwa yataelekezwa kwa Yanga na Simba ambao wamekuwa mabalozi wakubwa wa nchi katika mashindano ya CAF kwa miaka ya karibuni.

Yanga wameendelea kujijengea heshima kubwa baada ya kucheza hatua mbalimbali za juu katika mashindano ya Afrika na sasa wanaingia wakiwa na lengo la kuvuka hatua ya makundi na kupigania nafasi ya kutwaa ubingwa.

Simba nao wanaingia na historia yao ya kupambana dhidi ya vigogo wa bara, jambo lililowafanya kujijengea heshima kubwa Afrika Mashariki.

Kwa Azam FC, nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho ni fursa ya kurejesha makali yao katika mashindano ya CAF, huku Singida Black Stars wakitaka kuendeleza mafanikio waliyoonyesha katika msimu uliopita walipofanikiwa kufika hatua ya makundi.

KVZ na KMKM kutoka Zanzibar nazo zinatarajiwa kutumia ushiriki wao kujitangaza zaidi katika ramani ya soka la Afrika huku zikisaka rekodi mpya ya kufika mbali zaidi kufuatia Mlandege msimu uliopita kukwama hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MABINGWA WA ZAMANI WAREJEA

Moja ya vivutio vikubwa vya msimu huu ni uwepo wa mabingwa wengi wa zamani.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, zipo klabu tisa zilizowahi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Zamalek na TP Mazembe zinaongoza kwa kutwaa mataji matano kila moja, huku Esperance de Tunis ikiwa na mataji manne.

Mamelodi Sundowns imewahi kutwaa ubingwa mara mbili, wakati Orlando Pirates, Club Africain, MC Alger, ASEC Mimosas na Pyramids FC kila moja ikiwa imeonja ubingwa mara moja.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, CS Sfaxien ndiyo klabu yenye mafanikio makubwa zaidi ikiwa imetwaa ubingwa mara tatu.

USM Alger na Raja Casablanca zimewahi kunyanyua taji hilo mara mbili kila moja, huku Al Ahly ikiwa imewahi kulitwaa mara moja.

Uwepo wa klabu hizo unaifanya droo ya mwaka huu kuwa na mvuto mkubwa kutokana na historia na uzoefu wao katika mashindano ya CAF.


AL AHLY KIVUTIO

Habari kubwa zaidi msimu huu ni kushiriki kwa Al Ahly katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.

Ni jambo lisilo la kawaida kwa klabu hiyo yenye historia kubwa zaidi Afrika, lakini litafanya Kombe la Shirikisho kuwa na ushindani mkubwa zaidi.

Al Ahly itaingia ikiwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na uzoefu wake, ubora wa kikosi na historia yake katika mashindano ya kimataifa.

AZAM YAPATA FAIDA

Habari njema kwa Azam FC ni kwamba haitaanza mashindano kutoka raundi ya awali.

CAF imeiweka Azam FC miongoni mwa klabu nane zitakazoanzia moja kwa moja hatua ya pili ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Klabu nyingine zilizopewa nafasi hiyo ni Al Ahly, USM Alger, AS FAR, CR Belouizdad, Raja Casablanca, AS Maniema Union na AS Otoho.

Hatua hiyo inaipa Azam FC muda zaidi wa kujiandaa pamoja na kupunguza idadi ya mechi za kucheza kabla ya kufika hatua ya makundi.


MAMILIONI MEZANI

Mbali na heshima ya kutwaa ubingwa wa Afrika, msimu huu pia una ushindani mkubwa kutokana na ongezeko la fedha za zawadi.

CAF imeendelea kuboresha mfumo wa zawadi ili kuongeza ushindani na kuziwezesha klabu kujiendesha vizuri kifedha.

Kila timu inayoshiriki mashindano hayo itapata Dola 100,000 (Sh265 milioni) za Marekani kwa ajili ya gharama za usafiri katika hatua za awali.

Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika atazawadiwa Dola 6,000,000 (Sh15.9 bilioni), huku wa pili akipata Dola 2,000,000 (Sh5.3 bilioni).

Timu zitakazofika nusu fainali zitapata Dola 1,200,00 (Sh3.2 bilioni), robo fainali Dola 900,000 (Sh2.4 bilioni) na kila timu itakayofuzu hatua ya makundi itahakikishiwa Dola 700,000 (Sh1.9 bilioni).

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, bingwa atapata Dola 4,000,000 (Sh10.6 bilioni), wa pili Dola 1,000,000 (Sh2.7 bilioni), nusu fainali dola 750,000 (Sh2 bilioni), robo fainali Dola 550,000 (Sh1.5 bilioni) na kila timu itakayocheza hatua ya makundi itapata Dola 400,000 (Sh1 bilioni).

Fedha hizo zimeongeza hamasa kwa klabu nyingi ambazo sasa zinaona mashindano ya CAF kuwa fursa ya kuongeza mapato pamoja na kujitangaza kimataifa.


NAFASI YA KLABU ZA TANZANIA

Kwa miaka ya karibuni, soka la Tanzania limeendelea kupanda katika viwango vya Afrika kutokana na mafanikio ya Yanga, Simba na Azam FC katika mashindano ya CAF.

Matokeo hayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayoheshimiwa zaidi Afrika Mashariki na sasa matarajio ni kuona klabu zake zikisonga mbele zaidi.

Yanga na Simba wanatarajiwa kubeba matumaini makubwa ya Watanzania katika Ligi ya Mabingwa, huku Azam FC na Singida Black Stars wakisaka mafanikio katika Kombe la Shirikisho.

Kwa upande wa Zanzibar, KVZ na KMKM watakuwa na nafasi ya kuonyesha maendeleo ya soka la visiwani dhidi ya wapinzani kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

MWANZO WA VITA

Droo ya Agosti 6 haitatoa bingwa, lakini itaweka msingi wa safari ya kila timu kuelekea ndoto zake.

Baadhi ya klabu zitapata bahati ya kukutana na wapinzani wanaoweza kuvuka kirahisi, huku nyingine zikikutana mapema na vigogo wa bara na kufanya safari yao kuwa ngumu.

Hata hivyo, historia ya mashindano ya CAF imeonyesha kuwa mara nyingi matokeo huamuliwa uwanjani na si kwa ukubwa wa jina la mpinzani. Ngoja tuone.