Naomi Osaka: Staa wa tenisi asiyekuwa na shughuli ndogo kazini
Muktasari:
- Sheria kali za michuano ya Wimbledon iliyofanyika mwezi uliopita zinawataka wachezaji kuvaa mavazi meupe pekee, lakini hilo halikumzuia Osaka kufanya tukio lake la kuvutia kabla ya mchezo wake dhidi ya Elsa Jacquemot.
WIMBLEDON, ENGLAND: NAOMI Osaka aliendelea na mtindo wake wa kuvutia katika mashindano ya tenisi ya Wimbledon, baada ya nyota huyo wa Japan kuingia uwanjani akiwa amevalia vazi la kimono la kuvutia katika mchezo wake wa kwanza, huku akiahidi kuwa bado kuna mengine mengi yanakuja.
Sheria kali za michuano ya Wimbledon iliyofanyika mwezi uliopita zinawataka wachezaji kuvaa mavazi meupe pekee, lakini hilo halikumzuia Osaka kufanya tukio lake la kuvutia kabla ya mchezo wake dhidi ya Elsa Jacquemot.
Mashabiki waliokuwa kwenye Uwanja wa 3 walilipuka kwa shangwe Osaka alipoingia kwenye nyasi akiwa na vazi lililochota msukumo kutoka kwenye mavazi ya jadi ya sherehe za Kijapani. Mbunifu wa mavazi wa Tokyo, Hana Yagi, alikuwa ametumia pia wazo kutoka kwenye kirigami, sanaa ya Kijapani ya kukata karatasi kutengeneza vazi hilo.
Osaka alivaa vazi jeupe maalumu lililopambwa kwa michoro ya korongo na maua ya cherry, vitu vinavyoashiria utamaduni wa Japan. Vazi hilo lilikuwa na mikono mipana yenye umbo la kengele, mkanda wa obi unaovaliwa kwenye kimono na utepe mrefu wa nyuma.
Baada ya ushindi wake wa seti 6-1, 7-5 dhidi ya Jacquemot, Osaka alisema: "Ninapofikiria Wimbledon, jambo la kwanza ni rangi nyeupe. Ni mashindano ya zamani zaidi, siyo? Halafu kuna suala la utamaduni na mila zake."
"Ninapofikiria hilo, nafikiria tamaduni zangu na urithi wangu, ambao ni wa Kijapani na Haiti. Nikichunguza zaidi utamaduni wa Japan, nafikiria umbo maarufu zaidi ambalo kwangu ni kimono. Huhitaji hata kuona rangi ya kimono ili kujua kwamba ni kimono."
Osaka pia anasema alichochewa na filamu yake anayoipenda, Kill Bill, hasa mhusika wake Lucy Liu.
"Nakumbuka nilivyopenda sana uhusika wa Lucy Liu. Alikuwa na kimono cheupe kabisa, na nilifikiri kilikuwa kitu kizuri na cha kuvutia. Ndipo wazo likaanza kukua. Ilikuwa tafsiri yangu mwenyewe huku nikionyesha heshima na upendo mkubwa kwa Japan."
VAZI LENYE HISTORIA YA JAPAN
Osaka alikamilisha mwonekano wake kwa mapambo ya nywele ya kanzashi, ambayo kihistoria yalivaliwa na geisha, pamoja na vito kutoka kampuni maarufu ya lulu ya Japan, Mikimoto.
Mbunifu Yagi aliliambia jarida la Vogue kwamba vazi hilo lilitengenezwa kutokana na Shiromuku za zamani (mavazi ya jadi ya harusi ya Kijapani), Kimono, mavazi ya harusi, ambayo yote ni mavazi ya sherehe yaliyotengenezwa kuashiria nyakati muhimu katika maisha ya watu.
Baada ya kusalimiana na Jacquemot, Osaka alikwenda kwenye kiti chake na kuvua tabaka za nje za vazi hilo, ambazo zilitengenezwa kuondolewa, na kubaki na vazi jeupe la Nike la mchezo lililokuwa pia na mapambo yanayofanana.
"Nilifikiri ilikuwa jambo la kufurahisha kwa sababu sikudhani mtu yeyote alitarajia hivyo," anasema Osaka.
"Nilijaribu kuzingatia mchezo na kuvaa 'headphones' zangu. Lakini nilihisi kwamba nilipopita karibu na watu, waligeuka kabisa kunitazama. Niliona hilo kuwa jambo la kufurahisha."
Anasema baadhi ya watu walimpongeza. "Watu wengine walikuwa wakisema, 'wow, hiyo ni kimono nzuri sana.' Lilikuwa jambo zuri kusikia."
Osaka anasema amezoea kuvaa mavazi ya kipekee, "kila mtu ana njia yake ya kuonyesha kwamba anapenda mitindo. Mimi huwa nashangaa ninapoingia chumba cha kubadilishia nguo kwa sababu wachezaji wengi huniuliza maswali kuhusu mavazi yangu."
Baadhi ya wachezaji walimuuliza kama ana kimono moja tu kwa sababu ni jeupe na nini hutokea likichafuka.
"Waliniuliza, likichafuka unalibadilisha rangi? Je, hilo linakiuka sheria za Wimbledon kwa sababu si nyeupe tena?"
Wimbledon haina hofu na mtindo wa mavazi wa Osaka, ambapo mkurugenzi anayemaliza muda wake, Sally Bolton, anasema hawakuwa na wasiwasi kwamba angekiuka sheria za mavazi.
"Tuko watulivu, mradi tu linafuata kanuni ya mavazi meupe," anasema Bolton na kuongeza:
"Sijawahi kuzungumza naye kuhusu anachovaa, lakini kama ilivyo kwa wanamichezo wetu wote wanahitaji tu kufuata sheria za mavazi meupe. Sidhani kama tutakuwa na tatizo lolote."
BALAA LAKE FRENCH OPEN
Kuingia kwa Osaka Wimbledon akiwa kivazi cha pekee kumekuja wiki chache baada ya vazi lake la dhahabu lenye msukumo wa Mnara wa Eiffel katika French Open kuzua mjadala, ambapo baadhi ya watu walimshutumu kwamba alikuwa akiweka mbele mitindo kuliko tenisi.
Osaka, anayelipwa takribani Pauni 7.5 milioni kwa mwaka kutokana na mkataba wake na Nike, hakurudi nyuma. Aliingia Roland Garros akiwa na koti na sketi zilizotengenezwa upya kutoka kwenye mavazi yake ya zamani ya mechi.
Katika mchezo wake wa raundi ya nne dhidi ya Aryna Sabalenka, alivaa koti na sketi yenye mapambo ya kung'ara juu ya vazi lake la dhahabu.
Mpinzani wake wa raundi ya kwanza, Laura Siegemund, alimkosoa akisema: "Nilikuja hapa kucheza tenisi, siyo kufanya onyesho la mitindo."
Lakini, Jacquemot hakuliona hilo kama tatizo, akisema: "Nadhani linaonyesha utu wake. Kwa kweli halinisumbui kabisa. Mavazi yake ni mazuri, hivyo ni jambo zuri."
Mpinzani wake mwingine, Donna Vekic, alisema: "Baadhi ya watu wanaichukulia tenisi kwa uzito kupita kiasi. Tulia, ni vazi tu. Ni vizuri kwamba anafanya vitu tofauti na kujieleza kupitia mitindo."
MALKIA WA MITINDO
Osaka amekuwa maarufu kwa kuingia uwanjani kwa mitindo ya kipekee katika mashindano makubwa ya Grand Slam, kwani hata katika Australian Open mwezi Januari mwaka huu, aliingia akiwa na vazi lililochota msukumo kutoka kwa samaki aina ya jellyfish.
Alifika Rod Laver Arena akiwa na kofia kubwa yenye pazia jeupe na mwavuli, kisha akafanya mazoezi akiwa na koti lenye mikunjo na vazi lililofanana na mikia ya jellyfish. Katika Indian Wells, aliingia uwanjani akiwa na mapambo ya mtindo wa kikabila kwenye midomo, pua na masikio, pamoja na vazi jeusi la Nike lenye michoro ya ngozi ya duma.
Pia alivutia macho kwenye Met Gala mwaka huu akiwa na onyesho la kipekee la "kubadilika ngozi", ambapo alivaa koti jeupe lililofunikwa manyoya mekundu yaliyofanana na damu, kisha kulivua na kubaki na vazi jekundu lililopambwa kwa fuwele lililofanana na misuli na mishipa ya mwili.
Osaka anasema: "Ni jambo la kufurahisha kuwaona wabunifu wakifanya kazi, hasa pale wanapokuwa na kitu maalumu wanachotakiwa kukizingatia wakati wa kubuni." Kuhusu vazi lake la dhahabu la French Open, anasema: "Nilipoliona kwa mara ya kwanza nilihisi kama Mnara wa Eiffel wakati wa usiku ukiwa unang'ara."
Lakini pia anatania kwamba aliogopa jua lingeakisi mwanga mwingi na mwamuzi angemtoa uwanjani, "nilifikiri labda mwamuzi angenitoa kwa sababu linameremeta sana." Osaka anasema katika baadhi ya matukio ya Grand Slam mara nyingi hujisikia kuwa mburudishaji.
"Wakati mwingine watu husema wanamichezo ni sehemu ya biashara ya burudani. Kwangu mimi, kuingia uwanjani kwenye Grand Slam ndiyo wakati pekee ninapohisi kama mimi ni mburudishaji."
Na bado ana mipango zaidi, ambapo anadai kuwa na mavazi mengine tayari kwa ajili ya raundi mashindano yajayo, akisema: "Napenda kubadilisha mambo. Najaribu kuwa na kitu tofauti kila raundi."