Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Miaka 90 Yanga bado imara sana

Muktasari:

  • Timu hiyo ilianzishwa mwaka 1857, karibu miaka 167 iliyopita na kwa sasa inacheza katika Ligi Kuu ya Majimbo ya Kaskazini, Mashariki Daraja la Kwanza ambayo ni kama Ligi Daraja la nane katika mfumo mzima wa soka la England.

SHEFFIELD FC ya England inatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kama klabu kongwe kuliko zote duniani ambayo bado inaishi na inafanya shughuli za soka.

Timu hiyo ilianzishwa mwaka 1857, karibu miaka 167 iliyopita na kwa sasa inacheza katika Ligi Kuu ya Majimbo ya Kaskazini, Mashariki Daraja la Kwanza ambayo ni kama Ligi Daraja la nane katika mfumo mzima wa soka la England.

Klabu hiyo ilianza kucheza soka kwa mfumo na kanuni zake yenyewe kwani ilianza kwa kushindanisha timu zake mfano ‘waliooa’ v ‘wasiooa’.

Kwa bahati mbaya baada ya ujio wa chama cha soka, kanuni mpya za nchi nzima na soka la kulipwa (professional football), Sheffield FC haikukubali mabadiliko haya haraka, hivyo kujikuta inadumaa katika madaraja ya chini huku timu jirani za Midlands kama Notingham na Stoke City zilizoundwa baadae zikisonga mbele na kuiacha ikijivunia historia.

Hadithi ya kuvutia ni ya mwaka 2007 wakati ilipopewa nafasi ya kusherehekea kumbukumbu ya miaka 150 ya kuanzishwa.

Sherehe hiyo iliudhuriwa na Rais wa Fifa enzi hizo, Sep Blatter na mgeni rasmi alikuwa gwiji wa soka Pele wa Brazil.

Sheffield iliyokuwa kwenye ligi za ‘mchangani’  ikapewa ofa ya kucheza na klabu kubwa za Ulaya za Milan na Ajax. Sherehe zilinoga sana, sherehe za umri mkubwa lakini bila mafanikio makubwa.

Wakati Sheffield ikiwa imeshakula chumvi ya zaidi ya karne na nusu, hapa nyumbani Young Africans SC ya jijini Dar es Salaam ilisherehekea mwaka wa 90 tangu kuanzishwa kwake.

Jumanne ya wiki hii, klabu hiyo maarufu kama Yanga ilitimiza umri huo tangu ilipoanzishwa rasmi Februari 11, 1935.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa akili mnemba, Yanga ndiyo klabu ya soka kongwe kuliko zote Tanzania na Afrika Mashariki.

Uchambuzi huo pia unaitaja klabu hiyo iliyochukua ubingwa mara 30 kama klabu yenye mafanikio zaidi Tanzania ikifuatiwa na wapinzani wao Simba waliochukua ubingwa wa nchi mara 22.

Kimahesabu, Yanga imekuwa ikichukua ubingwa mara moja katika kila miaka miwili tangu mfumo wa ligi ya nchi uanze mwaka 1965.

Unajiuliza ni nini kimeifanya Yanga iendelee au izidi kuwa maarufu nchini katika umri wa miaka 90?

Kusema kweli, Yanga imezikamata nyoyo na akili za wafuasi wake ambao wamekuwa nyuma yake inyeshapo mvua na liwakapo jua.

Maarufu kama klabu ya ‘Wananchi’, Yanga imejizolea umati wa mashabiki ambao ni uti wa mgongo kwa klabu yoyote ya soka na zaidi isiyomilikiwa na taasisi.

Historia ya kuanzishwa kwa klabu hii imehusishwa na harakati za kupigania ustawi, masilahi ya wenyeji na ukombozi wa Tanganyika kutoka kwa Waingereza.

Inasemekana ni klabu iliyokuwa inakutanisha wanamichezo mchana na usiku ikifanya harakati za kisiasa zilizokuwa zinapigwa vita na dola wakati huo.

Rais wa Kwanza wa Tanganyika, Julius Nyerere na wanaharakati wengine wa TANU waliitumia Yanga kama sehemu ya kufanya harakati zao.

Yanga pia ilihusika katika harakati za Zanzibar zilizokuja kuzaa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Upo ushahidi wa Yanga kuwa na wafuasi Zanzibar miaka mingi kabla ya Mapinduzi na kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa mstari wa mbele.

Haikushangaza Sheikh Karume alitoa fedha za kujenga makao ya klabu za Yanga na Simba kutokana na ombi la viongozi wa Yanga na Simba waliomtembelea Zanzibar mwaka 1969.

Uongozi bora uliojikita katika maendeleo ya klabu ni moja ya nguzo zilizoisimamisha klabu ya Yanga.

Ikumbukwe kwa muda mrefu klabu imeongozwa na watu wa kujitolea rasilimali muda na fedha ili mradi kuona klabu yao inasonga mbele.

Sababu nyingine ya klabu kuendelea kuwa imara na kupata wafuasi katika vizazi vipya ni uwezo wa klabu kunyumbulika kulingana na wakati.

Mabadiliko ya sheria, kanuni na namna ya kuendesha soka yamekuwa yakibadilika lakini Yanga hawakukubali kubaki nyuma.

Uongozi umekuwa ukibadilika na viongozi wapya wakija na maono mapya ambayo yamesaidia kuipeleka klabu mbele.

Pamoja na changamoto ya migogoro kama ule wa katikati ya miaka ya 1970 uliosababisha kuigawa klabu vipande viwili, bado Yanga ilisimama na kurudia uimara wake na kuchukua ubingwa mwaka 1981.

Pamoja na mafanikio lukuki na viunzi vya changamoto ilizoruka, bado Yanga ina safari ndefu na kazi kubwa ili ifikishapo karne na nusu isiwe kama Sheffield FC bali iwe ni bora kuliko sasa.

Yanga kwa sasa ni moja ya klabu 15 zinazofanya vizuri barani Afrika. Inatakiwa juhudi na maarifa kubaki hapo au kwenda mbele zaidi. Kama klabu wajue malengo na ushindani wao ni kiwango cha Afrika zaidi kuliko ligi ya ndani.

Mashindano ya Afrika ni chanzo kizuri cha mapato kwa klabu zinazofanya vizuri.

Miundombinu ya soka, zaidi viwanja vya mazoezi na mechi limekuwa ni tatizo sugu kwa Yanga. Imefikia mahali ujenzi wa uwanja kwa Yanga limekuwa ni neno la kuombea kura kwa viongozi miaka nenda miaka rudi. Kiongozi atakayewezesha ujenzi wa uwanja wa klabu atajiweka katika vitabu vya historia ya klabu hiyo ya jangwani.

Klabu ya Yanga haijaweka mkazo wa kutosha katika soka la vijana. Miaka ya nyuma zilikuwepo program za vijana zilizoonyesha mafanikio lakini bahati mbaya zilikuwa mabegani mwa makocha Dk Victor Stanslescu na Tambwe Leya wa Romania na Zaire (Congo DR) mtawalia. Makocha walipoondoka program zikafa. Klabu kubwa duniani zinakuwa na shule za soka na mfumo wa vijana ambao ni bango la maendeleo endelevu ya klabu. Klabu kubwa haiwezi kuishi kwa kutegemea wachezaji waliolelewa na klabu nyingine peke yake. Klabu za kisasa zinachukua vijana na kuwalea hata katika umri mdogo wa miaka sita.

Ni bahati kwamba Yanga wanasherekea miaka 90 wakiwa ni mabingwa wan chi lakini wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili mwaka 2035 wawe na sherehe ya kumbukumbu ya miaka 100 yenye historia na mafanikio na si historia tu kama Sheffield FC. Hongera sana Young Africans Sports Club!


Mwandishi wa Makala haya ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.