Nani kubeba Bundesliga? Hawa wanashuka daraja!
Muktasari:
- Maswali hayo na mengine yanajibiwa kupitia utabiri wa Opta wa msimu wa Bundesliga 2026/27 uliofanywa kabla ya ligi hiyo kuanza jana usiku, ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich waliwakaribisha VfB Sttuttgart kwenye Uwanja wa Allianz Arena.
MUNICH, UJERUMANI: JE, Bayern Munich wanaweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga)? Ni timu zipi zitafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya? Na je, klabu zilizopanda daraja zinaweza kuepuka kushuka?
Maswali hayo na mengine yanajibiwa kupitia utabiri wa Opta wa msimu wa Bundesliga 2026/27 uliofanywa kabla ya ligi hiyo kuanza jana usiku, ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich waliwakaribisha VfB Sttuttgart kwenye Uwanja wa Allianz Arena.
Vincent Kompany ameiongoza Bayern Munich kutwaa ubingwa katika misimu yake yote miwili akiwa kocha, na utawala wao hauonekani kupungua nguvu.
Walitwaa ubingwa 2025/26 mwezi mmoja kabla ya msimu kumalizika, huku pia wakimaliza kusubiri kwao kwa miaka sita kutwaa tena DFB-Pokal baada ya kuifunga Stuttgart katika fainali.
Bayern wameongoza kubeba Bundesliga katika misimu 13 kati ya 14 iliyopita, na msimu pekee ambao walikosa ubingwa ulikuwa wa 2023/24 wakati Bayer Leverkusen ya Xabi Alonso ilipowanyamazisha. Hivyo, kwa mara nyingine tena, Bayern ndiyo timu inayotajwa kuwa ya kuangaliwa zaidi.
Borussia Dortmund walikuwa na matumaini katikati ya msimu uliopita kwamba wangeweza kuwapindua wapinzani wao hao wakubwa, lakini hatimaye walishindwa na kumaliza wakiwa mbali na kilele cha msimamo. RB Leipzig, Stuttgart na Hoffenheim, ambao walishangaza walimaliza wakiwa nyuma zaidi.
Heidenheim na St Pauli zote zilishuka daraja, huku Wolfsburg, ambao wamekuwa sehemu ya Bundesliga kwa muda mrefu, nao wakishuka baada ya kufungwa mabao 2-1 na Paderborn katika michezo miwili ya mchujo wa kupanda na kushuka daraja. Schalke na Elversberg ndizo timu zilizopanda na kurejea au kuingia Bundesliga.
Kwa hiyo, simulizi za msimu wa 2026/27 zitakuwa zipi? Je, kuna timu inayoweza kutoa upinzani mkali dhidi ya Bayern katika mbio za ubingwa au vijana wa Kompany watatwaa taji la 36 katika historia ya klabu? Na ni timu zipi zinaweza kujikuta zikivutwa kwenye vita vya kushuka daraja? Twende pamoja.
NANI KUTWAA UBINGWA?
Kwa mara nyingine, Bayern Munich wanatarajiwa kutawala Bundesliga msimu huu, na inaonekana kuwapo kwa uhakika mkubwa kuhusu hilo baada ya kuona Rekordmeister wakitwaa ubingwa kwa urahisi katika misimu miwili iliyopita.
Bayern walitangazwa mabingwa msimu wa 2025/26 tangu Aprili 19, na kuwa moja ya timu zilizowahi kutwaa ubingwa mapema zaidi katika historia ya Bundesliga, baada ya kufikia ubingwa huo huku zikiwa zimesalia mechi nne.
Bayern pia waliweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa Bundesliga wakitupia nyavuni mara 122. Hakuna timu nyingine Ulaya iliyofikisha hata mabao 100, huku Barcelona ikiwa ndiyo iliyokaribia zaidi kwa kufunga 95.
Kikosi hicho cha Kompany kilionekana kutoshikika msimu uliopita kikimaliza kikiwa na tofauti kubwa ya pointi 16 dhidi ya Dortmund iliyomaliza nafasi ya pili.
Bayern walipoteza mchezo mmoja tu walipofungwa kwa kushangaza mabao 2-1 na Augsburg mwezi Januari. Kwa hiyo, haishangazi kwamba Opta inawapa nafasi kubwa zaidi vya kutwaa ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo, ikiwa na uwezekano wa asilimia 76.7.
Tayari wameanza vyema msimu wa 2026/27 baada ya kuifunga Dortmund 2-1 na kutwaa Franz Beckenbauer Supercup ambayo ni sawa na Ngao ya Jamii huku kwetu, jambo ambalo watatumaini kuwa ishara nzuri kuelekea msimu mpya.
Bayern walipoteza pointi katika michezo sita pekee msimu uliopita wakitoka sare mara tano na kupoteza mchezo mmoja, huku wakishinda mara 28. Pia waliongoza katika takwimu za mabao yaliyotarajiwa wakiwa na 100.9 xG, huku Dortmund ikiwa timu pekee iliyofungwa machache kuliko Bayern baada ya kuruhusu 34 dhidi ya 36 ya Bayern.
Pia bado wana safu hatari ya ushambuliaji inayowajumuisha Harry Kane, Luis Díaz na Michael Olise, huku Ismael Saibari akiongezwa kwenye orodha hiyo. Nathaniel Brown pia ni mchezaji mpya aliyeng'ara katika mechi za maandalizi ya msimu.
Bayern wamepewa uwezekano wa asilimia 98.4 wa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, kombe ambalo Kompany anatamani kuliongeza kwenye mafanikio yake. Inaonekana ubingwa wa Bundesliga uko mikononi mwa Bayern.
Lakini je, kuna timu inayoweza kuvuruga utawala huo? Dortmund wanatarajiwa kuwa miongoni mwa timu zitakazowania nafasi za juu baada ya kufanya vizuri kwa kiwango cha kuridhisha msimu uliopita. Wakiingia katika msimu wa pili kamili chini ya kocha Niko Kovac, Dortmund wana uwezekano wa asilimia 8.7 wa kuwapita Bayern na kumaliza kileleni.
Hata hivyo, nafasi yao inayotabiriwa zaidi ni kumaliza nafasi ya pili, wakiwa na uwezekano wa asilimia 23.0. Wanaofuatia ni Bayer Leverkusen, ambao sasa wanafundishwa na Carles Martínez baada ya msimu wa 2025/26 wenye misukosuko ambapo walibadilisha makocha mara mbili.
Leverkusen wana uwezekano wa asilimia 5.0 wa kutwaa ubingwa wa pili ndani ya misimu minne. Ubingwa wao wa mwisho pia ulipatikana chini ya kocha Mhispania Xabi Alonso. Ni timu nyingine nne pekee zinazopewa zaidi ya asilimia moja ya uwezekano wa kutwaa taji la Bundesliga.
Leipzig wanaongoza kundi hilo kwa uwezekano wa asilimia 2.71 wakiwa mbele kidogo ya Stuttgart kwa asilimia 2.67, licha ya Stuttgart kutabiriwa kumaliza juu ya timu ya Martin Demichelis katika msimamo. Hoffenheim wanapewa uwezekano wa asilimia 1.19, huku Freiburg ikiwa na 1.13.
KUFUZU LIGI YA MABINGWA
Kama inavyoelezwa, Bayern wana uwezekano mkubwa wa kufuzu Ligi ya Mabingwa kama kawaida, huku Borussia Dortmund (BVB) ikiwa na uwezekano wa asilimia 62.2 wa kuungana nao.
BVB wamefuzu Ligi ya Mabingwa katika kila mmoja wa misimu 14 iliyopita. Usajili wao katika dirisha hili haukuwa wa kuvutia sana, hata baada ya kumpoteza Karim Adeyemi, wanatarajiwa kuendeleza rekodi.
Kuna uwezekano wa asilimia 9.8 wa Dortmund kushuka hadi nafasi ya kufuzu Europa League, huku ikiwa na uwezekano mwingine wa asilimia 7.3 wa kulazimika kucheza Conference League.
Jambo ambalo Kovac atataka kuliendeleza ni kiwango bora cha ulinzi, kwani waliruhusu mabao machache zaidi Bundesliga msimu uliopita. Hata hivyo, tatizo la Dortmund linaweza kuwa ni wapi watapata mabao, hasa iwapo Serhou Guirassy ataondoka kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Leverkusen watashiriki Europa League msimu huu baada ya msimu wao mgumu wa 2025/26, lakini wanatarajiwa kurejea Ligi ya Mabingwa. Wanapewa uwezekano wa asilimia 52.6 wa kumaliza ndani ya nne bora.
Tayari wana mwanzo mzuri msimu huu baada ya kuifunga Wehen Wiesbaden ya daraja la tatu kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza chini ya Martínez kwenye DFB-Pokal.
Hata hivyo, mbio za nafasi ya mwisho ya kufuzu Ligi ya Mabingwa zinatarajiwa kuwa kali, huku wakitenganishwa na Stuttgart na Leipzig kwa tofauti ndogo.
Stuttgart wanatarajiwa kumaliza ndani ya nne bora kwa asilimia 39.4, wakati timu hiyo ya kocha Demichelis itafanya hivyo katika asilimia 37.2, licha ya kuwa na uwezekano mdogo wa kutwaa ubingwa.
Kwa hiyo, inatarajiwa kushuhudiwa ushindani mkali wa nafasi za Ligi ya Mabingwa, huku timu kadhaa zikiwa na nafasi ndogo ya kuvuruga mpangilio unaotarajiwa.
Hoffenheim walikuwa miongoni mwa timu zilizoshangaza katika mbio za nne bora msimu uliopita, na hatimaye walimaliza wakiwa pointi moja tu nyuma ya nafasi hiyo na kupata nafasi ya kucheza Europa League.
Uwezekano wao wa kuboresha nafasi hiyo ni asilimia 22.0, ukiwa juu kidogo ya Freiburg waliomaliza wakiwa washindi wa pili wa Europa League msimu uliopita. Freiburg wana uwezekano wa asilimia 21.6 wa kumaliza ndani ya nne bora.
Mainz pia wana nafasi nzuri ya asilimia 15.9 ya kumaliza ndani ya nne bora. Kwa kuwa ushindani wa nafasi za Ligi ya Mabingwa unatarajiwa kuwa mkali, uwezekano wa baadhi ya timu kushuka hadi Europa League pia unastahili kuangaliwa.
Stuttgart wana uwezekano mkubwa zaidi wa kucheza Europa League, wakiwa na asilimia 11.0, huku Leipzig wakiwa na asilimia 10.8. Leverkusen pia wana uwezekano wa asilimia 10.6 wa kumaliza nafasi ya tano au sita.
NANI KUSHUKA BUNDESLIGA?
Schalke wamerejea Bundesliga kwa mara ya kwanza tangu 2021, huku Elversberg wakicheza ligi ya juu kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kumaliza nafasi ya pili katika 2. Bundesliga. Paderborn nao waliimaliza safari ya Wolfsburg ya miaka 29 katika Bundesliga baada ya bao la Laurin Curda dakika ya 10 ya muda wa nyongeza katika mchezo wa pili wa mchujo kati ya timu zilizokuwa Bundesliga na 2. Bundesliga (sawa na Daraja la Pili).
Hata hivyo, wanatarajiwa kupata wakati mgumu. Paderborn wamewekewa alama za kuwa timu ya pili yenye uwezekano mkubwa wa kushuka daraja, ikiwa ni asilimia 23.2, nyuma ya Schalke yenye asilimia 24.5.
Schalke watatumia uzoefu pamoja na mabao ya mshambuliaji mkongwe Edin Dzeko wakiwaamini yatawasaidia katika harakati za kubaki Bundesliga, baada ya kumsajili tena mapema msimu huu.
Kwa upande mwingine, Schalke wana uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza nafasi ya 16 na kucheza mchujo wa kubaki Bundesliga. Uwezekano wao wa kufika nafasi hiyo ni asilimia 10.3, ukiwa juu kuliko timu nyingine yoyote. Elversberg wako nyuma kidogo kwa asilimia 10.2.
Kwa mujibu wa Opta, Elversberg wana nafasi kubwa zaidi ya kubaki Bundesliga miongoni mwa timu zilizopanda daraja, ingawa bado wana uwezekano wa asilimia 22.9 wa kushuka.
FC Koln walimaliza nafasi ya 14 msimu uliopita, lakini walifungwa mabao 63, idadi ya nne kwa wingi zaidi katika Bundesliga. Timu mbili kati ya zilizowafunga mabao mengi zaidi kuliko wao zilishuka daraja, hivyo watatakiwa kuboresha safu ya ulinzi. Koln wanatarajiwa kushuka daraja wakipewa asilimia 21.9.
Kwa upande mwingine, Werder Bremen waliomaliza nafasi ya 15 msimu wa 2025/26 wakiwa pointi tatu tu juu ya Wolfsburg waliomaliza chini yao, wanatarajiwa tena kujikuta katika vita vya kushuka daraja. Wana uwezekano wa asilimia 20.2 wa kushuka moja kwa moja, huku Hamburg ikiwa nyuma kidogo kwa asilimia 20.1.
Union Berlin pia ni miongoni mwa timu zinazoweza kuvutwa kwenye vita vya kushuka daraja, ingawa uwezekano wao wa kushuka ni mdogo zaidi, ukiwa asilimia 14.3.
Union Berlin walianza vizuri msimu uliopita kabla ya kushuka hadi eneo la hatari kutokana na matokeo mabaya mwishoni mwa msimu. Kocha wao mpya, Mauro Lustrinelli, atataka kujiimarisha zaidi ili kuepuka kumaliza msimu mwingine kwa presha kubwa.