NIONAVYO: Tutafute mafanikio michezoni kwa hatua za maendeleo

MICHUANO ya soka ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 inafikia tamati Jumapili kwa mechi ya fainali  itakayowakutanisha wenyeji tembo wa Ivory Coast na tai wa kijani wa Nigeria.
Baada ya vumbi kutulia kila taifa litakaa chini kuangalia nini walichovuna, wapi wameteleza na nini kifanyike ili waweze kufanya vizuri hii ni kwa wale wa fungu la Taifa Stars, na kwa waliofanya vizuri waangalie wapi pa kuimarisha ili wafanye vizuri zaidi.

Hakika mashindano haya yametuonyesha ni wapi tulipo na wapi tunapaswa kuwa. Udhaifu wetu umewekwa hadharani kwa watu kuona lakini hii si mara ya kwanza na ni juu yetu kukereka.
Tangu nchi hii ipate uhuru, Tanzania imeshiriki Afcon mara tatu na kuambulia jumla ya pointi tatu.

Yapo mataifa kama Afrika Kusini, Angola na hata majirani zetu wa Msumbiji na Zambia wameshiriki mara nyingi na kupata mafanikio zaidi yetu.

Wimbo ni uleule hata katika michezo mingine.Timu zinaandaliwa baada ya vyama husika au wizara husika inapopewa barua ya kuonyesha uwepo wa mashindano fulani. Hakuna nguvu kubwa inayowekwa kwenye michezo ya shule za msingi (Umitashumita) au hata ile ya sekondari (Umisseta).

Michezo hii imekuwa ni ratiba tu ya kukamilisha kalenda ya mwaka badala ya kuwa sehemu ya kuonyesha vipaji kama vilivyoandaliwa huko shuleni. 

Kadhalika hata katika vyama kama chama cha riadha, chama cha ngumi za ridhaa na vinginevyo huwezi kusikia shughuli za maana sana za maendeleo ya vijana, vimekuwa ni vyama vya mashindano.

Ni kweli mashindano ni sehemu muhimu ya chama cha michezo, lakini utashindanisha nini ikiwa hukuandaa watoto na vijana kuja kuwa wanamichezo wa kiwango cha kimataifa? 
Sera zimekuwa zikitungwa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya michezo lakini kwa kiasi kikubwa karatasi za sera zimekuwa zikiishia kufungia vitumbua mitaani kwani vitendo havionekani na kama vipo ni kwa kiasi kidogo. Unapoona nchi zinatwaa medali na tuzo za kimataifa siyo suala la kubahatisha, ni kazi kubwa inakuwa imefanyika.

Kuongelea maendeleo ya michezo na mafanikio katika mashindano ni sawa na kuongelea maendeleo ya kilimo na mafanikio katika gulio la chakula.

Ni sawa na kuongelea kinachoendelea katika tasnia ya kilimo dhidi ya kinachoendelea katika masoko ya Kariakoo, Tandale, Tegeta Nyuki, soko jipya na mengine yanayouza chakula kama yalivyotapakaa Dar es Salaam na miji mikubwa nchini.

Katika michezo yote mpira wa miguu umekuwa na mafanikio katika mashindano ya ndani japo ni vigumu kuyaita mafanikio hayo kama ya kisera au maendeleo ya mchezo wenyewe.

Mtandao mmoja wa kimataifa umetaja Ligi Kuu Tanzania kama moja ya ligi sita bora barani Afrika. Hayo si mafanikio madogo hasa kwa nchi iliyo kusini mwa jangwa la Sahara nje ya Afrika ya Kusini. Kana kwamba hiyo haitoshi, klabu zinazotokea katika Ligi Kuu (hasa za Simba na Yanga) zimewekwa kati ya klabu 20 bora kabisa barani Afrika.

Kwa sasa Simba SC ni kati ya timu nane waanzilishi wa mashindano mapya ya Ligi ya Afrika (AFL) huku klabu hizo mbili zikishiriki Ligi ya Mabingwa mwaka huu. 

Simba wamekuwa wenyeji katika hatua za makundi na robo fainali za mashindano ya klabu barani Afrika huku Yanga ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Katika Ligi Kuu unaweza kuona namna klabu hata vzile zinazoitwa ndogo kama Tabora United, Ihefu na nyingine zikiwa zimesheheni wachezaji mahiri hasa wa kigeni.

Angalia kikosi cha Taifa Stars kwa kulinganisha na mataifa mengine hata majirani zetu Uganda, nahisi bado sisi ni madalali wa Kariakoo na hatujawekeza vya kutosha mashambani. Hatuna wigo mpana wa uchaguzi wa wachezaji wa timu ya taifa.

Kwa maana nyingine hatujafanya vya kutosha katika maendeleo ya mpira. Waganda wanaita wachezaji wao wengi walioko Ulaya kwa ajili ya timu ya taifa, sisi tunajaribu kutafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania ambao hatukuchangia kuwaendeleza. Ni kama tunarusha jiwe gizani.

Kuita wachezaji wenye asili ya Tanzania siyo jambo baya, lakini hilo haliwezi kuwa msingi wa mipango yetu ya maendeleo. Tulee wanamichezo wetu kwa viwango tulivyojiwekea. Tukibahatika kupata mwanamichezo mwenye vinasaba vya Tanzania, hiyo tutashukuru kama nyongeza tu.

Ligi yetu ni kama soko la Kariakoo; tunauza tusichozalisha. Ligi yetu ni bora, sawa, lakini tunazalisha wachezaji wa kutosha kuilisha ligi ili iendelee kuwa bora? Je, tunazalisha makocha wa wengi wenye viwango kuitosheleza ligi yetu? Madaktari je?

Wataalam wa lishe? Watawala? Masoko na habari? Naamini sehemu kubwa ya majibu yatakuwa ni HAPANA.
Jibu hilo ndilo linaturudisha kwenye ukweli kuwa tumewekeza zaidi katika gulio (matukio/mashindano) kuliko shambani (maendeleo). Lala uamke ukutane na tangazo kwamba wachezaji wa kigeni kwenye Ligi Kuu wamepunguzwa idadi kwa kila klabu; je, ligi yetu itakuwa ileile? Walimu wa kigeni wakipunguzwa au wataalam wa viungo   je? Jibu linarudi palepale kwamba hatujawekeza vya kutosha katika maendeleo endelevu.

Angalia viwanja vyetu mikoani na mitaani nje ya vile vinavyochezewa Ligi Kuu, utaumia sana. Viwanja havina viwango vya kusaidia vijana wadogo kujifunza mpira kisayansi maana kuna vichuguu, mabonde, majaruba na kadhalika.
Maendeleo ya mpira yanaanza na uzalishaji wa wachezaji kwa maana ya soka la vijana. Taifa lolote haliwezi kusema linafanya maendeleo endelevu ya mpira wa miguu na hata michezo mingine kama halina miradi na miundombinu ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya vijana.

Klabu zinazonunua wachezaji bila kuzalisha wachezaji zina maendeleo bandia ambayo yanaweza kuondoka wakati wowote. Duniani kote hakuna klabu iliyofanikiwa kuzalisha wachezaji wote inaowataka lakini siku zote uti wa mgongo wa mafanikio ya klabu ni wachezaji na hata wataalamu waliokulia katika mpango wa klabu husika.

Hapa kwetu ni jukumu la mamlaka za mpira na hata wizara inayohusika na michezo kuwekeza na kuweka sera zaidi katika maendeleo ili kuendana na kasi ya uwekezaji katika matukio.
Ukiangalia viwango vya Fifa wastani wa viwango vya Tanzania kwa timu ya taifa ya soka ya wanaume ni nafasi ya 125 duniani na nafasi zaidi ya 30 barani Afrika huku tukiwa na ligi bora na klabu bora. Ni kama kuvaa suti na kandambili. Tunatakiwa kuwekeza katika vijana, wataalamu na miundombinu ya kutosha wakati soko linapatikana hapa nyumbani. Tunatakiwa kukimbia wakati wenzetu wanatembea.

Afcon imetuonyesha jinsi Watanzania wanavyopenda michezo lakini zaidi wanapenda mafanikio katika michezo. Timu ya Taifa ilipoanza kufanya vibaya (dhidi ya Morocco) kule Ivory Coast, hapa nyumbani ikawa kama msiba.

Hata hivyo, haikuishia hapo Watanzania hawa wakaanza kujinasibisha na wachezaji wa kigeni wanaocheza hapa nchini waliokuwa kwenye timu za mataifa kama Mali, Burkina Faso, Zambia na DR Congo. 

Hii inakupa picha ya kiu ya mafanikio miongoni mwa Watanzania japo hili limekuwa gumu kama kupata tone la maji kwenye nchi yenye mafuriko na mvua nyingi. Tunashindwa kuandaa wanamichezo wazuri katika nchi ya watu takribani milioni 60.

Tunashindwa kutafuna mfupa uliotafunwa na vinchi kama Iceland na Cape Verde vyenye watu chini ya milioni moja.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.