NIONAVYO: Mwanzo mzuri Afcon 2025 kwa nchi za Afrika Mashariki
Muktasari:
- Kenya iko kileleni mwa Kundi J linalozijumuisha nchi za Namibia, Zimbabwe na Cameroon ikikusanyia pointi nne, baada ya kutoka suluhu nyumbani dhidi ya Zimbabwe kabla ya kuifunga Namibia kwa mabao 2-1 mechi zote zikipigwa Afrika Kusini.
MICHUANO ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco mwaka 2025, ilishuhudiwa mechi za pili zikimalizika juzi Jumanne, huku mataifa ya Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda wenyeji wa fainali za 2027, zikiwa na mwanzo mzuri kwenye hatua hii.
Kenya iko kileleni mwa Kundi J linalozijumuisha nchi za Namibia, Zimbabwe na Cameroon ikikusanyia pointi nne, baada ya kutoka suluhu nyumbani dhidi ya Zimbabwe kabla ya kuifunga Namibia kwa mabao 2-1 mechi zote zikipigwa Afrika Kusini.
Taifa Stars ya Tanzania kama ilivyo kwa majirani zao hao, ilianza kwa suluhu nyumbani dhidi ya Ethiopia kisha kushinda ugenini kwa mabao 2-1 mbele ya Guinea, mechi iliyopigwa Ivory Coast na wenyeji waliamua kuchezea huko kwa sababu nchini kwao kumekosekana uwanja wenye kukidhi matakwa.
Stars ipo nyuma ya DR Congo inayoongoza Kundi H, ikizidiwa pointi mbili kwani Wakongoman wana sita na Tanzania ina nne, pointi kama ilizonazo pia, Uganda The Cranes iliyopo Kundi K ikilingana na Afrika Kusini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Uganda nayo ilishinda mechi moja na kutoka sare moja pia kama ilivyo kwa majirani zao hao, ikifungana mabao 2-2 ugenini dhidi ya Afrika Kusini, kabla ya kuwafunga Congo Brazzaville mabao 2-1.
Kwa sasa timu hizo zinasubiri mechi za raundi zijazo zitakazochezwa Oktoba, Tanzania ikiwa na kibarua mbele ya DR Congo, Kenya itaumana na Cameroon, huku Uganda itamalizana na Sudan Kusini ambao kwa miaka ya karibuni imekuwa kama hasimu mkubwa wa The Cranes.
Kwa matokeo hayo kuna dalili njema kwa timu hizo kwenda Morocco kama zitatumia vyema turufu ya mechi nne za kumalizana hatua hiyo ya makundi na kila timu mbili za juu za kundi zinafuzu moja kwa moja fainali hizo za Afcon 2025.
Ikiwa timu hizi wenyeji wa 2027 zitafanikiwa kwenda Morocco na kufanya vizuri, basi hilo litachagiza kuchangamka kwa mashindano yanayoandaliwa kwa pamoja na mataifa haya matatu mwaka 2027.
Ni muhimu sana kwa mataifa wenyeji kujenga timu zao na kuleta upinzani katika mashindano husika badala ya kuwa wasindikizaji tu.
Mashabiki wenyeji pia huwa nyuma ya timu zao na mashindano kwa jumla ikiwa timu zao zitasonga mbele.
Ujenzi wa timu kwa ajili ya Afcon 2027 ni sasa na wala si baada ya 2025.
Kuna baadhi ya wachezaji wanaweza kwa sababu moja au nyingine, wasionekane katika fainali hizo za 2027 kwa sababu mbalimbali ikiwamo umri na hata viwango, lakini kwa kuwa na kikosi chenye muunganiko mzuri, inafaa angalau nusu ya wachezaji wanaoshiriki Afcon 2025 wawe katika vikosi vya timu hizo mwaka 2027.
Ushindi katika Afcon unategemea sana uzoefu wa wachezaji na hivyo mashindano ya kufuzu na fainali za 2025 zitatoa fursa hiyo kwa timu zetu.
Jambo jingine la kufuraisha kwa timu za Afrika Mashariki ni kuona baadhi ya miundombinu ikitumika au kuruhusiwa kutumika. Uganda na Kenya mabao huko nyuma walikuwa wakitumia viwanja vya ugenini kwa michezo yao ya nyumbani sasa wanaweza kutumia viwanja vyao vya Nelson Mandela na Kasarani vilivyoko Kampala na Nairobi mtawalia.
Bila shaka miundombinu hiyo na mengine itaimarishwa na mingine mipya kujengwa na kupata michezo mingi ya majaribio kabla ya kuanza kutumika. Kwa upande wa Tanzania viwanja kama Benjamin Mkapa, Amani Complex na Azam Complex tayari vina ruksa ya kuandaa mashindano ya kimataifa.
Mashindano haya ya mtoano ya Afcon 2025 yatawezesha timu 24 kupatikana kwa ajili ya fainali hizo za 35 za mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kuanza Desemba 21 2025 hadi Januari 18, 2026 katika miji sita za nchi hiyo ya Morocco.
Afrika ya Mashariki kupitia nchi za Kenya, Tanzania na Uganda ilipeleka na kukubaliwa kuandaa kwa pamoja mashindano ya Afcon 2027 yanayotarajiwa kuchezwa katika miji mbalimbali ya mataifa hayo matatu ambayo yataandaa mashindano hayo makubwa barani Afrika kwa mara ya kwanza.
Hivyo matokeo ya sasa yatumiwe kama moja ya silaha ya kuwapeleka Morocco kibabe kwa mara nyingine kucheza fainali za Afcon 2025, kisha kujipanga upya kwa msimu wa 2027 kama wenyeji wa fainali hizo.
Kila kitu kinawezekana, muhimu wasibweteke kwa sasa kwani kazi iliyopo mbele yao ni kubwa kuliko walipo. Kazi kwao!
Mwandishi wa
makala HAYA ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la SOKA Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.