Ni lini kanda ya Cecafa itacheza Afcon?
Muktasari:
Yaani kazi yetu imekuwa kuwashangilia wenzetu tunapozidi kufuatilia fainali hizo kwenye runinga, mitandao, redioni na katika vyombo vingine vya habari kwani kanda yetu haina hata timu moja inayotuwakilisha huko.
KWA mara nyingine mataifa wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), tumebaki kuwa watazamaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea kule Equatorial Guinnea.
Yaani kazi yetu imekuwa kuwashangilia wenzetu tunapozidi kufuatilia fainali hizo kwenye runinga, mitandao, redioni na katika vyombo vingine vya habari kwani kanda yetu haina hata timu moja inayotuwakilisha huko.
Hakuna tunayeweza kujivunia kuwa ni ndugu yetu huko ili tumpe sapoti. Swali langu ni kwa viongozi wa soka wa kanda hii, Je, tutazidi kuwa watazamaji tu mpaka lini? Hivi tatizo letu la kutoshiriki fainali hizi linatokana na nini ndugu zanguni?
Haya ni maswali ambayo kwa kweli yamejaa katika vinywa vya wapenzi wa soka. Hivi karibuni nilipokuwa jijini Dar es Salaam ndani ya Uwanja wa Taifa nikitazama mechi baina ya Yanga na JKT Ruvu, dada mmoja mwandishi wa habari aliniuliza nini shida yetu kiasi cha kutoshiriki Afcon. Ilinibidi nipunge hewa kidogo kutafuta jibu sahihi la kumpa.
Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu kanda hii ina wachezaji mahiri kabisa wa soka, lakini tatizo linaonekana kuwapo kwa viongozi ambao wameweka mbele shibe zao badala ya kuendeleza soka. Ndiyo maana maandalizi yetu kila mara huwa ni duni.
Nimewahi kuwa Afrika Kusini, Nigeria, Congo, CapeVerde pamoja na sehemu nyingine kadhaa, hawana wachezaji wa maana sana kuliko sisi. Lakini jamaa hawa wanatushinda kwa sababu wanafanya maandalizi mazuri, huwa na mechi nyingi za kujipima nguvu tofauti na sisi.
Viongozi wa soka katika nchi zetu kazi yao kulalamika hakuna fedha, tunaishia kucheza na Somalia wakati Ivory Coast inakipiga na Hispania au Algeria wapo Ufaransa huku Congo wakiwa Italia zikicheza mechi za kujipima nguvu, kwa mtaji huo tutafika?
Mabosi wetu wa soka kwa kuwapunja wachezaji posho zao wapo mstari wa mbele, soka letu limejaa malumbano kila kukicha na kambi zetu ndiyo usiseme yaani zimejaa madeni makubwa.
Tanzania imewahi kushiriki Afcon mara moja tu, mwaka 1980. Kuna wasomaji wengi wa safu hii walikuwa hawajazaliwa. Uganda mara ya mwisho kucheza Afcon ilikuwa mwaka 1978, Kenya angalau kidogo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2004 , lakini imeshapita miaka kumi.
Lakini cha ajabu viongozi wetu hawaishi kutamba eti wameendeleza kiwango cha soka. Jamani ukitaka kuvuna ni lazima upande mbegu, kisha unyunyuzie mbolea, umwagilie, upalilie na unyunyuzie dawa ya kuua wadudu. Kumbuka malumbano yaliyotokea kambi ya Nigeria yamewafanya mwaka huu wakose fainali za Afrika.
Pia, tuna tatizo la ukosefu wa viwanja. Mfano Kenya tuna uwanja mmoja tu unaoweza kuandaa fainali za Afcon, Moi International Sports Centre Kasarani. Tanzania nao wana mmoja tu, Uwanja wa Taifa sawa na Uganda wenye Nelson Mandela Stadium pekee.
Ili kuwa mwenyeji wa Afcon, ni lazima nchi iwe na zaidi ya viwanja sita vya kimataifa. Hata kwa jumla wetu Afrika Mashariki hatuwezi kuwa wenyeji wa Afcon. Hata kwenye hoteli nako tuna matatizo.
Jingine linalotuponza ni pangapangua ya makocha wa timu zetu za taifa. Kila kukicha makocha wanabadilishwa na hivyo timu zinakosa mwendelezo wa ufundi, lakini Afrika Kaskazini au Magharibi hawafanyi hivyo mara kwa mara.
Tunapobadili ovyo makocha, nao hubadili ovyo wachezaji na matokeo yake ndio haya, tupo hapa hapa siku zote. Inafaa kocha apewe muda mrefu kutengeneza kikosi kizuri, angalau miaka miwili isipungue kwa kocha kuunda kikosi tena akiwa amepewa ushirikiano wa kutosha na shirikisho la soka. Kocha anapaswa kuachiwa uhuru wa kuchagua kikosi. Tuache mambo ya kumlazimisha kocha ampange fulani. Jamani, hebu tukae chini na tufikirie nini haswa tunapswa kufanya ili tuweze angalau kupeleka timu moja Afcon. Inaweza kuwa Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda au hata Burundi. Kama hatuwezi kufuzu huku basi tujenge viwanja ili angalau tuambulie kuwa wenyeji.