Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Ghafla tu tumekinai udhamini

Mwesigwa Pict
Mwesigwa Pict

Muktasari:

  • Iko hadithi ya Maria Antoneitta, malkia wa mwisho wa ufalme wa Ufaransa, ambaye baada ya kuona watu wanaandamana kulalamikia njaa na ukosefu wa mkate akasema ‘Kwa nini wasipewe keki?’

Maskini akipata, makalio hulia mbwata. Kipato huleta majivuno. Aliyeshiba hamjui mwenye njaa. Misemo hii, labda na mingine hujaribu kueleza jinsi mabadiliko ya kiuchumi au ustawi wa mtu unavyoweza kumsahaulisha magumu mengi aliyopitia au kuwasahau walio katika hali kama yake ya zamani.

Iko hadithi ya Maria Antoneitta, malkia wa mwisho wa ufalme wa Ufaransa, ambaye baada ya kuona watu wanaandamana kulalamikia njaa na ukosefu wa mkate akasema ‘Kwa nini wasipewe keki?’

Soka letu limepitia kipindi kigumu sana na hata sasa hatuwezi kusema kipindi hicho kimepita kabisa.

Yanga na Simba ni klabu kongwe nchini zikikaribia umri wa miaka 90 na zimepitia mazingira magumu sana.

Siku hazigandi, wakati huu wanachekelea fadhili lukuki kiasi cha kuanza kuchagua nani awafadhili na nani asiwafadhili.

Wanasema ombaomba hapaswi kuwa mchaguzi. Nina picha ya wachezaji wa Simba wakiwa wamevaa jezi ya timu ya taifa ya Ujerumani (Magharibi) iliyotwaa ubingwa wa dunia mwaka 1990, pia nina picha ya Yanga ikiwa imevalia jezi ya Taifa stars.

MW01
MW01

Ilikuwa kawaida na hakuna aliyejali. Wafadhili kama Highway Carriers ya Azim Dewji na Bobby Soap ya Mohamed Viran walinunua jezi na kuzipiga chapa na kuwapa Simba na Yanga ambao kwao hicho kilikuwa ni kivuno.

Ni hadi miaka ya 2000, ndipo timu zilipoanza kuingia mikataba ya kuvalishwa jezi na wadhamini. Hata hivyo, starehe hiyo walikuwa nayo Yanga na simba na baadae Azam FC waliopanda daraja wakiwa na uhakika wa fedha za kuwavalisha.

Pale timu zilipoanza kuwa na uhakika wa kuvaa jezi za kwao na wadhamini kifuani, ndipo mashabiki walipoanza kuwa na uhakika na jezi inayovaliwa na timu zao kwani ule utamaduni wa kila siku kuja na jezi ambayo haikueleweka ukawa unakufa taratibu. Mashabiki nao wakaanza kuvaa jezi ili kujinasibisha na klabu zao pendwa.

Klabu za Ulaya kama Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Liverpool, Arsenal, Manchester United, Juventus, Chelsea, Manchester City na vingine vingi vimetengeneza pesa nyingi kutokana na biashara ya fulana na udhamini.

Pesa hizo ni nyingi kiasi cha kugharimia sajili za wachezaji wakubwa na mahitaji mengine.

MW02
MW02

Safari ya kutoka kutegemea ufadhili kwenda kwenye udhamini si nyepesi. Wako watu wengi waliojitolea kufadhili klabu za soka na wakaishia kufilisika. Ilifikia mahali kukawa na msemo ukitaka kufilisika basi jihusishe na ufadhili wa soka.

Mifano ipo mingi sana ingawa binadamu tumeumbwa kusahau. Yanga watakuwa wanakumbuka hali yao ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Tunaongelea Yanga iliyokataa kupokea pesa za udhamini karibu miaka 12 iliyopita ikiwa na madai kama ya wanaojiita wazee wa watani zao.

Njaa ilipoingia, walirudi shirikisho kuulizia pesa walizoapa kutopokea.

Safari ya kutoka kutegemea ufadhili haijaisha. Pengine watu wanaona soka la Tanzania katika macho ya Yanga na Simba.  Hali bado ni ngumu kwa klabu nyingi za ligi kuu na Championship.

MW04
MW04

Siyo kila timu ina fahari ya kulala kwenye hoteli ya nyota tano au kupanda ndege. Siyo kila timu ina uchaguzi wa nani awe mdhamini wake au la.

Leo inasikitisha kuna watu wanalalamika mdhamini mmoja kujihusisha na klabu nyingi za ligi kuu. Ukiwasikiliza wanaolalamika, hawana hata wazo moja la namna timu hizo zinavyoweza kujiendesha iwapo watalazimika kutafuta mdhamini asiyejihusisha na timu nyingine.

Wanaopinga kampuni moja kudhamini klabu nyingi wanasahau udhamini wa Azam kwa timu nyingi, pamoja na wao wenyewe kuwa na timu, ndiyo umepandisha kiwango cha soka nchini. Udhamini wa Azam kwa klabu zaidi ya 16 umechangia kwa kiasi kikubwa ligi ya Tanzania kuwa ya sita kwa ubora Afrika.

Jambo moja wasilolijua wanaotamani kupunguza wadhamini, ni udhamini hauna maana ya umiliki. Kampuni hutumia klabu za michezo kutangaza na kukuza biashara zao, lakini hawana maamuzi kwa kinachotokea ndani ya mchezo.

Mfano mzuri ni uwepo wa Kampuni ya Shirika la Ndege la Emirates la Umoja wa Falme za Kiarabu ambalo linazidhamini klabu kama Arsenal, AC Milan, Benfica, Real Madrid na Olympique Lyon zinazoshiriki mashindano ya mataifa yao na pia Ulaya. England, pamoja na kuidhamini Arsenal, Emirates inadhamini pia mashindano ya Kombe la FA ambalo linashirikisha Arsenal na klabu nyingine zaidi ya 90 za madaraja tofauti.

NI
NI

Uwepo wadhamini kama Azam, MO, GSM, NBC, CRDB ni jambo la heri kwa Bodi ya Ligi, TFF na soka letu kwa jumla.

Inasikitisha tunaposahau enzi ya timu kufungiwa hotelini huku wachezaji na viongozi wakiwekwa bondi kwa kushindwa kulipa bili, timu kukosa nauli kuhudhuria michezo yake na hata michezo mingi kuahirishwa kwa sababu ya kushindwa kugharimia safari.

Leo CRDB na NBC zimekwenda hatua nyingine mbele wakaweka udhamini kwa klabu moja au klabu kadhaa au hata kuanzisha klabu zao. Hili likitokea litakuwa jambo jema kwani ni raslimali zaidi zinaingia kwenye soka letu.

Hakuna shutuma zilizothibitishwa na wanaodai uwepo wa mgongano wa masilahi pale mdhamini mmoja anapodhamini klabu zaidi ya moja kwenye ligi moja. Woga huu ni matokeo ya mtazamo wa kizamani wa amlipaye mpiga zumari ndiye huchagua toni ya wimbo.

Kwa kiasi kikubwa soka letu linaendeshwa kwa weledi na hivyo Bodi ya Ligi na TFF zina uwezo wa kuhimili na kudhibiti migongano ya masilahi.

Tunapopigia kelele klabu nyingi kudhaminiwa na kampuni moja, tukumbuke si mdhamini anayezifuata hizi klabu bali anafuatwa kuombwa usaidizi.

Si kila timu ina bahati kama ya yule malikia wa Ufaransa, ya kula keki miongoni mwa wasio na muhogo wa kubebena. Si kila timu ni Yanga, Simba na Azam wenye fahari ya kushindanisha wadhamini. Bado tunahitaji sana wadhamini. Wadhamini ni washirika, wadhamini si wamiliki, wadhamini hawapangi vikosi au kuamua mchezo, wadhamini wanawezesha mazingira bora ya uendeshaji wa soka.


Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).