Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NINAVYOJUA : Waandishi wasiwageuze chambo Julio, Minziro

Muktasari:

Wengi wamekuwa wakitamani kumuona jinsi atakavyopambanua hoja mbalimbali pale atakapokuwa anaulizwa maswali na waandishi wa habari kwa sababu amekuwa kivutio sana katika kujibu maswali hayo.

MASHABIKI wengi wa soka wamekuwa na hamu kubwa ya kumuona kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wa Mwadui atakavyoweza kuifanya kazi yake ndani ya kikosi hicho baada ya miaka mingi kujipatia umaarufu akiwa Simba.

Wengi wamekuwa wakitamani kumuona jinsi atakavyopambanua hoja mbalimbali pale atakapokuwa anaulizwa maswali na waandishi wa habari kwa sababu amekuwa kivutio sana katika kujibu maswali hayo.

Hayupo pekee yake, pia kuna kocha mwingine mzoefu na mwingi wa maneno, Fred Felix Minziro ambaye japo si muongeaji sana kwenye vyombo vya habari lakini ni mmoja kati ya makocha ambao huwa na aina fulani ya misimamo katika kusimamia kazi yake.

Ni kocha mwenye ujasiri sana katika kuhakikisha anapigania uwezo wa kazi yake. Yeye na Julio ni baadhi ya makocha wachache waliowahi kuzichezea Simba na Yanga na kuendelea kubaki midomoni mwa wadau wa soka nchini.

Wengine ni kina Boniface Mkwasa, Mbwana Makata, Joseph Lazaro, Mrage Kabange na Abdallah Kibadeni kwa bahati mbaya sana watu wengi bado wana dhana potofu juu ya wao kufundisha timu nyingine nje ya Simba na Yanga.

Kumekuwa na hisia mbaya hasa timu zao zinapokuwa zinakutana na timu zao za zamani, watu wanadhani Julio hawezi kufanya lolote licha ya kuwa Mwadui pale atakapovana na Simba, zaidi ya kufungwa, kitu ambacho si sahihi na wala hakuna kocha yeyote duniani anayeweza kufanya hivyo. Dhana hiyo imejengeka pia vichwani mwa Wanahabari ambao baada ya kuyasikia kwa watu wengine ambao hawajawahi kuwa na ushahidi wa hayo, na kutumia kama njia ya kuulizia maswali yao kwa makocha hao wawili yaani Julio na Minziro. Maswali hayo kimsingi huwa hayana mashiko na mengine yanasikika vibaya kwenye masikio ya wapenda soka hapa nchini, unajiuliza mwandishi wa habari anamuuliza vipi Fred Felix kwamba’ kocha inasemekana umeshangilia kimya kimya leo ulivyofungwa na Yanga!

Hii ilikuwa ni siku ambayo Yanga iliifunga JKT mabao 4-1, hili ni swali linalotoka kwa mwandishi wa habari ambaye kila mara amekuwa akihudhuria michezo ya ligi siku zote, anaanza vipi kumuuliza kocha kitu asichokuwa na uhakika nacho wala ufahamu mzuri? Au mwandishi wa habari anamuuliza kocha Jamhuri baada ya kocha huyo kuwa amemweleza sababu za uhalisia wa jinsi bao walilofungwa na Azam lilivyotokea, akioanisha na upepo mkali uliokuwapo uwanjani kuwa namna moja ama nyingine uliyumbisha mwendo wa mpira angani na kumfikia mfungaji. Mwandishi anajaribu kulinganisha penati iliyokoswa na Rashid Mnadawa mchezaji wa Mwadui kuwa nayo ilitoka nje sababu ya upepo? Yapo maswali mengi ambayo kwangu nayaona siyo maswali yenye busara na kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwadhalilisha makocha hawa na kuwapunguzia ari ya kufundisha soka hapa nchini.

Wanahabari na wadau wengine wa soka wanatakiwa kujua kuwa ukocha wa soka si kazi rahisi na lelemama, ni kazi inataka utashi wa mtu kweli kweli kwa mazingira ya nchi hii unapomuona kocha anafundisha timu inatakiwa apongezwe.

Kwa mtu yeyote anayefundisha mpira jua anaifundisha timu hiyo kwa moyo wote, hakuna kocha duniani anayependa kufungwa!

Licha ya Julio au Minziro walizichezea Simba na Yanga, lakini hivi leo maadili na mapenzi ya kazi zao yanawafanya wawe na furaha kubwa pale wanapofanikiwa kuzifunga timu hizo. Haya yameshatokea mara nyingi huko nyuma na yataendelea kutokea, Kocha Abdallah Kibadeni akiwa na Nyota Nyekundu, Majimaji na Kagera Sugar amekuwa akizifunga sana timu hizo za Simba na Yanga na siku alipoifunga Simba akiwa na Kagera Sugar misimu miwili iliyopita alitamka wazi wazi kuwa yupo kikazi zaidi na siyo mapenzi. Miaka ya 1990 wakati Mkwasa alipoachishwa kazi Yanga na aliibukia Sigara ambapo katika mchezo uliofuata Sigara hiyo ya Mkwasa iliifunga Yanga mabao 3-1 huku yeye akitamka alipohojiwa kuwa ukitaka kumuua nyoka usimtazame usoni.

Minziro ameifunga Yanga akiwa na timu mbalimbali, aliwahi kuifunga Yanga bao 2-0 akiwa anaifundisha timu ya Polisi-Zanzibar kwenye Ligi ya Muungano, huku Julio alipoifundisha Kajumulo alizisumbua sana Simba na Yanga. Hii inadhihirisha kuwa kila kocha anapenda mafanikio na mafanikio hayaji kirahisi kama hutopata ushindi kwa kila mchezo, ndio maana nasema tuwape heshima zao makocha wetu hawa wazalendo.