Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Pamoja Bid safi, sasa tutembee pamoja 2027

HATIMAYE historia imeandikwa Afrika Mashariki baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutangaza kuzipa uenyeji, Tanzania, Kenya na Uganda kupitia Pamoja Bid (maombi ya pamoja ya nchi hizo) kwa kushinda mbele ya wapinzani wengine waliokuwa wakiwania kuandaa Fainali za Afrika (Afcon) 2027.

Uamuzi huo wa CAF haukuwa wa kushangaza japo ni wa kihistoria kwa Afrika ya Mashariki ambayo haijawahi kuandaa mashindano haya na katika ukanda mzima, japo ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mara ya mwisho yalifanyika 1957 na mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 1976 ikiwa ni mara ya tano. Kuna sababu za kimpira za siasa na siasa za mpira na za kitaasisi pia zilizopelekea kwa kiasi kikubwa maombi ya Kenya, Tanzania na Uganda kufanikiwa.

Ni sera ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na CAF na zaidi ni agenda ya Rais wa shirikisho hilo la Afrika, DK. Patrice Motsepe kuona mpira unachezwa katika kila taifa la Afrika. Ili sera hii ifanikiwe ni muhimu kuhakikisha matukio makubwa ya kimpira yanatawanywa kote Afrika. Kwa muda mrefu mashindano makubwa yamekuwa yakifanyika katika mataifa ya Kaskazini na kwa kiasi fulani Afrika Magharibi yenye miundo mbinu bora ya kimpira kulinganisha na yale ya Afrika Mashariki.

Hili halikuwa sahihi katika kueneza mpira wa miguu hivyo kuchangia maamuzi haya ya Kamati ya Utendaji ya CAF.

Mwaka 2014, Libya ilinyang’anywa na CAF uenyeji wa Afcon ya 2017 kutokana na kuwepo vita. Serikali ya Tanzania chini ya Rais Kikwete ilitoa ruhusa ya kuomba kuchukua nafasi ya Libya. Maombi hayo hayakupita na Gabon akapewa uenyeji. Lakini Rais wa CAF wa wakati huo Issa Hayatou akaeleza bayana utashi wake wa kuiona Tanzania ikiwa mwenyeji katika siku za karibuni; Moja ya masharti tuliyopewa ilikuwa ni kuandaa mashindano ya CAF ya vijana au yale ya wanawake ili kuthibitisha uzoefu kabla ya kufikiriwa kuwa wenyeji. Mwaka 2016 tulipeleka maombi ya kuandaa Afcon ya vijana chini ya miaka 17 ya mwaka 2019 na mwaka 2017 Mjini Libreville tukakabidhiwa bendera ya uenyeji na kuyaandaa mashindano hayo ya Afcon (U17) kwa mafanikio.Hiki ni kigezo ambacho pia kimechangia CAF kufikiria Pamoja Bid 2027

Utashi wa kisiasa wa viongozi wa mataifa ya Kenya, Tanzania na Uganda kwa maana ya Marais William Ruto, Samia Hassan na Yoweri Museveni umechangia kwa kiasi kikubwa maombi ya Afrika Mashariki kuchukuliwa kwa uzito wake. Kwenye makaratasi FIFA inasema mpira hauingiliani na siasa lakini kiutendaji ni matokeo ya uwanjani tu yasiyoingiliwa na siasa lakini katika maamuzi mengine ya utawala wa mpira serikali zina nafasi kubwa kama tulivyoona hapa nchini na hata kwa FIFA. Si jambo rahisi kwa CAF na Rais wake Motsepe kupuuza maombi ya marais watatu. Nguvu ya marais wao inaonyesha utashi (commitment) ya kuyafanya mashindano hayo ya 2027 kwa mafanikio.

Katika siasa za mpira wa Afrika, ni vigumu kwa uongozi wa CAF kupuuza ukanda wenye mataifa zaidi ya 10 unapotaka jambo lake. Ukanda wa Cecafa ulio chini ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia una kura za maamuzi zaidi ya 10 ndani ya CAF. Kwa hiyo ukanda huo wenye zaidi ya 20% ya kura kwenye vikao vya CAF ni vigumu kuukatalia unapotaka jambo lake maana kinyume na hivyo kutoridhika kwao kunaweza kuigharimu CAF kama taasisi na uongozi wake pia.

Bila shaka kuna sababu nyingine zilizo kwenye andiko lililowasilishwa na maombi hayo ya Pamoja 2027 ikiwa ni kueleza maendeleo ya miundombinu na huduma kama barabara, hoteli, hospitali, viwanja vya mazoezi n.k. Ni juu ya serikali na vyama wenyeji kukaa chini na kuhakikisha kilichokuwa kwenye karatasi kinaamia kwenye vitendo. 

Mwaka 2027 unaweza kuonekana mbali lakini kwa mahitaji ya mashindano makubwa kabisa barani Afrika muda huo ni mfupi. Kuna umuhimu wa kuunda kamati za maandalizi ndani ya mataifa hayo matatu na pia kamati ya maandalizi ya pamoja. Kuna mambo na majukumu ya kugawana kati ya mataifa haya ambayo binafsi sina hakika kama yote yatakuwa kwenye andiko lililowasilishwa CAF.

Kuandaa mashindano kwa pamoja (competition co-hosting) kuna faida nyingi ikiwa ni pamoja na shamrashara za kuwa na timu nyingi wenyeji lakini kunaweza kuwa na changamoto hasa kunapotokea tofauti katika kugawana majukumu na maslahi. Hili ni jambo la kuangalia kwa makini na kuhakikisha wahusika wote wanaenda pamoja.

Hapa ndipo Pamoja 2027 itapaswa kuwa pamoja ili kuwa na msimamo wa pamoja kwa maana ya kuogelea pamoja na kuzama pamoja. Kuandaa kwa pamoja kunaweza kuonekana kurahisisha maombi lakini utekelezaji wake haujawahi kuwa mwepesi. Kuna haja ya kuchuma jani kutoka matukio kama Kombe la Dunia Korea&Japan 2002 au yajayo ya Canada, Mexico & USA 2026 wakati wa kujiandaa kwa mashindano haya.

Juhudi za maombi zilianza chini ya Rais Kikwete, Afcon U 17 ikafanyika Dar es Salaam chini ya Hayati John Magufuli na hatimaye Pamoja Bid ikafanyika na kufanikiwa chini ya Rais Samia Suluhu. Imechukua pia marais watatu wa CAF yaani Hayatou, Ahmad na sasa Motsepe. Hii ni hatua kubwa kwa mpira wa Tanzania na Afrika Mashariki.

Mwandishi ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.