Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake msitoboe kila mahali

UREMBO Pict

Muktasari:

  • Ukweli kutoka kwa Wataalamu ni kwamba si kila eneo la mwili limeumbwa kwa ajili ya kutobolewa. Kuna sehemu ambazo hutobolewa kwa urahisi na kupona vizuri, lakini zipo ambazo zina mishipa mingi ya damu, neva muhimu au hukaa kwenye mazingira yanayorahisisha maambukizi. Ndiyo maana kabla ya kuvaa kipini kwa sababu ya urembo, ni muhimu kuelewa madhara yanayoweza kujitokeza.

SIKU hizi ukitaka kuonekana wa kisasa, kwa baadhi ya wanawake ni lazima uwe na kipini sehemu fulani ya mwili. Wengine wameishia kutoboa masikio, lakini sasa mitindo imehamia puani, kitovuni, ulimini, nyusi, midomoni na hata sehemu za siri.

Kinachosikitisha ni kwamba wengi wanakimbizana na mitindo ya mitandaoni bila kujiuliza kwanza kama sehemu wanayotoboa ni salama au la.

Ukweli kutoka kwa Wataalamu ni kwamba si kila eneo la mwili limeumbwa kwa ajili ya kutobolewa. Kuna sehemu ambazo hutobolewa kwa urahisi na kupona vizuri, lakini zipo ambazo zina mishipa mingi ya damu, neva muhimu au hukaa kwenye mazingira yanayorahisisha maambukizi. Ndiyo maana kabla ya kuvaa kipini kwa sababu ya urembo, ni muhimu kuelewa madhara yanayoweza kujitokeza.

URE 02

MASIKIO NI ENEO SALAMA ZAIDI

Kutoboa sehemu ya chini ya sikio ndiyo njia inayokubalika zaidi kwa sababu eneo hilo lina nyama laini na mishipa michache. Hata hivyo, kutoboa kwa vifaa visivyo safi kunaweza kusababisha maambukizi, usaha, uvimbe na makovu yanayobaki maisha yote. Kutoboa sehemu ya juu ya sikio huchelewa kupona na huongeza hatari ya maambukizi makubwa.


PUANI SIO SALAMA

Kutoboa pua ni mtindo unaopendwa na wanawake wengi, lakini eneo hilo lina bakteria wengi kuliko watu wanavyofikiri. Endapo vifaa havikutakaswa au kipini hakihudumiwi vizuri, unaweza kupata maambukizi yanayosababisha uvimbe, usaha na maumivu ya muda mrefu. Wataalamu pia hushauri kuepuka kubadilisha kipini kabla jeraha halijapona.

URE 01

KITOVUNI HATARI

Vipini vya kitovuni vinaonekana vya kuvutia, lakini eneo hili hupata msuguano wa mara kwa mara kutokana na nguo na harakati za mwili. Hali hiyo husababisha jeraha kuchelewa kupona, kutokwa na usaha au kuacha kovu kubwa. Kwa baadhi ya watu, kupona kunaweza kuchukua miezi kadhaa.


ULIMINI SIO PAZURI

Kutoboa ulimi ni miongoni mwa maeneo yenye hatari zaidi kwa sababu mdomoni kuna bakteria wengi. Baada ya kutobolewa unaweza kupata uvimbe mkubwa, maumivu wakati wa kula na kuzungumza, kutokwa damu au hata kuharibu meno kutokana na kipini kugongana nacho mara kwa mara.

URE 03

MIDOMO SIO LAZIMA

Vipini vya mdomoni vinaweza kuonekana vya kuvutia, lakini msuguano wa kipini dhidi ya fizi unaweza kusababisha fizi kujiondoa taratibu na kuacha mizizi ya meno wazi. Pia meno yanaweza kupasuka au kuchakaa kutokana na kugongwa na kipini kila mara unapoongea au kula.


NYUSI

Eneo la nyusi lina ngozi nyembamba. Kwa baadhi ya watu mwili hukataa kipini na kukisukuma nje taratibu, jambo linaloweza kuacha kovu lisiloisha. Pia eneo hili linaweza kuvimba kwa muda mrefu ikiwa halitatunzwa vizuri.


KWENYE CHUCHU

Baadhi ya wanawake hutoboa chuchu kwa sababu za urembo au mtindo, lakini ni eneo lenye mishipa mingi ya fahamu. Kutoboa sehemu hiyo kunaweza kusababisha maumivu makali, maambukizi, kutokwa damu na kuathiri unyonyeshaji endapo kutatokea matatizo kwenye mirija ya maziwa.


SEHEMU ZA SIRI

Ingawa wapo wanaochagua kutoboa sehemu za siri kwa sababu mbalimbali, wataalamu wengi wa afya wanaonya kuwa eneo hili lina unyevunyevu wa muda wote na bakteria wengi.

Hali hiyo huongeza uwezekano wa maambukizi, kutokwa damu, maumivu makali na kuchelewa kupona. Endapo utaratibu hautafanywa na mtaalamu katika mazingira safi, madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.

URE 04

WASIKIE WADAU

Diana Songa anasema, yeye haamini kabisa kama urembo pekee ni kutoboa masikio kwani kuna mambo mengi ambayo mwanamke anaweza kuyafanya yasiyoumiza na akawa mrembo.

"Kwangu siamini kama urembo pekee ni kujitoba toboa, ila naweza kupaka mafuta mazuri,kusuka nywele na hata kuvaa vizuri bila hata kutoboa mwili na bado nikaonekana mrembo sana.'

Nevumba Abubakary anasema anatamani sana kutoboa pua ila aliwahi kuambiwa na Bibi yake ambaye ameshafanya hivyo kuwa, urembo huo unamaumivu makali sana.

"Napenda sana kutoboa pua ila naogopa kwa sababu nilishaambiwa ni eneo lililo na maumivu makali sana, aliyeniambia ni Bibi yangu na alisema kabisa sitaweza kuvumilia uchungu wake."

Charles Abel anasema kuwa;"Kama mwanamke ameweza kutoboa maeneo hatari kwenye mwili wake, hawezi kushindwa kunitoboa na mimi au hata hisia zangu."

Shebby Kondo anasema kuwa:"Mwanamke ambaye ametoboa kila maeneo kwangu ni muhuni tu siwezi hata kumuoa."

Mpoki Thomson anasema kuwa:"Inategemea ila kwa upande wangu naona ni kawaida kwa sababu ni urembo."

Baraka anasema kuwa;"Nikikutana na mwanamke aliyejitoboa maeneo mengi nikimuona nashindwa kumuelewa, kwa sababu sio jambo la kawaida na pia nitaangalia na mavazi yake."


MSIKIE DAKTARI

Daktari Dorcas Natse anasema wengi wanatoboa sehemu ya juu ya ngozi kwa hiyo inatengeneza alama na kama utatumia vifaa feki wako kwenye hatari ya kutopona haraka.

"Kabla ya kutaka kutoboa kokote kule, jambo la kwanza fahamu aina ya ngozi yako, wapo ambao wamejikuta wakibaki na makovu au hata kuota vinyama sehemu ambazo wamezitoboa.

"Sio rahisi sana mtu kupata magonjwa makubwa kama kansa, zaidi hutapata heshima kwenye jamii ila shida ya watu wengi wanatumia vifaa feki katika harakati hizo, jambo ambalo linaweza kusababisha vidonda visivyopona kwa haraka na kupelekea kupoteza kabisa maana ya urembo."