Hussein Tindwa: Mchezaji aliyeifia simba uwanjani
Muktasari:
- Minong’ono hiyo ilihusu kifo cha Hussein Tindwa aliyekuwa mchezaji wa klabu hiyo ambaye saa chache tu zilizopita, alikuwa amevaa jezi ya timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria.
MAGHARIBI ya Mei 12, mwaka 1979, viunga vya Jiji la Dar es Salaam na hasa Mtaa wa Msimbazi yalipo Makao Makuu ya Klabu ya Simba, vilianza kupata minong’ono ya habari za simanzi.
Minong’ono hiyo ilihusu kifo cha Hussein Tindwa aliyekuwa mchezaji wa klabu hiyo ambaye saa chache tu zilizopita, alikuwa amevaa jezi ya timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria.
Hizo ni nyakati tofauti na hizi. Wakati huo hakukuwa na simu za mkononi wala mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Instagram, X, Tiktok na mingine.
Nyakati hizo, kwa uhakika kabisa, ilibidi tukio ulione kwa macho yako au uthibitishiwe na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Nchi yetu ilikuwa haina televisheni wakati huo.
Mara baada ya taarifa kuthibitishwa na RTD, ilikuwa siku ya simanzi kubwa kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi. Vilio vilihanikiza eneo lote la Msimbazi ambako mashabiki walikuwa wamekusanyika.
Kuna taarifa tofauti kuhusu ni wakati gani hasa Tindwa alipoteza uhai wake. Hata hivyo, zipo taarifa kadhaa ambazo zimethibitishwa na mashuhuda wa tukio hilo.
Mosi ni Tindwa akiwa ameanza kuaminika kama mmoja wa mabeki wa kati wa Simba mwaka 1979, alikuwa ameruka juu na mchezaji wa Racca wakiwa wanawania mpira.
Aliposhindwa kuinuka, aliyekuwa mlinzi wa kushoto wa Simba wakati ule, Mohamed Kajole alikwenda kumwangalia kujua nini kimempata. Kajole alikuta Tindwa akiwa amepoteza fahamu lakini akionyesha dalili za uhai.
Wapo mashabiki wanaoamini Tindwa alifia palepale uwanjani lakini kwa sababu ya kutotaka kuleta taharuki mchezoni, kifo kile hakikutangazwa pale.
Mmoja wa mashabiki na wanachama maarufu wa Simba hivi sasa, Mkubwa Kambi alipata kunieleza zipo taarifa pia Tindwa alipoteza uhai maeneo ya karibu na Klabu ya Simba (Mtaa wa Msimbazi) wakati anapelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Katika miaka takribani 90 ya uhai wa Simba, Tindwa ndiye mchezaji pekee aliyeingia kwenye rekodi ya kufia uwanjani katika maana yake halisi kuondoa msemo wa kawaida wa wachezaji kufia uwanjani.
Tindwa alikuwa mtu wa namna gani?
Katika simulizi za kusisimua zaidi za Klabu ya Simba, mojawapo ni ile inayohusu timu hiyo kufungwa mabao 4-0 na Mufulira Wonderers ya Zambia jijini Dar es Salaam na yenyewe kwenda kuwafunga Wazambia hao kwa mabao 5-0 jijini Kitwe, Zambia.
Unaweza ukadhani Simba ilikuwa na timu imara sana wakati huo. Lakini kwa mujibu wa maelezo aliyowahi kunipa baba yangu, marehemu Mzee Peter Kamwaga, timu haikuwa nzuri namna hiyo.
Wachezaji wanne wa kutegemewa wa Simba, akiwemo aliyekuwa jirani yetu Kurasini, Temeke, Adam Sabu, walikuwa wamefungiwa kucheza kutokana na adhabu waliyopewa na Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kutokana na kufanya fujo katika mechi ya ligi.
Ndiyo sababu kina Tindwa walipata nafasi ya kucheza kwenye mechi ile. Hata mfungaji wa mabao matatu (hat trick), Thuwein Ally, alilazimika kucheza kama namba tisa kwenye mechi ile kwa sababu ya kukosekana kwa mwenye namba yake, Jumanne Masimenti.
Nimezungumza na mchezaji bora wa wakati wote wa Simba, Abdallah Kibadeni, kuhusu Tindwa ambaye ni mchezaji aliyekuwa akimfahamu vizuri akiwa kawahi kumfundisha.
“ Nimemfundisha Tindwa wakati akiwa mchezaji wa Simba na nilipoondoka kwenda MajiMaji niliondoka naye. Alikuwa ni mchezaji msikivu ambaye alikuwa anakuja vizuri sana,” anasema.
Kibadeni anasema hakushangaa wakati Tindwa aliporudi Simba kwa sababu tayari kipaji chake kilikuwa kinafahamika. Ingawa alikuwa mzuri wa kati – kwa mujibu wa Kibadeni, alikuwa pia na uwezo wa kucheza namba nyingi uwanjani.
Kwa mujibu wa simulizi za baadhi ya watu waliokuwa karibu na shughuli za klabu wakati ule, Tindwa hakuonyesha utofauti au hali isiyo ya kawaida kabla ya mechi ile.
Taarifa zilizokuja kutolewa baadaye na madaktari, marehemu alikuwa na tatizo la moyo kwenye maisha yake yote ya uchezaji, zilikuja kama mshtuko miongoni mwa waliomfahamu.
Mwandishi wa habari, Mohamed Kuyunga ambaye amewahi kuandika kwa undani kuhusu tukio la kifo cha Tindwa, amewahi kueleza kwenye uchunguzi uliofanyika baada ya kifo cha mchezaji huyo, alionekana kuwa na moyo mkubwa ambao haukuendana na kazi ya kucheza mpira.
Akiandikia katika gazeti hili, Kuyunga alieleza madaktari walishangaa ilikuwaje Tindwa aliweza kucheza mpira kwa muda wote huo pamoja na tatizo hilo kubwa la moyo. Ni Kuyunga pia ndiye aliyeeleza moyo wa marehemu Tindwa ulifanyiwa uchunguzi maalumu na wataalamu hao ili kujifunza kitu kutoka hapo.
Kwa wapenzi wa soka wa kizazi hiki, ni rahisi kukumbuka tukio la kifo cha aliyekuwa nyota wa Cameroon, Marc Vivien Foe, kwa sababu ni kitu kilicho kwenye kumbukumbu zao na wengine waliliona mubashara wakati likitokea.
Kwa sababu hiyo, jezi ya Cameroon na namba 17 aliyokuwa akivaa Foe zimebaki kama samani za kudumu za historia ya soka ya taifa hilo.
Ni bahati mbaya Watanzania wawili tu kati ya 10 utakaopishana nao leo, ndiyo pengine ama walikuwa watu wazima au kwa namna moja au nyingine wamewahi kusikia kumhusu mchezaji huyo.
Hata picha za Tindwa zilizopo ni zile za kufifia za black and white na mashabiki wa Simba wanajua kidogo sana kumhusu.
Kwa sababu ya kumtendea haki tu na kuheshimisha dhana nzima ya wachezaji kufia uwanjani, jina la Hussein Tindwa lilikuwa linatakiwa kufahamika na kuimbwa na kila shabiki wa Simba kila kwenye mechi nyakati zote.
Simba inahitaji bendera kubwa yenye picha ya Tindwa itakayokuwa inapepea katika eneo moja la uwanja wa klabu popote pale utapojengwa. Yeye anatakiwa kubaki kuwa sehemu ya samani ya klabu kwenye uhai wote wa klabu.
Baba yangu aliniambia kilichoifanya Simba kuifunga Mufulira 5-0 nchini Zambia haikuwa kwa sababu klabu ilikuwa na kikosi bora kuliko vyote. La hasha. Sababu kubwa ilikuwa ni kikosi cha wachezaji vijana waliokuwa tayari kuipigania uwanjani na ikiwezekana kuiacha nafsi ndani ya uwanja.
Marehemu Hussein Tindwa alikuwa sehemu ya wachezaji hao. Na miezi michache baadaye, akafia uwanjani akiwa amevaa jezi ya Wekundu wa Msimbazi.
Nimemkumbuka Tindwa wiki iliyopita wakati niliposoma ujumbe ambao nahodha wa zamani wa Italia na AC Milan, Paolo Maldini, aliuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuomboleza kifo cha nahodha na pacha wake kwenye safu ya ulinzi ya Italia, Franco Baresi, pale alipoandika;
“Mi hai insegnato a lottare fino all’ultimo respire, cosa significhino l’attaccamento alla maglia e il valore” ambayo tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili angesema;
“Ulinifundisha kupambana hadi pumzi yako ya mwisho, nini thamani ya kufa na jezi yako na thamani ya kuwa kiongozi halisi”.
Jioni ile ya Mei 12, 1979, Tindwa alituacha duniani pale Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam huku jezi yake ikiwa imeng’ang’ana kwenye mwili wake.
Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari ambaye amewahi kuwa Msemaji na Katibu Mkuu wa Simba